Jumatano, 11 Desemba 2019

JAJI KIONGOZI ARIDHISHWA NA UTENDAJI KAZI WA MAHAKAMA MTANDAO TANGA.



Na  Mwandishi  Wetu 

Jaji Kiongozi wa Mahakama  Kuu  ya Tanzania,  Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi ameupongeza  uongozi  wa  Mahakama  Kuu Kanda ya Tanga kwa kazi kubwa na nzuri waliyoifanya  ya utekelezaji wa Mahakama Mtandao (E- Judiciary ) licha  ya kupata bajeti ndogo.

Aidha, Jaji Kiongozi huyo amempongeza  Afisa Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) Bi. Amina Ahmad kutokana na jitihada zake za kutumia vyema taaluma yake kubuni na kuanzisha mifumo ya kielektroniki ya ndani kwa ajili ya kusaidia utunzaji na uhifadhi salama wa majalada ya mashauri na nyaraka mbalimbali za kiutendaji.

Afisa Tehama huyo alibuni mifumo hiyo kwa  kupitia mifumo ya “Tanga Record Centre”, E- Office, E-Library na Receive & Return File Database (Double R).

Vile vile alimpongeza Afisa huyo kwa kuwezesha kusimikwa (Installation) kwa mifumo ya matangazo kwa umma (Public Announcement system) na uoneshaji wa orodha ya mashauri kwenye Televisheni (Case Broadcasting system).

Alipongeza utendaji wa pamoja (Team work) uliojengwa na watumishi wa Kanda ya Tanga chini ya uongozi na usimamizi wa Jaji Mfawidhi, Mhe. Amiri Mruma.

Mhe. Jaji Kiongozi aliyasema hayo baada ya kupokea taarifa ya Kanda iliyosomwa kwake na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Tanga, Mhe. Francis Kabwe, na baadae kujionea shughuli na utendaji wa mifumo ya kielekroniki kupitia ratiba ya ziara yake ya siku moja aliyoifanya tarehe 10 Desemba mwaka huu.

Katika ziara hiyo  alionyesha kuridhishwa na utendaji wa kanda hiyo na kusema kuwa,  inastahili kuwa ya kimkakati kwa mafunzo ya vitendo kwa viongozi wapya hasa kwa kuzingatia kwamba iko jirani na Chuo cha Uongozi wa Mahakama - Lushoto (IJA).

Dkt Feleshi aliutaka uongozi huo kuwatambua, watumishi wanaothubutu kuonesha ubunifu kutokana na vipaji vyao waeleweke na kuenziwa ili waendelee kuwa hazina ya Mhimili wa Mahakama badala ya kukatishwa tamaa.




 Mhe. Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akisaini kitabu cha wageni alipokuwa Mahakama Kuu Tanga.

Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Francis Kabwe akisoma taarifa ya Kanda


 Afisa Tehama wa Mahakama Kuu Tanga, Bi. Amina Ahmad(mwenye gauni nyeusi) akielezea utekelezaji na usimikaji wa Mfumo wa Kielektroniki wa Maktaba ya Mahakama Kuu Tanga (E- Library).


Mhe. Jaji Kiongozi akizungumza na wananchi waliofika Mahakama Kuu kwa ajili ya kupata huduma mbalimbali.
Mhe. Jaji Kiongozi (Aliyesimama) akizungumza na baadhi ya watumishi wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga.



Mhe. Jaji Kiongozi (wa katikati) akiwa kwenye picha ya pamoja na Wajumbe wa Menejimenti ya  Mahakama Kuu  Kanda  ya Tanga. Kushoto kwake ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu  Kanda Tanga Mhe. Amiri Mruma akifuatiwa na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Mhe. Francis Kabwe. Kulia kwake ni Jaji wa Mahakama Kuu Kanda ya  Tanga, Mhe. Edson Mkasimongwa akifuatiwa na Mtendaji wa Mahakama Kuu Kanda ya Tanga, Bw. Ahmed Selemani Ng’eni.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni