Na Magreth Kinabo-Mahakama
Mahakama
ya Tanzania katika kipindi cha miaka minne ya uongozi wa Serikali ya Awamu ya Tano
imefanikiwa kukamilisha miradi 42 ya ujenzi na ukarabati wa majengo yake katika
ngazi zote kuanzia Mahakama Kuu mpaka Mahakama za Mwanzo.
Miradi
hiyo ya ujenzi imetekelezwa katika maeneo mbalimbali nchini kwa lengo la
kutatua changamoto iliyopo ya upungufu na uchakavu wa majengo ya Mahakama na
kutekeleza azma ya Serikali ya kuboresha
na kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi.
Akizungumza
na Waandishi wa Habari leo, Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw. Mathias
Kabunduguru amesema kutokana na ukamilishwaji wa miradi hiyo, Mahakama ya
Tanzania inatarajia kuzindua majengo ya Mahakama za Wilaya za Ruangwa na Kilwa.
Jengo
la Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa litazinduliwa Januari 14, 2020 na Waziri Mkuu
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa. Wakati Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma atazindua jengo la Mahakama ya Wilaya
ya Kilwa Januari 15, 2020.
‘Tunajenga
majengo haya kwa kuzingatia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ili kurahisisha
shughuli za utoaji haki kwa wakati,’ alisema Kabunduguru.
Alisema
miradi ya ujenzi iliyokamilika inajumuisha majengo manne ya Mahakama Kuu ambapo
imejenga majengo mapya katika mikoa ya
Kigoma na Musoma na kuanzisha huduma za Mahakama Kuu pamoja na kuyafanyia
ukarabati mkubwa majengo ya Mahakama Kuu kanda za Mbeya na Tanga.
Aidha,
Mahakama ya Tanzania imekamilisha ujenzi wa majengo matano ya Mahakama za Hakimu
Mkazi katika mikoa ya Pwani, Manyara, Geita, Njombe na Simiyu.
Katika
kipindi cha miaka minne Mahakama imefanikiwa kukamilisha ujenzi wa majengo 16
ya Mahakama za wilaya ambazo ni Bagamoyo, Kigamboni, Mkuranga, Ilala, Kibaha,
Babati na Bariadi. Majengo mengine ni pamoja na Mahakama za wilaya za Chato,
Geita, Bukombe, Ruangwa, Kilwa Masoko, Bariadi, Kondoa, Longido, Chunya na
Kasulu.
Aliongeza
kuwa kwa upande wa Mahakama za Mwanzo, Mahakama imefanikiwa kujenga majengo mapya ya Mahakama za Mwanzo Kawe (Dar es salaam),Mkunya (Newala),
Msanzi (Sumbawanga), Mtowisa (Sumbawanga), Uyole (Mbeya), na Ngerengere (Morogoro).
Mahakama
imekamilisha miradi ya ujenzi wa majengo ya Mahakama za Mwanzo iliyokuwa
imesimama katika maeneo ya Iguguno (Singida), Bereko (Kondoa), Wasso (Loliondo),
Old Korogwe na Magoma (Korogwe). Maeneo mengine ni Mvomero (Morogoro), Karatu (Arusha),
Robanda (Serengeti), Itinje (Simiyu), Totowe na Mlowo (Songwe).
Mahakama
inaendelea na ujenzi wa majengo ya Mahakama za Hakimu Mkazi katika mikoa ya Katavi
na Lindi pamoja na Mahakama za wilaya za Rungwe, Kilindi, Sikonge,
Wanging’ombe, Makete na Bunda.
Aidha
ujenzi wa Majengo ya Mahakama za Mwanzo Mtae (Tanga), Laela (Sumbawanga),
Lugarawa (Ludewa), Mang’ula na Mlimba (Morogoro) unaendelea. Kwa upande wa
ukarabati, Mahakama inaendelea na ukarabati mkubwa wa jengo la Mahakama Kuu ya
Tanzania kanda ya Sumbawanga. Miradi hii yote inatarajiwa kukamilika kabla ya
Juni 2020.
Alisema
Mahakama inaendelea na kasi ya uboreshaji wa miundombinu yake ambapo leo imeingia
Mkataba na Wakandarasi kujenga majengo sita ya Mahakama Kuu maarufu kama vituo
vya utoaji wa Haki Jumuishi (Intergrated Justice Centre) katika mikoa ya
Morogoro, Dar Es Salaam (Kinondoni na Temeke), Dodoma, Mwanza na Arusha.
Katika
mwaka huu wa fedha Mahakama inakusudia kujenga majengo mengine 33 katika maeneo mbalimbali nchini.
Ujenzi wa majengo haya unaenda sambamba na uwekaji wa mifumo ya kisasa ya
TEHAMA.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Bw.
Mathias Kabunduguru akizungumza na waandishi wa habari kuhusu uzinduzi wa
majengo ya Mahakama ya Mahakama ya Wilaya ya Ruangwa na Wilaya ya Kilwa.
Kaimu Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Eva Nkya na (kushoto) ni Mkuu wa Kitengo cha
Usimamizi wa Majengo wa Mahakama ya Tanzania, Mhandisi Khamadu Kitunzi
wakimsikiliza Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania(hayupo pichani).
Mtendaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Bw. Solanus Nyimbi(kulia) na
Mkurugenzi wa Teknolojia ya Habari na
Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania, Bw, Kalege Enock (kushoto) wakimsikiliza
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania( hayupo pichani).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni