Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma
amewashauri Mawakili wapya kutumia elimu ya sheria kibiashara ili kuweza
kukabiliana na changamoto ya ukosefu wa ajira katika sekta hiyo.
Kauli hiyo ameitoa leo Desemba 13, 2019 katika mahafali ya 61 ya kuwapokea na
kuwakubali Mawakili wapya 558 yaliyofanyika katika viwanja vya Shule ya Sheria
kwa Vitendo (School of Law) jijini Dar es Salaam.
Ambapo alisema sekta hiyo, katika karne ya 21 inakabiliwa
na changamoto mbalimbali ambazo ni shinikizo la kiuchumi, kijamii na mabadiliko
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
Alisema uzoefu wa huko Marekani katika kukabiliana na changamoto ya
Mawakili kukosa ajira ni kuwapatia elimu maalum ya biashara, na mbinu za
kufanya biashara.
“Mawakili lazima
watambue Makampuni yao ya Uwakili (Law Firms) ni biashara
kama zilivyo biashara zingine. Ujuzi wa biashara
utamwezesha Wakili afahamu biashara ya Kampuni yake ya Uwakili. ujuzi wa biashara ni zana ya kuendeshea Kampuni yako
ya Uwakili au biashara nyingine yoyote ile”, alisema Jaji Mkuu.
Aidha, alisema kuwa ujuzi katika
biashara utawaweka katika hali ya utayari wa kushidana katika soko la huduma ya
uwakili katika dunia ambayo mipaka ya huduma hizo na zinginezo zenye ushindani mkubwa.
Aliongeza kuwa changamoto ya
Mawakili kukosa ajira za kudumu ipo katika nchi nyingi kama vile Australia, Marekani, na Kanada.
“Mawakili lazima mkubali ushindani kutoka
nje ya Tanzania. Jengeni madaraja ya ushirikiano na Mawakili wenzenu vijana wa
nchi za Jumuiya ya Afrika Mashariki, Jumuiya ya Maendeleo Kusini mwa Afrika
(SADC) ili mtafute biashara ndani na nje ya Tanzania”, alisisitiza.
Aliongeza kwamba mawakili
hao, wanapaswa kujifunza lugha za kimataifa kwa ufasaha mfano:- Kiingereza, Kifaransa na Kichina.
Naye Mwakilishi wa
Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Onorius Njole amewashauri, kuwa kwenda kufanya
kazi katika maeneo yaliyo mbali na miji mikubwa yakiwemo maeneo ya vijijini kwa
kuwa yana uhitaji mkubwa wa huduma hizo.
Kwa upande wake,
Rais wa Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) Dkt. Rugemeleza Nshala aliwasii
wafanye kazi za uwakili kwa bidii, weledi na kuzingatia maadili ili kuiwezesha Mahakama
kutimiza jukumu la msingi la kutenda haki.
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Sekretarieti ya Ajira katika Utumishi wa
Umma hapa Tanzania inaonyesha kuwa ni idadi ndogo ya wahitimu wa Sheria walioomba kujaza nafasi
za kazi katika Utumishi wa Umma ndio walifanikiwa kupata ajira 2017/2018,
ambapo walioomba walikuwa 3,250 waliopata walikuwa 88 sawa na
asilimia 2.7na mwaka 2018/22019 walioomba walikuwa 2,826 waliopata walikuwa 19 sawa na
asilimia 0.6.
Naibu Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.Sharmillah
Sarwatt akitaja majina ya Mawakili wapya waliokubaliwa na kuapishwa leo katika katika
viwanja vya Shule ya Sheria kwa vitendo (School of Law).
|
Mawakili wapya waliokubaliwa na kuapishwa leo wakitoa heshima kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma. |
Wajumbe wa Baraza la Elimu ya Sheria kwa Vitendo wakifuatlia sherehe ya kuapishwa Mawakili hao. |
Mwakilishi wa Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Bw. Onorius Njole akitoa hotuba katika sherehe hizo.
|
Jaji Mkuu wa Tanzania Prof. Ibrahim Hamis Juma akitoa
hotuba wakati wa sherehe hizo.
|
Mawakili hao wakiwa katika picha ya pamoja.
(Picha na Magreth Kinabo na Innocent Kansha – Mahakama
ya Tanzania.)
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni