Ijumaa, 24 Januari 2020

MKUU WA WILAYA TEMEKE KUTUMIA MAHAKAMA INAYOTEMBEA KUTOKOMEZA UCHANGUDOA


Na Magareth Kinabo- Mahakama
Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bw.Felix Lyaniva amesema kwamba atahakikisha anatumia Mahakama Inayotembea mara kwa mara ili kutokomeza vitendo vya biashara ya uchangudoa, uhalifu, unywaji wa pombe za saa za kazi, uhalifu, uzururaji na uchafuzi wa mazingira katika eneo lake.
Kauli hiyo imetolewa leo Januari 24, mwaka huu wakati Mahakama hiyo, ilipokuwa ikiendesha mashauri yaliyoletwa mahakamani hapo kwa ngazi ya Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive maarufu kama ‘Mahakama ya Jiji'.

Mashauri hayo  yanahusu watuhumiwa walikamwatwa baada ya Manispaa ya Temeke, kufanya operesheni maalum ya watu wanaojihusisha na makosa makosa hayo.
Huduma hiyo iliyokuwa ikitolewa katika viwanja vya Zakhem vilivyoko Mbagala jijini Dar es  Salaam.
‘Mahakama Inayotembea ni suluhisho la kutokomeza vitendo vya biashara ya uchangudoa, uhalifu, unywaji wa pombe saa za kazi na uhalifu. Tunataka watu wafanye kazi halali na kufuata sheria za nchi,’ alisema Lyaniva huku akiongeza kwamba hataki kuona vitendo hivyo kwenye eneo lake.
Alisema watuhumiwa hao, walikamatwa na ushahidi ukiwepo.
Lyaniva aliongeza kwamba anaiomba Mahakama ya Tanzania, kutoa huduma hiyo mara kwa mara kwenye wilaya hiyo, ikiwezekana kwa kila Ijumaa.
Akizungumza kuhusu watuhumiwa waliofikishwa mahakamani hapo, Mratibu wa Mahakama hiyo, Mhe Moses Ndelwa, ambaye pia ni Hakimu Mkazi alisema wako takribani 50.
Hivyo mashauri hayo yanasikilizwa, baada ya kupokea maelezo kutoka kwa waendesha mashitaka na wapelelezi.
Ndelwa alifafanua kwamba watuhumiwa hao wametonzwa faini ya Sh. 20,000 hadi 50,000 kulingana na makosa waliyotenda.

Naye Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Suzan Kihawa alisema watuhumiwa hao , wanakiri makosa ndio maana hayahitaji uchunguzi hali iliyosababisha kusikilizwa kwa haraka.

Mashauri hayo yalisikilizwa na Hakimu Mkazi Mkuu wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Sokoine Drive, Aziza Kalli.
Wakati huohuo, baadhi ya wakazi wa Mbagala, wakizungumza kwa nyakati tofauti, ambao ni Adamu Juma alisema tukio hilo limemfundisha kwamba unaweza kukamatwa na kuhukumiwa hapo kwa hapo.
Wengine ni Hamisi Ally umri wa miaka (22), Said Hemed (20), Eva Michael(40) na Abuu Ramadhani walisema wanaishukuru Serikali kwa kuleta huduma hiyo, ambayo inakwenda vizuri na kuwezesha mashauri kusikilizwa kwa wakati na kupunguza mlundikano wa mahabusu au kesi kuchukua muda mrefu.
Pia Mahakama hiyo itawasaidia kupunguza vitendo hivyo katika eneo hilo.

 Mkuu wa Wilaya ya Temeke, Bw.Felix Lyaniva (kulia) akizungumza jambo leo  na Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Wilaya ya Temeke, Mhe. Suzan Kihawa (katikati) kuhusu  operesheni ya kutokomeza vitendo vya biashara ya uchangudoa, uhalifu, unywaji wa pombe za saa za kazi,  uhalifu, uzururaji na uchafuzi wa mazingira katika eneo lake katika viwanja vya viwanja vya Zakhem vilivyoko Mbagala jijini Dar es Salaam.


Gari maalum la Mahakama Inayotembea likiendelea kutoa huduma. pembeni watu wakishuhudia tukio na huduma hiyo.



 Baadhi ya watu wakishuhudia huduma na watuhumiwa hao.


Baadhi ya watu wakishuhudia huduma na watuhumiwa hao.
(Picha na Magreth Kinabo - Mahakama







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni