Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa ameipongeza Mahakama ya
Tanzania kwa matumizi mazuri ya fedha katika ujenzi wa majengo yake.
Akizindua rasmi jengo jipya
la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa leo, Waziri Mkuu amesema hatua ya Mahakama
kutumia ujenzi gharama nafuu katika ujenzi wa jengo hilo ni matumizi mazuri ya
fedha za Umma.
“Mahakama ya Tanzania ni chombo
ambacho kimemuunga mkono Rais wetu ambaye amekuwa akisisitiza matumizi mazuri
ya fedha za Umma, hivyo nampongeza sana Jaji Mkuu wa Tanzania”, alisema Waziri
Mkuu.
Jengo hilo linalojumuisha
ngazi mbili za Mahakama ambazo ni Mahakama ya Mwanzo na ya wilaya ya Ruangwa limegharimu
kiasi cha shilingi milioni 782,547,340, ambayo ni ndogo ukilinganisha na Wazabuni
wengine waliotaka kujenga jengo hilo kwa zaidi ya shilingi bilioni moja.
Waziri Mkuu amewataka watumishi
wa Mahakama kuendelea kutoa haki kwa wote kwa kuwa ni Mhimili muhimu wa dola ambao
huchangia katika kuleta amani ya nchi.
Amemshukuru Jaji Mkuu kwa
kusogeza huduma za Mahakama karibu na wananchi wa Ruangwa kwa kuwa hatua hiyo itasaidia
kupunguza gharama kubwa walizokuwa wakiingia wananchi kwa kusafiri umbali wa takribani
kilometa 180 kufuata huduma za Mahakama mkoani Lindi.
“Wananchi wa wilaya ya
Ruangwa mmepata bahati ya kupata jengo hili zuri, hivyo nawahimiza kutunza na
kulinda miundombinu yake bila kufanya uharibifu wa aina yoyote”, alisisitiza.
Awali akimkaribisha
Waziri Mkuu, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka
watumishi wa Mahakama kutoa huduma bora zinazoendana na uzuri wa jengo na kuachana
na tabia na mienendo inayoenda kinyume na maadili.
“Tukumbuke kuwa Mahakama
ni mali ya wananchi na wanayo haki ya kupatiwa huduma bora hivyo tutoe huduma itakayowaridhisha
wananchi wanaofika mahakamani kutafuta haki”, alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu pia amewaasa
wananchi kutumia Mahakama kutatua migogoro yao badala ya kuegesha kesi
mahakamani. Amesema wananchi pia wanayo haki kisheria ya kutumia usuluhishi
kabla ya kufungua mashauri mahakamani.
Aidha amewaasa wananchi
na watumishi wa Mahakama kutunza miundombinu ya jengo hilo ili lidumu kwa muda
mrefu kwa kuwa mahakama bado ina safari ndefu katika kujenga majengo yake.
Jaji Mkuu pia ameiomba Serikali
kuanzisha Mahakama mahali yanapoanzishwa maeneo ya utawala. Lengo la Mahakama
ni kufikisha huduma ya utoaji haki kwa kuwa na majengo yake katika kila kata,
tarafa, wilaya na Mikoa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akisalimiana na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma mara baada ya kuwasili Mahakama ya wilaya ya Ruangwa kwa ajili ya kuzindua jengo jipya la Makahama hiyo.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma wakifungua pazia kuashiria uzinduzi wa jengo jipya la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akikagua jengo la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa mara baada ya kulizindua rasmi.
Wananchi wa wilaya ya Ruangwa wakiwa kwenye uzinduzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa.
Baadhi ya watumishi wa Mahakama ya Tanzania na viongozi mbalimbali wa vyombo vya Ulinzi na Usalama wakiwa kwenye hafla ya uzinduzi wa jengo la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa.
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya wilaya ya Ruangwa.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya wilaya ya Ruangwa.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akizungumza wakati wa hafla ya uzinduzi wa Mahakama ya wilaya ya Ruangwa.
|
Waziri Mkuu wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa akikata utepe kuashiria kuzindua jengo la Mahakama ya wilaya ya Ruangwa, wa pili kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi na wa kwanza kulia ni Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni