Na
Festor Sanga- Mahakama Kigoma
Jumla ya Mahakimu 29 wa
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma wamepatiwa mafunzo kwa ajili ya kuwajengea
uwezo wa kutekeleza majukumu mbalimbali.
Mafunzo hayo yametolewa
kwa Mahakimu wa ngazi zote katika kanda
hiyo,Novemba Mosi, mwaka huu, ikiwa ni muendelezo wa utekekezaji wa mpango wa mafunzo
ya ndani kwa watumishi wa Mahakama kwa
mwaka wa fedha 2019/2020 yaliyoandaliwa na kanda hiyo
kwa awamu tatu.
Akifungua mafunzo hayo,
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Ilvin Mugeta aliwataka
Mahakimu kama viongozi kuyatambua vema majukumu yao na mwelekeo wa Mahakama.
Alisema juu ya umuhimu
wa kuimarisha maadili na utendaji kazi kwa kuwa na mwelekeo unaofanana. “tumekutana
ili tuwe na mtazamo na mwelekeo wa pamoja katika kutekeleza majukumu yetu ya
Utoaji Haki kwa mujibu wa Sheria, Kanuni,Taratibu na Miongozo ya utoaji Haki”,
alisisitiza.
Mada zilizofundishwa katika
mafunzo hayo, ni Mpango Mkakati wa
Mahakama wa Miaka Mitano 2015/2016 hadi 2019/2020, kwa kuoanisha na majukumu ya
kila siku ya Mahakimu, ujazaji sahihi wa rejesta za mashauri, makosa
yanayojirudia katika Uendeshaji wa Mashauri ya Jinai na Maadili ya Maafisa wa
Mahakama na ya Utumishi wa Umma.
Mafunzo hayo yalitolewa
na Mhe. Mugeta na Jaji wa Mahakama Kuu Kigoma, Mhe. Jaji Athman Kirati.
Pamoja na Mafunzo hayo,
siku hiyo pia ilitumika kufanya Kikao cha
Wanachama wa Chama cha Majaji na Mahakimu (JMAT) Tawi la Kigoma, kilicholenga
kujadili Mustakabali na Ustawi wa Chama sambamba na kufanya uchaguzi wa
Viongozi wa Chama hicho.
Awali, akitoa maelezo
mafupi ya mafunzo hayo, Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Bw. Moses
Mashaka alisema ni mkakati wa kutatua changamoto zilizobainika wakati wa Kaguzi
za Mahakama na Magereza, ambapo yatahusisha watumishi 66 na yataendeshwa kwa
awamu tatu, awamu ya kwanza imehusisha Mahakimu wote na awamu zinazofuata
zilihusisha watumishi wasio Mahakimu hususani wanaofanya kazi zaidi ya
walizoajiriwa kuzifanya.
Mafunzo hayo
yalihitimiswa kwa wajumbe wote kuwa na maazimio ya pamoja na kuahidi kutekeleza
majukumu yao kwa ufanisi na uadilifu katika kuifanya kanda ya Kigoma kuwa ya
mfano bora wa usimamizi na uendeshaji wa majukumu ya Mahakama na kutekeleza
Mpango Mkakati kwa ufanisi.
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma (aliyesimama) Mhe. Ilvin Mugeta akifungua Mafunzo
ya Mahakimu Mapema Novemba 01, mwaka huu. Kulia ni Jaji Athuman Kirati, Jaji wa
Mahakama Kuu Kigoma.
|
Mtendaji wa Mahakama
Kuu Kanda ya Kigoma Bw. Moses Mashaka (aliyesimama) akitoa taarifa fupi kuhusu Mafunzo
yaliyofanyika katika Ukumbi wa Mahakama Kuu Kigoma.
|
Jaji Mfawidhi wa
Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe IIlvin Mugeta akitoa ufafanuzi kuhusu Mpango
Mkakati wa Mahakama kwa Mahakimu waliohudhuria mafunzo hayo.
|
Wajumbe wa kundi
mojawapo lilioundwa wakijadiliana jambo katika mafunzo yaliyofanyika mnamo
Novemba 01, mwaka huu.
|
Mwenyekiti wa Chama cha
Majaji na Mahakimu Tawi la Kigoma aliyechaguliwa, Mhe. Imani Batenzi akisoma
taarifa ya Chama mbele ya wajumbe.
|
Baadhi ya wajumbe wa
Chama cha Majaji na Mahakimu Tawi la Kigoma wakiwa katika picha ya pamoja.
(Picha na Festor Sanga-
Mahakama, Kigoma)
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni