Na
Lydia Churi- Bukombe, Geita
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma leo amezindua majengo mawili likiwemo jengo la Mahakama
ya Hakimu Mkazi Geita pamoja na lile la Mahakama ya wilaya ya Bukombe na
kuwataka watumishi wa Mahakama kutoa haki kwa kila mtanzania na kwa wakati
unaostahili.
Akizindua majengo hayo mkoani
Geita, Jaji Mkuu amesema kukamilika kwa majengo hayo kutaharakisha utoaji wa
huduma za Mahakama kwa kuwa majengo ni bora na ya kisasa.
Alisema watumishi wa
Mahakama wanalo deni kubwa la kuhakikisha kuwa majengo mazuri yanayozinduliwa
yanatumika kutoa haki kwa kila mtanzania na kwa wakati unaostahili.
“Bila kubadili tabia za utoaji wa huduma, haimaanishi
kwamba, kuwepo kwa majengo na miundombinu bora, basi kutakuwa na upatikanaji wa
huduma bora kwa mwananchi”, alisema.
Jaji Mkuu alisema kuzinduliwa kwa majengo hayo ya
kisasa pia kutawarahisishia watumishi kuwapa wananchi kile wanachostahili huku
akiwataka kutenda haki ili maana halisi ya kuwa na majengo na miundombinu bora
idhihirike.
Aidha Jaji Mkuu amewataka
Viongozi wa Mahakama Mkoa wa Geita kuhimiza na kusimamia matumizi ya TEHAMA na
hasa mfumo ulioboreshwa wa Kielekitroniki wa kuratibu mashauri (JSDS II) kwani
vyote hivi vikitumika kikamilifu vitasaidia kumaliza mlundikano wa Mashauri
(case backlogs).
Akizungumzia Mahakama za
Hakimu Mkazi Jaji Mkuu alisema kati ya mikoa 26 ya Tanzania Bara, ni mikoa 18
tu ndiyo yenye majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi. Mikoa 8 bado inatumia majengo
ya kupanga na ya muda yaliyoazimwa kutoka taasisi nyingine za Serikali na Halmashauri.
Katika mikoa 18 yenye
majengo, mikoa 10 ambayo ni Morogoro, Mara, Ruvuma, Mwanza, Lindi, Kigoma,
Kilimajaro, Shinyanga na Rukwa ina majengo chakavu, kiasi cha kuhitaji ukarabati
ama kujengwa upya miradi mingine inayotekelezwa.
Kwa upande wa Mahakama za
wilaya. Jaji Mkuu alisema kila wilaya hapa
nchini inapaswa kuwa na Mahakama ya wilaya ambapo kuna jumla ya wilaya 139
Tanzania bara lakini wilaya 111 tu ndizo zenye huduma moja kwa moja za Mahakama
ya wilaya.
Aliongeza kuwa Wilaya 28
zinahudumiwa na Mahakama za wilaya jirani (Concurrent jurisdiction) kwa
kutembelewa na Mahakimu huku akitolea mfano wa wilaya ya Geita inayohudumiwa na
wilaya ya Nyang’hwale na Mahakama ya wilaya ya Mbogwe inahudumiwa na Mahakama
ya wilaya ya Bukombe.
Jaji Mkuu alifafanua kuwa
katika wilaya zote Tanzania bara, wilaya zenye majengo ya Mahakama za wilaya ni
37 tu na zilizobaki 102 zinatumia majengo ya kupanga au kwa kuazimwa na Taasisi
nyingine za serikali kuu au halmashauri za wilaya.
Alisema moja ya mikakati iliyowekwa na Mahakama ni
kuhakikisha kuwa kila eneo jipya la kiutawala linaloanzishwa inajengwa Mahakama
kwa kuwa huduma za Mahakama ni muhimu kama ilivyo huduma nyingine.
Awali akitoa Taarifa ya miradi
ya ujenzi wa majengo hayo, Mtendaji Mkuu Mahakama ya Tanzania Bwn. Mathias Kabunduguru
alisema miradi hiyo mikubwa imetekelezwa na kampuni ya MOLADI TANZANIA LTD,
chini ya usimamizi wa Chuo Kikuu cha Ardhi (ARU).
Wananchi wa mji wa Ushirombo wilayani Bukombe wakiwa wamejitokeza kwa wingi kushuhudia uzinduzi wa Mahakama ya wilaya ya Bukombe uliofanywa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Bukombe. wWa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Geita Mhe. Robert Gabriel na wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Elieza Feleshi.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akikata utepe kama ishara ya kuzindua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi mkoa wa Geita na Mahakama ya wilaya ya Geita.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akitoa taarifa ya miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama.
Jaji
Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Elieza Feleshi akizungumza na wananchi wa Bukombe.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya wilaya ya Bukombe.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma, Mkuu wa mkoa wa Geita Mhe. Robert Gabriel na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakifungua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita pamoja na Mahakama ya wilaya ya Geita,
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa na viongozi mbalimbali wakishangilia mara baada ya kuzindua jengo la Mahakama.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akifungua pazia kuashiria uzinduzi wa Mahakam ya wilaya Bukombe.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma(katikati) akiwa katika picha pamoja na Mahakimu wote wa mkoa wa Geita pamoja na watumishi wengine wa Mahakama.
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiwa katika picha ya pamoja na watoto wa wilaya ya Bukombe
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akipokea maelezo kutoka kwa Mhandishi Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Khamdu Kitunzi mara baada ya kulizindua jengo hilo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita na Mahakama ya wilaya ya Geita.
(Picha na Lydia Churi-Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni