Lydia
Churi-Mahakama, Sumbawanga
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji, Naibu Wasajili, Watendaji na
Mahakimu wote nchini kutumia mamlaka yao ya usimamizi kuhakikisha wanakagua mfumo
wa kusajili na kuratibu mashauri (JSDS II) ili kuona namna mashauri yanavyosajiliwa
na kurekebisha endapo kuna makosa.
Jaji Mkuu ametoa agizo
hilo kufuatia hatua ya Mahakama ya Tanzania ya kuamua kufanya shughuli zake kwa
kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama) na kutaka kuacha kupokea
takwimu zake kwa njia ya makaratasi na badala yake, itakuwa ikizisoma takwimu hizo kwa njia ya
mtandao.
“Mwaka huu utakuwa ni
mwaka wa mwisho kwa Mahakama kupokea takwimu kwenye makaratasi, tutakuwa tukizisoma
moja kwa moja kwenye mtandao”, alisema Jaji Mkuu alipokuwa akizungumza na
Waandishi wa Habari wakati akifanya majumuisho ya ziara yake ya kikazi ya siku
tatu katika mikoa ya Songwe na Rukwa.
“Lengo ni kwenda katika
Mahakama ya karne ya 21, Mahakama inayotegemea zaidi mtandao kuliko kutegemea
makaratasi”, alisema.
Alisema mfumo wa kusajili
na kuratibu mashauri utawawezesha viongozi wa Mahakama kujua ni mashauri
mangapi yamesajiliwa nchini, mangapi hayajapangiwa Majaji na Mahakimu, na
mangapi yamezidi muda wa kuwepo Mahakamani na hivyo kufuatilia kwa urahisi.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
mfumo wa JSDS II utasaidia kuzidisha uwazi katika shughuli za Mahakama na
kuongeza imani zaidi ya wananchi kwa Mhimili huo.
Alisema Mahakama imedhamiria kuingia
katika Tehama ambapo mwezi Julai mwaka huu iliingia Mkataba wenye thamani ya
Sh. bilioni 4.1 na Shirika la Mawasiliano ya Simu Tanzania (TTCL) utakaowezesha
Mahakama kuingizwa kwenye Mkongo wa Taifa wa Mawasiliano ambapo majengo
157 ya Mahakama nchini yataunganishwa.
Mkataba huo utawezesha kuunganishwa kwa
majengo ya Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani, Mahakama Kuu,
Mahakama za Hakimu Mkazi, Mahakama za Wilaya na baadhi ya Mahakama za
Mwanzo zenye majengo ya kisasa.
Mahakama zitakazounganishwa kwenye mtandao huo ni Mahakama ya Rufani 1,
Mahakama Kuu 16, Mahakama Kuu Maalumu (Specialized Division 4, Mahakama
za Mkoa 29, Mahakama za Wilaya 112 na Mahakama za Mwanzo 10.
Alizitaja faida za
Mahakama kusajili mashauri kwa njia ya mtandao kuwa ni pamoja na kuwasaidia mwananchi
mwenye shauri Mahakama kufahamu mwenendo mzima wa shauri kwa kujua kila hatua
ya shauri lake kwa kufahamu hatua zinazofuata kwenye shauri lake kupitia
mtandao.
Jaji Mkuu amehitimisha
ziara yake ya kikazi katika mikoa ya Songwe na Rukwa ambapo alikagua shughuli
mbalimbali za Mahakama ikiwemo miradi ya ujenzi wa majengo ya mahakama na hali
ya utoaji haki kwa ujumla. Katika ziara hiyo, Jaji Mkuu alikagua ujenzi wa
majengo ya Mahakama za Mwanzo za Mlowo mkoani Songwe na Mahakama za Mwanzo za Msanzi
na Laela mkoani Rukwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akikagua shughuli za Mahakama katika Mahakama ya Mwanzo Sumbawanga mjini. kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrango na katikati ni Mkurugenzi Msaidizi wa Tehama wa Mahakama ya Tanzania, Machumu Essaba.
Jaji
Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akikagua ukarabati Mkubwa wa Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrango (wa pili kushoto) akiongozana na Jaji Mkuu kukagua ukarabati mkubwa wa Jengo la Mahakama Kuu Sumbawanga. Kulia ni Mtendaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Leonard Magacha akifuatiwa na Mtendaji wa Kanda ya Sumbawanga, Emmanuel Munda.
Jengo la Mahakama ya Mwanzo Laela Sumbawanga likiwa katika hatia za umaliziwaji.
Jengo la Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Sumbawanga likiwa katika ukarabati Mkubwa unaoendelea.
Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga wakimsikiliza Jaji Mkuu.
Jaji
Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kushoto) akizungumza na Watumishi wa Mahakama Kuu kanda ya Sumbawanga. Kushoto ni Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Sumbawanga Mhe. David Mrango na
kulia ni Jaji wa Kanda hiyo Mhe. Willbard Mashauri.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni