Jumamosi, 1 Februari 2020

MAKONDA: WANA DAR ES SALAAM TEMBELEENI MAONESHO YA WIKI YA SHERIA MNAZI MMOJA


Na Mary Gwera, Mahakama

Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda ametoa rai kwa wananchi wa mkoa huo kutembelea Maonesho ya Wiki ya Utoaji elimu ya Sheria yanayofanyika katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam ili kupata elimu ya sheria.

Mkuu huyo wa Mkoa ambaye alikuwa Mgeni rasmi katika uzinduzi wa Maonesho hayo yaliyotanguliwa na  matembezi maalum yaliyofanyika mapema Februari 01, 2020 kuanzia Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu hadi Mnazi Mmoja, alisema kuwa Maonesho hayo ni fursa kwa wananchi kupata haki zao.

“Mahakama ndio chombo pekee chenye mamlaka ya mwisho ya utoaji haki nchini, hivyo niwaombe wananchi wote wenye shida mbalimbali za kisheria kufika Mnazi Mmoja kupata msaada wa sheria badala ya kufika ofisi ya Mkuu wa mkoa kwa lengo la kutatuliwa changamoto za kisheria,” alieleza Mhe. Makonda.

Aidha, Mhe. Makonda amewaomba Watumishi wa Mahakama wanaotoa huduma katika maonesho hayo kuwaelimisha wananchi kuhusiana na masuala ya mirathi, watoto, ardhi na kadhalika kwani ndio masuala yenye changamoto kubwa.

Kwa upande wake, Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha amewahakikishia wananchi kuwa Mahakama imejipanga kikamilifu kutoa huduma ya elimu ya sheria hivyo amewataka kutembelea maonesho yanayoendelea Mnazimmoja na katika maeneo mbalimbali nchini.

“Wananchi waje kwa wingi kututembelea, tunatoa ushauri wa kisheria na kila tatizo litakalobebwa katika maonesho haya litafanyiwa kazi na kujibiwa ipasavyo,” alisisitiza Mhe. Jaji Mlacha.

 Wiki ya Utoaji elimu ya sheria inaendelea kufanyika katika Mahakama zote nchini ambapo kitaifa Maonesho hayo yanafanyika katika Viwanja vya ‘Nyerere Square’ jijini Dodoma.

Wiki ya utoaji elimu ya sheria itahitishwa na kilele cha Siku ya Sheria nchini itakayofanyika Februari 06, mwaka huu ambapo Mgeni rasmi anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Joseph Magufuli.
 Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda akizungumza wakati wa uzinduzi rasmi wa Wiki ya Utoaji Elimu ya Sheria katika Viwanja vya Mnazi Mmoja jijini Dar es Salaam.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha (kushoto), Mkuu wa mkoa wa Dar es Salaam, Mhe. Paul Makonda (kulia) pamoja na Wahe. Majaji wengine wa Mahakama na Watumishi wengine wa Mahakama wakifanya mazoezi katika Viwanja vya Mnazi Mmoja mara baada ya matembezi maalum ya uzinduzi wa wiki ya utoaji elimu ya sheria.
Mazoezi yakiendelea katika Viwanja vya Mnazi Mmoja mapema Februari 01, 2020.
Ukaguzi wa mabanda.
Meza Kuu pamoja na baadhi ya Mahakimu walioshiriki katika uzinduzi wa wiki ya sheria.
Meza Kuu katika picha ya pamoja na sehemu ya Naibu Wasajili wa Mahakama.
Mgeni rasmi (katikatik) pamoja na Wahe. Majaji walioketi wakiwa katika picha ya pamoja na Wanamichezo kutoka Wizara ya Katiba na Sheria ya Zanzibar.
Sehemu ya Watumishi wa Mahakama wakiwa wakifuatilia hafla ya uzinduzi rasmi wa Wiki ya Utoaji elimu ya sheria-Dar es Salaam.

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni