Na
Lydia Churi-Chato, Geita
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ameviagiza vyombo vyote vya
utoaji haki nchini kushirikiana na Mahakama ya Tanzania ili kuhakikisha watanzania
wanapata haki kwa wakati.
Akizungumza wakati wa
uzinduzi wa jengo la Mahakama ya Wilaya ya Chato alioufanya leo wilayani humo,
Rais Magufuli amesema kuchelewa kumalizika kwa mashauri pamoja na mlundikano wa
mahabusu magerezani hakusababishwi na Majaji au Mahakimu bali unasababishwa na baadhi
ya wadau wa Mahakama wakiwemo Wapelelezi, Waendesha Mashitaka na Mawakili.
“Polisi, wapelelezi, Magereza,
Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Mawakili shirikianeni na Mahakama ili
kurahisisha utoaji wa haki”, alisisitiza Rais Magufuli.
Aidha, Mhe. Rais
ameipongeza Mahakama ya Tanzania kwa hatua kubwa iliyofikia ya ujenzi wa
majengo ya Mahakama katika maeneo mbalimbali nchini. Amesema kujengwa kwa
Majengo haya kutasogeza huduma za Mahakama karibu zaidi na wananchi na pia
kutasaidia kupunguza idadi ya Mahabusu magerezani kwani huduma zitakuwa
zikitolewa kwa wakati.
Amesema licha ya ujenzi
wa majengo ya kisasa, Mahakama ni zaidi ya majengo hivyo ameahidi kushughulikia
changamoto ya upungufu wa watumishi wa Mahakama. Alisema, Serikali inajitahidi
kuongeza idadi ya watumishi wa Mahakama wakiwemo Majaji na Mahakimu. Jumla ya
Mahakimu 396 wameajiriwa na kufanya idadi ya Mahakimu kufikia 938 nchi nzima.
Kwa upande wa Majaji, alisema jumla ya Majaji 50 wameteuliwa hivi karibuni na
kufanya idadi yao kuwa zaidi ya 100.
Rais Magufuli pia amewata
watumishi wa Mahakama nchini kufanya kazi kwa bidii, weledi na uaminifu na
kuacha kujihusisha na vitendo vya rushwa kwa kuwa wananchi bado wana imani na
Mahakama ya Tanzania.
Awali akimkaribisha Mhe.
Rais, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka watumishi
wa Mahakama nchini kufanya kazi kwa bidii na kufuata maadili ili kuleta tija
katika kuwahudumia wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki.
Katika kuboresha
miundombinu ya Mahakama, Jaji Mkuu alisema hivi sasa Mahakama inaendelea
kutekeleza miradi 33 ya ujenzi wa majengo ya Mahakama za wilaya na Mwanzo katika
maeneo mbalimbali nchini.
Aliongeza kuwa jumla ya majengo ya Mahakama tatu za
Hakimu Mkazi yamekamilika katika mikoa ya Geita, Njombe, Simiyu, Manyara na
Kibaha. Alisema Mahakama pia imekamilisha ujenzi wa majengo 13 ya Mahakama za
Wilaya zikiwemo Chunya, Kasulu, Kondoa, Bagamoyo, Mkuranga, Kigamboni, Ilala, Bariadi,
Chato, Longido, Ruangwa, Kilwa na Bukombe.
Jaji Mkuu Mkuu kesho
anatarajiwa kuzindua jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Mkoa wa Geita pamoja na
jengo la Mahakama ya wilaya ya Bukombe.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakikata utepe kuashiria uzinduzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato. Kushoto ni Spika wa Bunge la Tanzania Mhe. Job Ndugai, wa nne kulia ni Mke wa Rais, mama Janet Magufuli na wa tatu kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwasili kwenye viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Chato baada ya kupokewa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
viwanja vya Mahakama ya Wilaya ya Chato baada ya kupokewa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Dkt. Eliezer Feleshi (katikati) na Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bwn. Mathias Kabunduguru.
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa Jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akitoa hotuba ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa hafla hiyo. |
Jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufulipicha ya pamoja na viongozi mbalimbali waliohudhuria hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato.
Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya akiwa katika picha ya pamoja na Watumishi wa Mahakama ya Tanzania mara baada ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Chato.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni