Na
Lydia Churi-Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema haitoshi kwa nchi kuwa na sheria katika
vitabu endapo sheria hizo hazieleweki, hazistawishi na haziboreshi maisha ya
wananchi.
Akizungumza baada ya
Matembezi ya kuzindua wiki ya Sheria ambayo hutumika kutoa elimu ya sheria leo
jijini Dodoma, Jaji Mkuu amesema ubora wa sheria siyo maandishi yaliyomo kwenye
sheria husika bali ni sheria kuwa na malengo yenye manufaa kwa wananchi.
Alisema pamoja na sheria
za Tanzania kuwa na malengo maalum bado sheria hizo zinatakiwa kufanikisha
malengo ya Dira ya Maendeleo ya mwaka 2025 ambayo ni kuboresha hali ya maisha
ya watanzania, kuweka mazingira ya amani, usalama na umoja na kujenga utawala bora.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
malengo mengine ni pamoja na kuwezesha jamii iliyoelimika vyema na inayojifunza
pamoja na kujenga uchumi imara unaokabiliana na ushindani kutoka nchi nyingine.
Alisema Kauli Mbiu ya Wiki
ya Sheria mwaka huu (Uwekezaji na biashara:jukumu la Mahakama na
wadau kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji) inawataka wote waliopewa
jukumu la kutunga sheria (Bunge), kutekeleza sheria (Serikali) na jukumu la utoaji haki (Mahakama) kujiuliza
endapo wananchi walio wengi ambao ni maskini watanufaika vipi na sheria au
taratibu za kimahakama.
“Taratibu za kisheria
zinapaswa kuwa na msukumo wa kimapinduzi ili kuwawezesha wananchi kupanda kutoka
katika hali duni walizonazo na kufikia mizani sawa na watanzania wenye uwezo wa
kiuchumi”, alisema Prof. Juma.
Alisema maonesho ya wiki
ya sheria hayana budi kutumika tambua vizuizi na vikwazo vyote vya Sheria na taratibu
za utoaji haki vikiwemo vizuizi na vikwazo dhidi ya haki kwa wanyonge. Aliongeza
kuwa vikwazo hivi havianzii mahakamani ingawa Mahakama ndio sehemu ya mwisho
inapotafutwa haki.
“Misingi ya kupata haki
lazima ianze mapema wakati wa kutunga Sheria kwa kubeba dhana ya kuwawezesha wananchi
walio masikini, Bunge linapotunga sheria lijiridhishe kuwa uwezeshaji ni kiini
muhimu katika sheria husika”, alisisitiza.
Akizungumzia umuhimu wa
elimu ya sheria kwa wananchi, Jaji Mkuu alisema Mahakama haiwezi kufanikiwa
katika kutekeleza jukumu lake la utoaji haki bila ya wananchi kufahamu Sheria na Kanuni
zinazoongoza taratibu za kimahakama. Aliwataka wananchi kujitokeza kwa wingi
katika viwanja vya Nyerere Square jijini Dodoma ili kupata elimu ya masuala ya
kisheria.
Wiki ya Sheria ambayo
huambatana na utoaji wa elimu ya sheria kwa wananchi imezinduliwa rasmi leo kwa
matembezi yaliyoongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania
Mhe. Job Ndugai. Matembezi hayo pia yalihudhuriwa na viongozi mbalimbali wa serikali
pamoja na wadau wa sekta ya sheria nchini.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (Katikati) akiwa katika Matembezi ya Uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini yaliyoongozwa na Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai leo jijini Dodoma. Wa kwanza kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, wa pili kushoto ni Katibu Mkuu wa wizara ya Katiba na Sheria, Prof. Sifuni Mchome, wa kwanza kushoto ni Jaji Mstaafu Januari Msofe na wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge.
Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai, Jaji Mkuu
wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (Kushoto) wakiwa katika Matembezi ya
Uzinduzi wa Wiki ya Sheria nchini yaliyoongozwa na Spika wa Bunge leo jijini Dodoma. Kulia Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer
Feleshi na wa pili kulia ni Mkuu wa Mkoa wa Dodoma Dkt. Binilith Mahenge.
Spika wa Bunge la Jamhuri
ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akisikiliza maelezo kuhusu kazi zinazofanywa na kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri alipotembelea mabanda ya Maonesho ya wiki ya Sheria ambayo huambatana na utoaji wa elimu ya sheria.
Jaji Mkuu
wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza.Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akizindua Vitabu Vitatu vya Muongozo wa Kusikiliza Mashauri Mahakamani vinatumika Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mkoa na Mahakama Kuu ( A hand book for Magistartes in Primary Courts, A guick reference for Magistrates in the District Court and Courts of Resident Magistrtes in Tanzania and Bench Book for Judges in Tanzania).
Spika wa Bunge la Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Job Ndugai akionyesha Vitabu Vitatu vya Muongozo wa Kusikiliza Mashauri Mahakamani vinatumika Mahakama za Mwanzo, Mahakama za Wilaya na Mkoa na Mahakama Kuu ( A hand book for Magistartes in Primary Courts, A guick reference for Magistrates in the District Court and Courts of Resident Magistrtes in Tanzania and Bench Book for Judges in Tanzania).
Baadhi ya viongozi wa Mahakama wakimsikiliza Mgeni rasmi wakati wa uzinduzi wa wiki ya Sheria leo jijini Dodoma. Mwenye miwani kushoto ni Msajili wa Mahakama ya Rufani Mteule Mhe. Kelvin Mhina |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni