Na Lydia Churi- Mahakama
Mahakama ya
Tanzania imefanikiwa kupunguza wastani wa muda wa kusikiliza shauri kutoka siku
515 na kufikia siku 345 kati ya mwaka 2015 na mwaka 2019.
Mtendaji Mkuu
wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru amewaambia waandishi wa Habari leo
kuwa wastani huo umepungua kutokana na Mahakama kujiwekea mikakati mbalimbali
ikiwemo kuongeza idadi ya watumishi.
Kwa mujibu
wa Mtendaji Mkuu, Mahakama ya Tanzania pia imefanikiwa kupunguza Mashauri ya
Mlundikano kutoka asilimia 16 mwaka 2015 na kufikia asilimia 4 mwaka
2019.
Alisema pamoja
na maboresho yaliyo fanyika na yanayoendelea katika kipindi cha miaka mitano,
serikali imetoa vibali vya kuajiri jumla ya watumishi wa kada mbalimbali 1414 wakiwemo Mahakimu 430.
Aidha, ili
kuhakikisha huduma ya utoaji haki inasonga mbele, kati ya mwaka 2016 na sasa, Tume
ya Utumishi wa Mahakama kwa mamlaka iliyopewa na Ibara ya 113 (1) (a) ya Katiba
ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania imemshauri Mheshimiwa Rais juu ya uteuzi wa Majaji wa Mahakama Kuu 39 na kufanya idadi ya Majaji kuwa 78. Aliongeza kuwa kati ya mwaka 2016 hadi sasa
jumla ya Majaji 28 wa Mahakama Kuu wamestaafu utumishi.
Alisema ongezeko
la idadi ya watumishi linalenga kutekeleza nia ya Mahakama ya kufupisha muda wa
usikilizwaji wa mashauri. Mahakama imejipangia utaratibu wake ambapo shauri katika
Mahakama za Rufani na Mahakama Kuu linapaswa kumalizika ndani ya miaka miwili, Mahakama
za Hakimu Mkazi na za wilaya mwaka na katika Mahakama ya Mwanzo halitakiwi
kuzidi miezi 6.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias
Kabunduguru (katikati) akiwa kwenye Mkutano na Waandishi wa habari (hawapo pichani). Wa pili kushoto ni Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya, wa pili kulia ni Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Bw. Solanus Nyimbi na kulia ni Mkurugenzi wa Tehama wa Mahakama ya Tanzania Bw. Kalege Enock. Kushoto ni Mkuu wa Kitengo cha Usimamizi wa Majengo cha Mahakama, Mhandisi Khamadu Kitunzi.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw.
Mathias
Kabunduguru (katikati) akizungumza.
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani
Bw. Solanus Nyimbi na Mkurugenzi wa Tehama wa Mahakama ya
Tanzania Bw. Kalege Enock wakifuatilia jambo wakati wa Mkutano na Waandishi wa habari.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni