Na
Mary Gwera, Mahakama-Arusha
Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Majaji Wafawidhi
nchini kuwa na umiliki ‘ownership’ ya masuala mbalimbali yanayohusiana na kazi zao
kwa maslahi mapana ya Taasisi na jamii kwa ujumla.
Akifunga rasmi
Mafunzo Elekezi ya siku tano (5) kwa Majaji Wafawidhi na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu ya
Tanzania yaliyofanyika katika Ukumbi wa ‘EAC’ jijini Arusha, Mhe. Jaji Mkuu
alisema kuwa Mahakama
ni Mhimili wa Dola uliopewa dhamana kubwa ya mwisho ya utoaji haki, na tafsiri
ya sheria hivyo kila Jaji ama Hakimu ana haki na wajibu wa kusimamia dhamana
hii.
“Kama viongozi wa maeneo yenu, mna wajibu wa
kumiliki/ kusimamia maeneo mbalimbali ikiwemo usimamizi wa sheria mbalimbali, usimamizi
wa utekelezaji wa Mfumo wa kielektroniki wa Usimamizi wa
Mashauri (JSDS II), kusimamia uadilifu na maadili ya Watumishi walio chini yenu
nk,” alisisitiza Mhe. Jaji Prof. Juma.
“Ili
kuhakikisha kuwa mfumo wa JSDS II unafanya kazi vizuri, ni vyema mkaendelea
kutoa mawazo yenu yenye tija kwa timu
yetu ya ndani inayoendelea kutengeneza mfumo huu ili kuwezesha mfumo huu
kufanya vyema,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.
Aidha, Mhe. Jaji Mkuu aliwataka Majaji hao wanapotoa huduma
kwa wananchi kuhakikisha kuwa kiwango cha wananchi wanaotumia huduma za
Mahakama wanaridhika, kuwa na upatikanaji wa taarifa muhimu za kesi na
kujiuliza endapo huduma zetu ni rafiki kwa wahudumiwa.
Awali, akimkaribisha Mhe. Jaji Mkuu kufunga rasmi mafunzo
hayo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki
Feleshi alimshukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kukubali kufanyika kwa mafunzo hayo
yenye mafanikio makubwa.
“Napenda nikushukuru Mhe. Jaji Mkuu kwa kuridhia kufanyika
kwa mafunzo haya, na vilevile nishukuru kamati nzima ya maandalizi kwa
kuwezesha kufanyika kwa mafunzo haya, kitu ambacho nasisitiza ni kuendelea
kufanya kazi kama timu moja ili kufanikisha mipango
tuliyoazimia/tuliyojiwekea,” alisema Mhe. Jaji Kiongozi.
Katika Mkutano huo ulioanza rasmi Desemba 02,2019 na kuhitimishwa
Desemba 06 mwaka huu, mada mbalimbali zilitolewa ikiwemo maendeleo ya utekelezaji
wa Mpango Mkakati wa miaka mitano wa Mahakama na Mradi wa Maboresho wa huduma
za Mahakama, Mfumo wa ‘JSDS’ II, Ukaguzi
na Usimamizi wa Mahakama za chini ‘Surbodinate Courts’, Mirathi na nyinginezo.
Kwa pamoja Wahe. Majaji hao wamekubaliana/wameridhia kuyafanyia
kazi yale yote yaliyojadiliwa na kuibuliwa katika mkutano huo kwa lengo la
kuboresha huduma ya utoaji haki kwa wananchi.
Pichani ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
akifunga rasmi Mafunzo elekezi ya siku tano (5) kwa Wahe. Majaji Wafawidhi wa
Mahakama Kuu ya Tanzania pamoja na baadhi ya Majaji wa Mahakama Kuu yaliyofanyika
katika Ukumbi wa ‘EAC’ jijini Arusha.
Picha za Wahe. Majaji wakifuatilia hotuba ya Mhe. Jaji Mkuu
alipokuwa akifunga rasmi mafunzo.
Jaji Kiongozi-Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki
Feleshi akizungumza na Wahe. Majaji katika Mafunzo hayo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias Kabunduguru
akifuatilia kinachojiri katika Mafunzo hayo.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna
akitoa neno.
Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama ya Tanzania (JDU), Mhe.
Zahra Maruma akinukuu masuala/maelekezo muhimu yaliyokuwa yakitolewa wakati wa
ufungaji wa mafunzo hayo.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimpatia
cheti cha Ushiriki wa Mafunzo kwa Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu, Kanda ya
Tanga, Mhe. Amir Mruma, wanaoshuhudia wa kwanza kushoto ni Jaji Kiongozi,
Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi kulia ni Jaji
Mfawidhi, Mahakama Kuu-Kanda ya Arusha, Mhe. Moses Mzuna. Wahe. Majaji
walioshiriki katika Mafunzo hayo wote walipatiwa vyeti vya ushiriki wa mafunzo
hayo.
Akiwa katika uso wa furaha, Mhe. Jaji Mkuu akionyesha cheti
chake cha ushiriki wa Mafunzo akiwa kati ya Wahe. Majaji walioshiriki
kikamilifu katika Mafunzo hayo. Hali kadhalika Mhe. Jaji Kiongozi alipatiwa pia cheti cha ushiriki wa Mafunzo hayo.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama-Arusha)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni