Ijumaa, 1 Novemba 2019

JAJI MKUU: MSIKUBALI KUINGILIWA KATIKA MAMLAKA ZENU



Na Mary Gwera, Mahakama

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewaasa Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya kutokubali maelekezo ya aina yoyote kutoka nje ya Mamlaka zao kuhusiana na mashauri yaliyopo mbele yao.

Akizungumza na Mahakimu Wakazi hao ,wapya 23 mara baada ya kuwaapisha rasmi, mapema Novemba 01, 2019 katika Ukumbi wa Mahakama ya Rufani-Dar es Salaam, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa Mahakimu hao wana mamlaka ya kusikiliza na kuamua mashauri bila kuingiliwa na yeyote.

“Jaji au Hakimu lazima awe ni mtu wa kuheshimu mamlaka nyingine, vivyo hivyo msikubali maelekezo ya aina yoyote kutoka nje ya Mahakama ama iwe Jaji au mtu mwingine kuhusiana na kesi/mashauri yaliyopo mbele yenu,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.

Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kwa kuwataka Mahakimu hao kutekeleza majukumu yao bila upendeleo kwa kuwa ni jambo linalosababisha matabaka baina ya watu/wananchi.

“Upendeleo ni jambo la hatari sana, muwe wawazi, muwe wasikilizaji makini, lazima muwasaidie wananchi ambao wengi hawajui sheria kwa kuwaelimisha,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Hali kadhalika, Mhe. Jaji Mkuu aliwapa angalizo Mahakimu hao juu ya uandishi wa hukumu sahihi kwa kutumia lugha inayoeleweka ili wananchi/wateja waweze kuelewa kwa urahisi.

Masuala mengine aliyowaeleza Mahakimu hao ni pamoja na kufanya tafiti, matumizi ya TEHAMA na kuishi viapo vyao wanapotekeleza majukumu yao. 

Jumla ya Mahakimu Wakazi wapya 23 wameapishwa na wamepangiwa kufanya kazi katika Mahakama za Mwanzo katika mikoa mbalimbali nchini.

Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwaapisha Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya  leo Novemba Mosi, mwaka huu katika ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo jijini Dar es Salaam. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Beatrice Mutungi.
Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya wakila kiapo cha kuitumia kazi yao leo Novemba Mosi, mwaka huu, katika ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo jijini Dar es Salaam.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza na Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya leo Novemba Mosi, mwaka huu katika ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwaapisha. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na kulia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Beatrice Mutungi.
Baadhi ya Viongozi na Maafisa wa Mahakama ya Tanzania na wageni waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.
Baadhi ya Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na wageni waalikwa wakiwa katika hafla hiyo.
Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu (hayupo pichani)  leo Novemba Mosi, mwaka huu, katika ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwaapisha.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof.Ibrahim Hamis Juma (wa pili kushoto) akiwa katika picha ya pamoja na  baadhi ya Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya aliowaapisha  leo Novemba Mosi, mwaka huu katika ukumbi namba mbili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, iliyopo jijini Dar es Salaam mara baada ya kuwaapisha. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, kulia wa pili ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe Beatrice Mutungi na wa kwanza kulia ni Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati.
Baadhi ya wageni waliaalikwa wakiwa katika picha ya pamoja na Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo aliyeapishwa leo.

Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Katarina Revocati akizungumza na  Mahakimu Wakazi wa Mahakama za Mwanzo wapya walioapishwa leo.

(Picha na Magreth Kinabo- Mahakama)


 

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni