Na
Lydia Churi-Mahakama Dodoma
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani amesema, mageuzi
makubwa yanayofanywa na Mahakama ya Tanzania hayatafanikiwa ikiwa watumishi wa Mahakama hawatakuwa waadilifu.
Akizungumza kwenye maadhimisho
ya kilele cha Wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini mjini Dodoma leo, Jaji
Mfawidhi amesema Mahakama ya Tanzania hivi sasa inafanya mageuzi ili kuweka
mazingira bora ya uwekezaji na biashara na pia kutimiza wajibu wake wa kikatiba
wa kutoa haki.
Amewataka watumishi wa
Mahakama pamoja na wananchi wanaotumia huduma za Mahakama kujiweka mbali na vitendo vya aina yoyote ya rushwa
na ukosefu wa maadili na kuwataka wananchi wema kutokuwa na hofu kutoa taarifa kwa
Mhimili huo au kwenye Taasisi zinazopamabana na vitendo hivyo.
“Kwenye hili hatutakuwa
wapole, tutachukua hatua kwa wachache watakaojaribu kutuchafua katika wakati
huu ambao tuko kazini kuijenga Taasisi yetu”, alisema Mhe. Siyani.
Amesema Mahakama Kuu ya
Tanzania kanda ya Dodoma haitakubali kunyooshewa vidole kwa vitendo viovu kwa
kuwa wanataka kuwa mfano bora kwa watoa huduma wengine, vinara na wanaoaminika
kwa wananchi.
Jaji Mfawidhi amesema,
kwa kutimiza wajibu wake, Mahakama
inatarajia wananchi wataongeza Imani na chombo hicho na hivyo kupeleka migogoro
yao mahakamani jambo ambalo litaimarisha
utawala wa sheria na na kuweka mazingira wezeshi ya uwekezaji na biashara.
Amesema maudhui ya Wiki
ya Sheria mwaka huu yanakumbusha Mahakama na wadau wake wajibu ilionao katika
kuhakikisha Tanzania inakuwa taifa lenye uchumi wenye ushindani wa haki, maisha
bora kwa watu wake na umuhimu wa uwekaji na uimarishaji wa mazingira bora na
wezeshi, kwa lengo la kuvutia uwekezaji wa mitaji ya kibiashara ya ndani na nje
ya nchi.
Kwa mujibu wa Jaji Mfawidhi,
mazingira bora kwa uwekezaji na biashara yanategemea uwepo wa utawala na
uongozi bora hasa kwenye eneo la utoaji haki kwa misingi ya sheria. Ameongeza
kuwa moja kati ya viashiria vya ubora wa mazingira ya uwekezaji nchini ni uwepo
wa chombo imara cha utatuzi wa migogoro
ya kibiashara.
“Mahakama inao wajibu wa
kulinda utawala wa sheria, utulivu na ustawi wa nchi kwa kuhakikisha haki
inapatikana kwa wakati na kutatua migogoro kwa amani,”alisema.
Amesema Mahakama
zinatakiwa kutenda haki kwa wote bila kujali hali ya mtu kijamii, kiuchumi na
kutochelewesha haki bila ya sababu za msingi, kutoa fidia kwa wanaoathirika
kutokana na makosa ya mwingine na kwa mujibu wa sheria mahususi zilizotungwa na
Bunge na kukuza na kuendeleza usuluhishi kati ya wanaohusika katika migogoro.
Siku ya Sheria nchini huadhimishwa
kila mwaka kuashiria kuanza rasmi kwa shughuli za Mahakama kwa mwaka husika.
Siku hii hutanguliwa na wiki ya Sheria ambayo kwa mwaka huu ilianza Januari 31
na kuhitimishwa leo Februari 5, 2020. Katika kipindi cha wiki ya sheria, elimu kuhusu
masuala ya sheria na huduma mbalimbali hutolewa na Mahakama kwa kushirikiana na
wadau wake.
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani akikagua gwaride rasmi kuashiria Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Sheria na Siku ya Sheria nchini yaliyofanyika leo kwenye viwanja vya Mahakama Kuu kanda ya Dodoma.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani akipokea salaam wakati wa gwaride
rasmi la Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Sheria na Siku ya
Sheria nchini yaliyofanyika leo kwenye viwanja vya Mahakama Kuu kanda ya
Dodoma.
Jaji
wa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. George Masaju akiwa pamoja na wahgeni waalikwa kwenye Maadhimisho hayo katika Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Sheria na Siku ya
Sheria nchini yaliyofanyika leo kwenye viwanja vya Mahakama Kuu kanda ya
Dodoma.
Jaji
Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania kanda ya Dodoma Mhe. Mustapher Siyani akikagua gwaride
rasmi kuashiria Maadhimisho ya kilele cha wiki ya Sheria na Siku ya
Sheria nchini yaliyofanyika leo kwenye viwanja vya Mahakama Kuu kanda ya
Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni