Alhamisi, 27 Februari 2020

BENKI YA DUNIA YAONYESHA NIA KUENDELEZA MRADI WA MABORESHO MAHAKAMA


Na Mary Gwera, Mahakama

Benki ya Dunia imeonyesha nia ya kuongeza fedha za mkopo kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Kimahakama kutokana na utekelezaji mzuri wa mradi huo katika kipindi cha awamu ya kwanza kinachotarajia kukamilika katika mwaka wa fedha 2020/2021. 

Mahakama ya Tanzania na Benki ya Dunia ‘WB’ wamefanya mazungumzo juu ya mchakato wa maandalizi ya kuongeza muda na fedha kwa ajili ya utekelezaji wa Mradi wa Maboresho ya Huduma za Kimahakama.

Mazungumzo hayo yaliyoshirikisha Ujumbe kutoka Benki ya Dunia pamoja na baadhi ya Watendaji Waandamizi wa Mahakama yalifanyika mapema Februari 26, 2020 katika Ukumbi wa Mikutano wa Kitengo cha Maboresho ya Mahakama jijini Dar es Salaam.

Kwa mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma alisema miongoni mwa masuala yaliyojadiliwa yatakayopelekea kupatikana kwa fedha hizo ni pamoja na kuibua maeneo yenye changamoto na kuona ni jinsi gani yanavyoweza kufanyiwa kazi na kuboreshwa ili kupata mwendelezo mzuri wa utekelezaji toka mwanzo hadi sasa.

“Miongoni mwa maeneo yaliyopendekezwa na Benki ya Dunia kufanyiwa maboresho zaidi na Mahakama ni pamoja na kuongeza Mafunzo kwa Watumishi, kuwa usimamizi thabiti wa Mifumo ya usimamizi wa fedha na kadhalika,” alieleza Mhe. Maruma.

Kwa upande wa Mahakama wameihakikishia Wajumbe wa Benki ya Dunia kuwa watatekeleza maeneo yote yaliyopendekezwa kwa ajili ya maboresho kufikia mwezi Aprili mwaka huu.

Ujumbe huo wa Benki ya Dunia upo nchini kuanzia Februari 19 mpaka Februari 28 mwaka huu lengo likiwa ni kufanya tathmini ya utekelezaji wa mradi huo unaotekelezwa na Mahakama ya Tanzania.

Katika kipindi hicho, ujumbe huo umefanya mazungumzo na Jaji Mkuu wa Tanzania, Jaji Kiongozi na baadhi ya Viongozi na Watendaji wa Mahakama ya Tanzania na vilevile kutembelea majengo mapya ya Mahakama ambayo ni Mahakama Kuu- Kanda ya Kigoma, Mahakama Kuu- Kanda ya Musoma pamoja na Arusha kuangalia ujenzi wa Kituo Jumuishi cha utoaji haki ‘IJC.’
 Mkuu wa Kitengo cha Maboresho-Mahakama ya Tanzania, Mhe. Zahra Maruma akizungumza jambo katika kikao kati ya Mahakama na Ujumbe kutoka Benki ya Dunia.

Mazungumzo yakiendelea kati ya Wajumbe kutoka Benki ya Dunia na Mahakama.

Mtaalam kutoka Benki ya Dunia, Bw. Waleed Malik akizungumza jambo katika kikao hicho.
 

 




Hakuna maoni:

Chapisha Maoni