Na Innocent Kansha na Salum Tawani.
Mahakama ya
Hakimu Mkazi Kisutu iliyopo Jijini Dar es Salaam leo kwa mara ya kwanza imetoa dhamana ya mahabusu Bw. Abubakari Seguni aliyepo katika Gereza la Keko kwa njia ya Mahakama Mtandao
maarufu kama ‘Video Conference’.
Dhamana hiyo
imetolewa na Mahakama hiyo kwa kushirikiana na Gereza la Keko lilipo katika
jiji hilo, wakati ilipokuwa ikieendesha
mashauri nane (8) kwa njia ya hiyo ikiwa
ni mwendelezo.
Mtuhumiwa huyo namba
tatu ambaye anakabiliwa na tuhuma ya rushwa na uhujumu uchumi katika shauri namba 43 la mwaka
2017 la jinai, akiwa na wenzake watano dhidi ya Serikali.
Shauri hilo
liletwa mahakamani hapo kwa ajili ya kutajwa,
awali Mwendesha Mashtaka Wakili
wa Serikali, Bi. Ester Martin alidai
kuwa shauri hilo halijakamilika kwa sababu upelelezi wake haujakamilika na linasubiri
kibali kutoka Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka nchini (DPP).
Akisoma masharti
ya dhamana mahabusu huyo, Hakimu Mkazi Mwandamizi Mhe. Augustina Mmbando alieleza
dhamana ya mshitakiwa ipo wazi kwa kuwa na wadhamini wawili watakao weka ahadi ya
shilingi milioni Sitini (ml. 60) na mmoja kati yao lazima awe mtumishi wa Umma
na kwa pamoja wawasilishe mahakamani hati zao za kusafiria.
Akiahirisha
shauri hilo, Mhe. Mmbando alisema litatajwa tena Januari 27, mwaka huu saa tatu (3: 00)
kamili asubuhi.
Mashauri mengine
saba ya jinai yaliyosikilizwa kwa njia
hiyo, ambayo yako katika hatua ya awali ya kutajwa yote
yalihusu Makosa ya Rushwa na Uhujumu Uchumi, kama inavyoelekeza Sheria Namba Tatu ya mwaka 2016 iliyofanya
mabadiliko ya Sheria ya Uhujumu Uchumi
Sura namba 200, ambayo upelelezi wake haujakamilika na mengine yakisubiri
kibali kutoka kwa DPP.
Ambapo shauri la kwanza lilikuwa linamhusu
mtuhumiwa Eke Bidi dhidi ya Serikali,
watuhumiwa wengine ni Wolfgang Sylivester, Xiao Shaudan, Hariri Hariri na
wenzake, Mohamed Ismail Sued na wenzake, Ally Anguzuu Sharifu na wenzake, Maarifa
Abbas Nassor na wenzake na Mohamed Mohamed, wakiwemo wenzake watano wote dhidi
ya serikali.
Mashauri hayo
yote yatatajwa tena Januari 27, mwaka huu.
Mmoja wa wananchi
waliofika mahakamani hapo kusikiliza shauri la ndugu yake, Bw. Rajabu Bakari
mkazi wa Kongowe alisema teknolojia ya
Mahakama Mtandao ni nzuri ila angependa kumwona ndugu yake uso kwa uso.
Mashauri hayo yenye
mahabusu 24 yameendendeshwa mahakamani hapo kupitia gereza hilo kufikia 10,
ambapo mawili yaliendeshwa wiki iliyopita Januari 10, mwaka huu.
Uendeshaji wa mashauri kwa njia hiyo ni mojawapo ya
malengo ya Mahakama ya Tanzania ya kuweza kusikiliza mashauri kwa wakati na
kupunguza gharama za uendeshaji wa mashauri
hayo mfano kuwalipa mashahidi, kuwasafirisha mahabusu, usalama wa
mahabusu , zikiwemo nyingine.
Picha ya pamoja ikionyesha washiriki wa zoezi la
mahakama mtandao katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu na Gereza la Keko
jijini Dar es Salaam.
Baadhi ya wananchi waliofika katika ukumbi wa mahakama
ya Hakimu Mkazi Kisutu, iliyopo jijini Dar es Salaam wakifuatilia mwenendo wa uendeshaji
mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao.
Maafisa wa magereza wakifuatilia mashauri kwa njia
Mahakama Mtandao (kushoto) Musa Kaswaka na (kulia) kwake ni George Mwambashi yaliyokuwa yakiendeshwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, jijini Dar
es Salaam.
(Picha na Innocent Kansha - Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni