Na
Magreth Kinabo na Mary Gwera, Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji wapya wa Mahakama Kuu ya Tanzania
kuwa sehemu ya maboresho yanayoendelea kufanyika ndani ya Mahakama.
Akifungua rasmi Mafunzo
elekezi ya awamu ya tano (5) kwa Wahe. Majaji 12 walioteuliwa na Mhe. Rais hivi
karibuni, Mhe. Jaji Mkuu aliwaeleza Majaji hao kuendeleza maboresho ikiwa ni
pamoja na kutoa haki kwa wananchi bila kuangalia maeneo waliyopo.
“Mahakama ya Tanzania
kwa sasa ipo katika utekelezaji wa Mpango Mkakati wake wa miaka mitano (5)
pamoja na Mradi wa Maboresho ya Huduma za Mahakama (CCP), kwa sasa utekelezaji
wake upo katika mwaka wa tatu (3) hivyo nawaalika kuwa sehemu ya muendelezo wa
utekelezaji wa maboresho hayo,” alisema Mhe. Jaji Prof. Juma.
Mafunzo hayo yanayofanyika
katika Kituo cha Mafunzo na Habari za Kimahakama Kisutu yamefunguliwa rasmi na
Mhe. Jaji Mkuu mapema Novemba 18 mwaka huu.
Mbali na hilo, Mhe.
Jaji Mkuu aliwataka Majaji hao pia kuzingatia dira na dhima za Mahakama ya
Tanzania kwa kuwataka kutoa haki kwa wote na kwa wakati bila upendeleo.
“Mnapotekeleza majukumu
yenu msikubali kuingiliwa na mtu yeyote iwe rafiki, mwanafamilia au hata Jaji
Mwandamizi juu ya mashauri yaliyopo mbele yenu kwani yapo chini ya mamlaka zenu
kikatiba,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.
Aliendelea kwa kuwataka
Majaji hao kusoma na kuzingatia Kanuni za Mwenendo kwa Maafisa wa Mahakama ‘Code of Conduct for Judicial Officers in
Tanzania, 1984’ zitakazowaongoza katika utendaji kazi na vilevile
kusimamia na kuviishi viapo vyao.
Awali akimkaribisha
Mhe. Jaji Mkuu kufungua rasmi Mafunzo hayo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer
Mbuki Feleshi alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kukubali kuruhusu kufanyika kwa mafunzo
hayo yatakayoleta tija kwa Majaji hao.
Mhe. Jaji Kiongozi
alisema kwa sasa kuna jumla ya Majaji wa Mahakama Kuu 77 ambao kwa wastani kila
Jaji anatakiwa kusikiliza jumla ya kesi 518 kwa mwaka na kuongeza kuwa ingawa idadi hiyo inaonekana
ni kubwa jitihada mbalimbali zinaendelea kufanyika zikiwemo za kitaaluma bila
kuathiri utoaji wa haki.
“Nina imani kwamba uelewa
na uzoefu mkubwa walionao Majaji hawa wapya pamoja na mafunzo wanaoenda
kupatiwa yatawawezesha kutoa mchango katika safari ya Mahakama kuelekea
Mahakama mtandao ‘e-Judiciary’, kutoa haki kwa viwango vinavyotakiwa na kuwa
wawajibikaji wazuri,” alieleza Mhe. Jaji Kiongozi.
Mafunzo ya aina hii
yamekuwa yakitolewa kwa Majaji wapya ambapo hupata fursa ya kujengewa uwezo na
wabobezi mbalimbali wakiwemo Majaji Wakuu Wastaafu, Majaji wa Rufani na wa
Mahakama Kuu waliokwisha staafu.
Katika mafunzo hayo
kutakuwa na wawezeshaji mbalimbali wakiwemo Majaji waliopo kazini na Wataalamu kutoka
Taasisi kadhaa katika sekta ya Sheria na Utumishi wa Umma.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwasilisha hotuba ya ufunguzi rasmi wa Mafunzo
elekezi kwa Wahe. Majaji wapya wa Mahakama Kuu.
Sehemu ya Wahe. Majaji
wapya wakimsikiliza Mhe. Jaji Mkuu alipokuwa akifungua rasmi mafunzo.
Jaji Kiongozi, Mahakama
Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi akizungumza katika Mafunzo
hayo.
Mkuu wa Chuo cha
Uongozi wa Mahakama-Lushoto, Mhe.Jaji Dkt. Paul Kihwelo akizungumza wakati wa
Mafunzo hayo.
Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto, Mhe. Jaji Dkt. Gerald Ndika
akitoa kwa Wahe. Majaji katika Mafunzo hayo.
Meza Kuu: Katikati ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, wa pili kushoto ni Mwenyekiti wa Baraza la
Uongozi wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama-Lushoto, ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani, Mhe. Dkt. Gerald Ndika, wa pili kulia ni Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi, wa kwanza kulia ni Jaji Mstaafu wa Mahakama Kuu, Mhe. Rose Teemba na wa kwanza kushoto ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Beatrice Mutungi.
Meza kuu katika picha
ya pamoja na Wahe. Majaji wapya wanaoshiriki katika Mafunzo elekezi.
Meza kuu katika picha
ya pamoja na sehemu ya Viongozi/Maafisa wa Mahakama pamoja na baadhi ya Wawezeshaji wa Mafunzo hayo. Wa tatu kulia (aliyesimama) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru.
Meza kuu katika picha
ya pamoja na Wajumbe wa kamati ya maandalizi ya Mafunzo hayo.
Meza kuu katika picha
ya pamoja na sehemu ya Watumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni