Jumatatu, 27 Januari 2020

RAIS MAGUFULI MGENI RASMI KILELE CHA SIKU YA SHERIA DAR ES SALAAM

Na Mary Gwera, Mahakama

Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli anatarajiwa kuwa mgeni rasmi katika kilele cha Maadhimisho ya Siku ya Sheria nchini  itakayofanyika  jijini Dar es Salaam, Februari 06, 2020.
 
Akizungumza na Waandishi wa Habari mapema Januari 27 mwaka huu, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliwaambia Wanahabari hao kuwa Siku hiyo ya Sheria itatanguliwa na Wiki ya Sheria ambayo ni mahsusi kwa ajili ya utoaji wa Elimu ya Sheria na taratibu za kimahakama.

“Katika Wiki ya Sheria kutakuwa na Maonesho ya utoaji elimu ya Mahakama yatakayofanyika rasmi kuanzia Januari 31, 2020 hadi Februari 5, mwaka huu katika viwanja vya ‘Nyerere Square’ jijini Dodoma na Mahakama mbalimbali nchini,” alieleza Mhe. Jaji Mkuu.

Mhe. Jaji Mkuu aliongeza kuwa kutakuwa na Matembezi maalum ya uzinduzi wa Wiki ya Sheria yatakayofanyika Februari 01, 2020 ambapo Mgeni rasmi kwenye matembezi hayo anatarajiwa kuwa ni Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job Yustino Ndugai (Mbunge). 

Mhe. Jaji Mkuu alisema matembezi hayo yataanzia Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dodoma na kuishia kwenye viwanja vya Nyerere Square ambapo ndipo maonesho ya wiki ya sheria yatakapofanyikia.

Mbali na Mahakama, maonesho hayo yatahusisha Wadau muhimu wa Mahakama wakiwemo; Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Wakili Mkuu wa Serikali, Ofisi ya Taifa ya Mashtaka, Ofisi ya Mkemia Mkuu wa Serikali, Tume ya Haki za Binadamu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA), Polisi, Magereza, Chama cha Wanasheria Tanganyika (TLS) na wengine.

“Naomba kutoa wito kwa wananchi kutembelea Maonesho hayo ambayo yatafanyika katika maeneo mbalimbali nchini ili kupata huduma na taratibu za ufunguaji wa mashauri, Sheria na taratibu zinazotumika katika kuendesha mashauri, Taratibu za mashauri ya mirathi, jinai, mifumo mbalimbali ya TEHAMA-Mahakamani, na mengineyo,” alisisitiza Mhe. Jaji Mkuu.

Maudhui ya Maadhimisho haya yanaashiria kuanza rasmi kwa mwaka mpya wa shughuli za Mahakama na huwa yanaambatana na kauli mbiu yenye maudhui mahsusi ya kutoa elimu kwa umma juu ya shughuli za utoaji haki. Maudhui ya Mwaka 2020 ni: “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.’’

Akizungumzia juu ya maudhui hayo, Mhe. Jaji Mkuu alisema kuwa yanaweka wazi kwamba, sheria, utawala wa sheria na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Kwa upande wa Dar es Salaam, Maonesho ya Wiki ya Sheria yatafanyika katika Viwanja vya Maonesho vya Mnazi-Mmoja na hafla ya kilele itafanyika katika eneo la Mahakama Kuu-Dar es Salaam kwa tarehe tajwa.


Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (kulia) akizungumza na waandishi wa habari (hawapo pichani) kuhusu Maadhimisho ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya  Sheria, itakayoanza Januari 31 hadi Februari 5, mwaka huu  na Siku ya Sheria nchini itakayofanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dodoma. Mkutano huo imefanyika leo  Januari 27, mwaka huu kwenye ukumbi wa Mahakama ya Rufani Tanzania. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi.
Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (katikati) akiwaonyesha  waandishi wa habari kitabu cha Mwongozo wa Utumiaji wa Huduma za Mahakama, ambapo taratibu zimewekwa  kwa lugha nyepesi ili kumwezesha mwananchi kuelewa kwa urahisi. Katika mkutano huo Mhe. Jaji Mkuu alizungumzia kuhusu Maadhimisho  ya Wiki ya Utoaji wa Elimu ya  Sheria, itakayoanza Januari 31 hadi Februari 5, mwaka huu  na Siku ya Sheria itakayofanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dodoma. Kushoto ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi. Kulia ni Naibu Msajili wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Eddie  Fussi.

 Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Fdeleshi akifafanua jambo kwa waandishi wa habari.
                  Baadhi ya Maafisa wa Mahakama na waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.
                         Baadhi ya waandishi wa habari wakati wa mkutano huo.

(Picha na Magreth  Kinabo – Mahakama) 


Hakuna maoni:

Chapisha Maoni