Na Mary Gwera, Mahakama
Jumla ya mashauri 100 yameanza kusikilizwa na Mahakama
inayotembea ‘mobile court’ katika zoezi maalum linalofanywa na Halmashauri ya
Wilaya ya Kinondoni kwa wananchi waliokamatwa kwa kosa la utiririshaji wa maji taka
katika wilaya hiyo.
Akizungumza katika mahojiano maalum, Hakimu Mkazi
ambaye pia ni Mratibu wa shughuli za Mahakama inayotembea, Mhe. Moses Ndelwa alisema
zoezi hilo limeanza rasmi Januari 10 mwaka huu katika Viwanja vya Biafra-Kinondoni
jijini Dar es Salaam.
“Lengo la zoezi hili maalum ambalo limeanza rasmi leo
(Januari 10, 2020) ni kusikiliza mashauri yanayotokana na ‘operation’ maalum
inayofanywa na Wilaya ya Kinondoni kwa watu wanaotiririsha maji taka ambayo
yamepangwa kumalizika ndani ya siku moja (1),” alieleza Mhe. Ndelwa.
Hii ni mara ya kwanza kwa Mahakama hii kufanya zoezi
maalum la usikilizaji wa mashauri mbali na mashauri ya kawaida inayosikiliza
katika ratiba zake za kawaida kwa maeneo inayotoa huduma katika mikoa ya Mwanza
na Dar es Salaam.
Aidha, huduma ya Mahakama inayotembea ni endelevu na
itakuwa ikitolewa katika mazoezi maalum katika maeneo yenye uhitaji maalum katika
mikoa ya Dar es Salaam na Mwanza ambapo huduma hiyo inapatikana kwa kuanzia.
Akizungumzia mafanikio ya huduma za Mahakama inayotembea,
Hakimu huyo Mkazi alisema hadi kufikia Desemba 2019, Mahakama hiyo tayari
imesikiliza jumla ya mashauri 95, huku Mwanza ikiwa imesikiliza jumla ya mashauri
57 na Dar es Salaam 38.
Aliongeza kuwa Mahakama hiyo imefanikiwa kuhudumia
jumla ya wananchi wanufaika 516 toka kuanza rasmi kwa huduma hiyo na kuwataka
wananchi wenye mashauri mbalimbali kutosita kujitokeza kusajili kesi zao katika
Mahakama hii.
Mahakama inayotembea imeanzishwa kwa lengo la kusogeza
huduma ya utoaji haki karibu zaidi na wananchi waliopo mbali na huduma za
Mahakama.
Baadhi ya wananchi
waliohudhuria kusikiliza hatima ya mashauri ya ndugu na Jamaa zao katika
mahakama inayotembea katika Viwanja vya Biafra-Kinondoni-Dar es Salaam.
Baadhi ya
Watumishi wa Mahakama wakiwa ndani ya Mahakama inayotembea kwa maandalizi ya kutoa huduma, wa kwanza kushoto ni Naibu Msajili wa Mahakama Kanda ya
Dar es Salaam, Mhe. Joseph Fovo, wa pili kushoto ni Mratibu wa Mahakama inayotembea, Mhe. Moses
Ndelwa na wengineo.
Baadhi ya
watuhumiwa wakishushwa katika gari la Polisi ili waweze kufikishwa katika
Mahakama inayotembea ili kusikiliza tuhuma zinazowakabili.
Mratibu wa
Mahakama inayotembea, Mhe. Moses Ndelwa akitoa ufafanuzi kwa Mwandishi wa
Habari juu ya shughuli zinazofanywa na Mahakama inayotembea.
(Picha na Tawani Salum na Innocent Kansha, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni