Jumamosi, 1 Februari 2020

BUNGE KUSHIRIKIANA NA SERIKALI KUIPATIA MAHAKAMA RASILIMALI


Na Magreth Kinabo- Mahakama
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Job  Ndugai ameahidi kushirikiana na Serikali kuhakikisha Mahakama ya Tanzania inapata rasilimali za kutosha ili iweze  kuendelea  kutimiza  jukumu  lake la msingi la kutoa haki kwa wakati.

Spika ameyasema hayo alip[okuwa akizindua rasmi Wiki ya  Utoaji  wa Elimu ya Sheria iliyoambatana na   matembezi  maalum ya kilomita tano yaliyoanza kwenye Viwanja vya Mahakama Kuu  Dodoma hadi kwenye Viwanja vya Nyerere Square jijini

‘’Bunge litashirikiana na Serikali, kuhakikisha  Mahakama inapata rasilimali za kutosha ili iweze kutekeleza majukumu yake ya kutoa haki kwa wakati,’’ alisema Spika.

Aidha Spika alitoa wito kwa wakazi wa Dodoma,  kuhudhuria katika viwanja   hivyo ili wapate nafasi ya kujua  haki zao na kupata elimu ya sheria kwa kuwa Mahakama si sehemu ya kuogopwa.‘ wananchi wakielewa haki zao hawatadanganywa,’ alisisitiza.

Spika pia aliipongeza Mahakama kwa kauli mbiu yake ya mwaka huu inayosema ‘Uwekezaji  na Biashara: Wajibu   wa Mahakama na Wadau  kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.’ Kwa kuwa inasaidia kufikisha dhamira ya Serikali  ya Awamu ya Tano kujenga uchumi imara  na viwanda.

Kwa upande wake Mkuu wa Mkoa wa  Dodoma, Dkt. Bilinith  Mahenge aliishukuru Mahakama ya Tanzania kwa kujenga majengo ya mkoani humo. 

Katika  maonesho hayo, Spika pia alizindua Vitabu Vitatu vya Muongozo wa Kusikiliza Mashauri  Mahakamani vinatumika  Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mkoa na Mahakama Kuu ( A hand book for Magistartes in Primary Courts, A guick reference for Magistrates in the District Court and Courts of Resident Magistrtes in Tanzania and  Bench Book for Judges in Tanzania).

Akizungumzia kuhusu vitabu hivyo, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer  Feleshi,  alisema vitabu vimeshawekwa kwenye Tovuti ya Mahakama ya Tanzania.

Wiki  hiyo imeanza Januari 31, mwaka huu na inatarajia kumalizika Februari 5, mwaka huu, ambapo kilele chake cha Siku ya Sheria nchini kitafanyika Februari 6, mwaka huu jijini Dar es Salaam kwenye ukumbi wa mikutano wa Mwalimu J. K. Nyerere. 

Mgeni rasmi katika kilele hicho, anatarajiwa kuwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli.
 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai. akiwa na Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma pamoj na viongozi wengine mara baada ya kumaliza Matembezi leo jijini Dodoma.

 Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai. akiwa katika moja ya mabanda kwenye maonesho ya wiki ya Sheria.
 Spika wa Bunge Mhe. Job Ndugai akionesha Vitabu Vitatu vya Muongozo wa Kusikiliza Mashauri  Mahakamani vinatumika  Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mkoa na Mahakama Kuu ( A hand book for Magistartes in Primary Courts, A guick reference for Magistrates in the District Court and Courts of Resident Magistrtes in Tanzania and  Bench Book for Judges in Tanzania) alipovizindua rasmi.

                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                                         

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni