Ijumaa, 31 Januari 2020

TIMU YA WANAMICHEZO KUTOKA ZANZIBAR YAWASILI KUSHIRIKI WIKI YA SHERIA 2020


Na Tawani Salum, Mahakama

Jumla ya Wanamichezo 45 kutoka Wizara Katiba na Sheria Visiwani Zanzibar wamewasili Jijini Dar es Salaam kwa ajili ya maadhimisho ya wiki ya sheria inayoanza rasmi Januari 31, 2020 na kilele chake Februari 06 mwaka huu.

Wanamichezo hao ambao wanaume ni 28 na wanawake 17 wamewasili katika  Mashindano  ya michezo mbalimbali ambayo itafanyika katika viwanja vya shule ya Sheria kwa vitendo (LST) Mawasiliano Jijini Dar es Salaam.

Michezo hiyo itakuwa ni mpira wa miguu ambapo itakuwa kwa upande wa wanaume, kuvuta Kamba ambapo itajumuisha wanaume na wanawake pamoja na kufukuza kuku mchezo huu nao utakuwa kwa upande wa wanaume na wanawake.

Kwa mujibu wa Kiongozi wa Msafara huo, Dkt. Salum Ahmed ambaye pia ni Afisa Sera Mwandamizi, Wizara ya Katiba ya Sheria  ya Zanzibar amesema kuwa Wanamichezo hao kutoka  Wizara ya Katiba na Sheria Visiwani Zanzibar inajumuisha  Taasisi mbalimbali 11.

Alizitaja Taasisi hizo ambazo ni Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashitaka, Mahakama, Sera, Mipango na Utafiti, Ofisi Kuu Pemba, Utumishi na Uendeshaji, Afisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali, Tume ya kurekebisha Sheria, Huduma za msaada wa kisheria na nyinginezo. 

Kiongozi huyo alisema kuwa, wanamichezo hao 44 wanatoka katika ofisi hizo, na daktari kutoka Wizara ya afya Zanzibar ambapo inafanya idadi yao kufikia wanamichezo 45.

“Mwaliko huu umelenga  kudumisha muungano wetu ambapo umeasisiwa na viongozi wetu Abeid Aman Karume pamoja na Mwalimu Julius Kambarage Nyerere na umeendelea na kusimamiwa na kudumishwa na Rais wetu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Ris John Pombe  Magufuli pamoja  na Rais wa Zanzibar na mwenyekiti Baraza la Mapinduzi Mhe.DK, Ali Mohamed Shein,” alieleza Dkt Ahmed.

Pia aliongelea kuhusu umuhimu wa ushiriki katika mashindano hayo ni kudumisha ushirikiano baina ya taasisi mbili Wizara ya katiba na sheria Zanzibar na Wizara ya katiba na sheria Tanzania Bara kupitia Mahakama ya Tanzania.

Wakati huohuo Mwenyekiti wa Michezo wa Mahakama ya Tanzania, Mhe.Kifungu Mrisho Kariho ambaye ameratibu ushirikishwaji wa Zanzibar katika wiki ya sheria mwaka huu 2020 amesema kuwa mashindano hayo ni  muhimu katika kujenga mahusiano ya kiudugu katika kutoka pande zote mbili.

“Mashindayo haya yatasaidia kuimarisha afya na kubadilishana  mbinu za kisasa na maboresho  katika utendaji wa kazi kwa kuzingatia kauli mbiu ya siku ya sheria mwaka huu uwekezaji na biashara wajibu wa Mahakama na wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji,” Mhe. Mrisho.

Mashindano haya ya wiki ya sheria hufanyika kila mwaka wakati wa kipindi hiki cha wiki ya sheria ambapo washiriki kutoka Visiwani Zanzibar hushirikiana na wenzao kutoka Tanzania Bara na hususani kutoka Jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya Wanamichezo hao wakiwasili kutoka Visiwani Zanzibar tayari kushiriki  katika mashindano  ya wiki ya sheria yatakayoanza kutimua vumbi mnamo 01/02/2020 katika viwanja vya Shule ya Sheria na Vitendo jijini Dar es Salaam.
 Baadhi ya Washiriki kutoka Visiwani Zanzibar wakipokelewa na mwenyeji wao, Bw.Fadhili Mmbaga, Afisa Utumishi-Mahakama Kuu (wa kwanza kulia) na wa pili kushoto ni mkuu wa Msafara huo, Dkt. Salum Ahmed ambaye pia ni Afisa Sera katika Wizara ya Katiba na Sheria Zanzibar wengine kushoto ni baadhi ya wanamichezo kutoka Visiwani Zanzibar.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni