Na
Mary Gwera, Mahakama
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli amewataka Viongozi
mbalimbali aliowaapisha kuwajibika ipasavyo katika majukumu yao mapya
waliyopangiwa.
Mapema Februari 03,
mwaka huu, Mhe. Rais amewaapisha Viongozi mbalimbali wa Wizara, Mahakama,
Majeshi na Mikoa aliowateua mwishoni mwa wiki kushika nyadhifa mbalimbali
katika hafla fupi ya uapisho iliyofanyika Ikulu jijini Dar es Salaam.
“Nendeni mkaijenge
Tanzania kwa manufaa ya wananchi na taifa kwa ujumla, hivyo ni wajibu wenu
kutekeleza majukumu yenu huku mkimtanguliza Mungu,” alisema Mhe. Rais.
Mhe. Rais aliongeza
kuwa hana shaka na Viongozi aliowateua huku akitoa sifa za kila mmoja wao na
kuwataka kutekeleza majukumu yao wakijua kuwa wanafahamika.
Kwa upande wake Jaji
Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amemshukuru Mhe. Rais kwa
uteuzi wa Viongozi waandamizi wa Mahakama kwani itasaidia kurahisisha utendaji
kazi.
“Mhe. Rais nikushukuru
kwa dhati juu ya uteuzi wa Viongozi wa Mahakama uliotupatia, kwa kuwa ni sehemu
muhimu katika utendaji kazi wa Mahakama, hususani upatikanaji wa Msajili Mkuu
ambaye ndiye injini ya shughuli za Mahakama, Mkuu wa Wasajili na Mahakimu wote
na vilevile kiungo kati ya Mahakama na Serikali,” alieleza Mhe. Jaji Prof. Juma.
Vilevile Mhe. Jaji Mkuu
alimshukuru pia Mhe. Rais kwa uteuzi wa Makamishna watatu (3) wa Tume ya
Utumishi wa Mahakama, kwa kuwa Tume hiyo pia ina wajibu mkubwa kwa ustawi wa
Mahakama.
Mbali na kumshukuru
Mhe. Rais kwa uteuzi wa Viongozi wa Mahakama na Makamishna wa Tume ya Utumishi
wa Mahakama, Mhe. Jaji Mkuu aliwapongeza Viongozi wote walioapishwa huku
akionyesha kufurahishwa pia na uteuzi wa Kamishna Jenerali wa Magereza kwa kuwa
ni mdau muhimu wa Mahakama.
Viongozi walioapishwa
katika hafla hiyo ni Makatibu Wakuu watano, Msajili Mkuu wa Mahakama, Msajili
wa Mahakama ya Rufani, Naibu Katibu Mkuu, Makatibu Tawala wa mikoa mitatu,
Kamishna Generali wa Magereza na Kamishna Jenerali wa Zima-moto na Uokoaji.
Aidha, katika hafla
hiyo; Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki
Feleshi alimuapisha Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Shamira Sarwatt.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe. Wilbard
Chuma kuwa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe.Kevin Mhina kuwa Msajili wa Mahakama ya Rufani (T).
Jaji Kiongozi, Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Mbuki Feleshi (kushoto) akimuapisha Mhe. Sharmillah Sarwatt kuwa Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania.
Rais wa Jamhuri ya
Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akimuapisha Mhe.Jaji Dkt. Gerald Ndika kuwa Kamishna wa Tume ya Utumishi wa Mahakama, anayeshuhudia kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma.
Baadhi ya Viongozi waliohudhuria hafla ya kuapishwa kwa Viongozi mbalimbali walioteuliwa mwishoni mwa wiki iliyopita.
Viongozi wapya wakila kiapo cha maadili.
Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli akiwa katika picha ya pamoja na Viongozi mbalimbali aliowaapisha. Kushoto ni Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma na kulia ni Katibu Mkuu Kiongozi, Mhandisi. John Kijazi.
(Picha na Mary Gwera, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni