Na Magreth Kinabo- Mahakama
Mahakama ya Tanzania imeokoa kiasi cha fedha Shilingi milioni 129 baada ya
kuendesha mashauri kwa njia ya Mtandao (‘Video Conference’).
Kati ya fedha hizo, Mahakama ya Rufani Tanzania, imefanikiwa
kuokoa kiasi cha shilingi Milioni 95 katika kipindi cha mwezi Oktoba, 2019 baada ya
kuendesha vikao maalum kwa njia ya mtandao wakati Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu imeokoa Shilingi milioni 34 katika kipindi cha mwaka jana.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo wakati akitoa taarifa kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya Sheria na Siku ya Sheria nchini, Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema katika
kipindi cha mwaka jana, Mahakama ya Rufani
iliendesha vikao hivyo ambavyo vilivyofanyika kwa njia ya video conferencing
kwenye vituo vya Dar es Salaam,
Mwanza, Mbeya, Tabora na Bukoba.
Alisema jumla ya maombi 60 yalisikilizwa na Majaji 18 wa
Mahakama hiyo, ambapo kila Jaji alipangiwa kusikiliza maombi kati ya
mawili na sita.
‘Gharama ya zoezi zima
la kutumia video Conferencing ilikuwa shilingi milioni 5 ambayo ilihusisha gharama
za Internet, pamoja na usafiri wa watumishi kwa ajili ya kwenda kuratibu
zoezi hilo. ‘Gharama hizo zilijumuisha pia kuwalipa Mawakili wa kujitegemea
wanaotakiwa kuwawakilisha wafungwa walio magerezani kwa makosa ya mauaji’,
alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu alisema Mahakama hiyo ingetumia utaratibu wa
kawaida ungegharimu Shilingi milioni 100.
Prof, Juma alifafanua
kwamba kutokana kutumika kwa njia hiyo, Majaji
walibaki jijini Dar Salaam lakini
waliweza kusikiliza maombi, na kisha kurudi maofisini kuendelea na shughuli zao
zingine.
Jaji Mkuu alisema mfumo
huo, umefungwa kwenye vituo sita vya Mahakama Kuu katika kanda za Dar es salaam,
Mbeya, na Bukoba pamoja na Kituo cha Mafunzo cha Kisutu, Gereza la Keko na Chuo
cha Uongozi wa Mahakama (Lushoto).
Kwa mujibu wa takwimu kutoka Idara ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano ya
Mahakama ya Tanzania, zinaonyesha kwamba upande wa Mahakama Kuu ya Tanzania kesi
zilizosikilizwa zinazohusu Makosa ya
Rushwa na Uhujumu Uchumi kwa njia hiyo
kuanzia Julai mwaka 2016 hadi Julai 8,
mwaka jana ni 375, yaliyotolewa maamuzi ni 371 na zilizobakia ni nne.
Wakati huohuo, kwa mujibu wa taarifa ilitolewa na Mtendaji wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu, Bi. Athanasia Kabuyanja ilisema kwamba
Mahakama hiyo katika kipindi cha mwak jana iliendesha kesi sita, zikiwemo za Uhujumu
Uchumi kwa njia ya video conference, kesi tano, mashahidi walikuwa nje ya nchi na moja shahidi
akiwa nchini.
Hivyo gharama iliyotumika kwa kesi zote sita ni Shilingi milioni 1.4 , ambapo utaratibu wa
kawaida ungetumia ungegharimu Shilingi milioni 34 hivyo njia hiyo imeokoa kiasi cha shilingi milioni
34.
Aidha Kabuyanja aliongeza pia kesi zilizosikilizwa kwa njia
hiyo kati ya Mahakama hiyo na Gereza la Keko kuanzia Januari 13, mwaka huu hadi
Januari 22 mwaka huu ni kesi 25.
Akizungumzia matumizi ya TEHAMA, Jaji Mkuu aliwataka wananchi watakaotembelea mabanda ya
Mahakama wakati wa maonesho ya Wiki ya utoaji wa elimu ya sheria wapate fursa
ya kujifunza ni kwa kiasi gani Mahakama
ya Tanzania imejipanga kutoa haki katika Karne ya 21 kwa ufanisi kwa matumizi
hayo.
Mifumo mingine ya TEHAMA inayofanya
kazi katika Mahakama ya Tanzania ni Mfumo ya Kielekitroniki
wa Kusajili na Kuratibu Mashauri (JSDS2), ambao ulizinduliwa na Mhe. Rais wa
Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Februari
6, mwaka jana. 2019.
‘Itakuwa faida kubwa kwao endapo wananchi wataelewa utaratibu
wa kufungua shauri kielekitroniki, kupokea wito kuhudhuria shaurini na hata
kupata taarifa za shauri kwa njia ya ujumbe mfupi wa simu,’ alisisitiza Jaji
Mkuu.
Alitaja mifumo mingine
inayotumiwa na Mahakama kuwa ni wa ramani
ambao unaonesha Mahakama za ngazi zote,
na taarifa za kila Mahakama na hali ya kila jengo la Mahakama nchini (Judiciary Map—JMAP). Mingine ni ule wa
kuwatambua Mawakili wenye leseni wanaotoa huduma za Uwakili (TAMS) na majina ya
Madalali wenye leseni hai.
Alisema mfumo mwingine ni ule wa kuhifadhi Hukumu za Mahakama
(TANZLII), ambapo kupitia mfumo
huo, hukumu 1,523 za Mahakama ya Rufani ziliwekwa hadi kufikia Disemba 13, 2019. Hukumu (maamuzi) za
Mahakama za Mahakama Kuu Masjala Kuu na kanda za Mahakama Kuu yalikuwa mashauri
1,297, wakati Mahakama Kuu—Divisheni ya Ardhi mashauri
yalikuwa 433, Mahakama
Kuu—Divisheni ya Biashara 238,
Mahakama Kuu—Divisheni ya Rushwa na Uhujumu Uchumi,72 na Mahakama Kuu—Divisheni ya Kazi 76.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akizungumza
na waandishi wa habari kuhusu Maadhimisho ya Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa
Elimu ya Sheria, itakayoanza Januari 31
hadi Februari 5, mwaka huu na Siku ya
Sheria itakayofanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dodoma. . Hafla hiyo imefanyika leo Januari 27, mwaka huu kwenye ukumbi wa
Mahakama ya Rufani Tanzania. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya
Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni