Na
Lydia Churi-Mahakama
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Majaji aliowateua
na kuwaapisha leo kufanya kazi kwa haki na kutoa hukumu kwa wakati.
Akizungumza mara baada
ya kuwaapisha Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na Viongozi wengine
aliowateua, leo Ikulu jijini Dar es salaam, Rais Magufuli amewapongeza Majaji
hao na kuwataka kutekeleza wajibu wao ili wananchi wapate haki kwa wakati.
“Haki hutolewa na Mungu
lakini ninyi mmepewa mamlaka makubwa hapa duniani ya kuhukumu hivyo katoeni
hukumu kwa haki na msicheleweshe haki”, alisema Mhe. Rais.
Aidha Mhe.Magufuli
amewataka Majaji wapya kutimiza wajibu wao kwa haki na kuwatumikia watanzania hasa
wale wanyonge ambao haki zao zinapotea.
Akimzungumzia aliyekuwa
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Katarina Revocati, Mhe. Rais
alimpongeza kwa kazi nzuri aliyofanya akiwa Mahakama ya Tanzania na kumtaka
akasaidie kuusimamia mkoa wa Njombe wenye fursa nyingi ili mkoa huo usonge
mbele.
Awali akizungumza, Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alimshukuru Mhe. Rais kwa
kuongeza idadi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania hatua itakayosaidia
mashauri kumalizika kwa wakati.
Alisema hivi sasa idadi
ya Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania imefikia 78 kutoka Majaji 66 waliokuwepo
kabla ya uteuzi wa jana. Alisema Majaji wawili wanatarajia kustaafu mwishoni
mwa mwaka huu na idadi yao itabaki kuwa ni Majaji 76 ifikapo mwezi Desemba
mwaka huu.
Alisema kulingana na
idadi hiyo ya Majaji, kila Jaji hivi sasa ana mzigo wa kusikiliza mashauri
zaidi ya 500 wakati uwezo wa Jaji mmoja ni kusikiliza mashauri 220 katika
kipindi cha mwaka mmoja.
Aliwataka Majaji
walioapishwa leo kutekeleza wajibu wao kwa mujibu wa sheria kwa kuwa Mahakama
ya Tanzania imejiwekea utaratibu wa kujisimamia katika kazi ambapo kila Jaji anatakiwa
kusikiliza na kumaliza mashauri 220 kwa mwaka, kutoa nakala za hukumu ndani ya
siku 21 tangu kumalizika kwa shauri na kutoa mwenendo wa shauri ndani ya siku
30.
“Mnaanza kazi kwa kuaminiwa,
Mhe. Rais amewaamini na mmeibeba imani, hivyo iendelezeni imani hiyo kwani
ikipungua tutatumia sheria”, alisisitiza Jaji Mkuu.
Akimzungumzia aliyekuwa
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania ambaye ameteuliwa kuwa Katibu Tawala wa
Mkoa wa Njombe, Jaji Mkuu alimpongeza kwa kazi nzuri aliyofanya ndani ya
Mahakama na kumtaka kwenda kuendeleza kazi hiyo nzuri pia katika mkoa wa Njombe.
Jana Rais Magufuli
alifanya uteuzi wa Majaji 12 wa Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na viongozi
wengine wakiwemo Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG), Katibu Tawala Mkoa wa Njombe (RAS), Balozi wa
Tanzania nchini Kuwait, Kamishna wa kazi, Mwenyekiti wa Tume ya Haki za
Binadamu na Utawala Bora na Makamu wake pamoja na Makamishna wa Tume hiyo.
Magufuli akimuapisha
Mhe. Joachim Tiganga kuwa Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania. Kabla ya uteuzi huu Mhe. Tiganga alikuwa Naibu Msajili Mfawidhi wa Mahakama Kuu-Kanda ya Dar es Salaam.
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza katika hafla hiyo.
|
Baadhi ya Viongozi
mbalimbali wa Serikali, Majaji na wageni waalikwa walioshiriki katika hafla ya
kuapishwa iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam, Novemba 04, 2019.
|
Mhe. Rais akizungumza mara baada ya kuapisha |
Spika wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Ndugai akizungumza katika hafla hiyo.
Meza kuu katika picha
ya pamoja na Viongozi walioapishwa pamoja na Wahe. Majaji wa Mahakama ya Rufani
(T).
|
Meza kuu katika picha
ya pamoja na Viongozi walioapishwa pamoja na Wahe. Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania.
|
Picha ya pamoja, meza
kuu, Viongozi walioapishwa pamoja na Watumishi mbalimbali wa Mahakama
walioshiriki katika hafla hiyo. Aliyesimama mstari wa kwanza (wa kwanza
kushoto) ni Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni