Alhamisi, 12 Machi 2020

BODI YA UDHAMINI WA TAARIFA ZA MAJUZUU YA SHERIA YAJIPANGA


Na Tawani Salum, Mahakama

Bodi ya Udhamini wa Taarifa ya Majuzuu ya Sheria imejipanga kukamilisha uchambuzi wa maamuzi ya Juzuu la mwaka 2019 ifikapo Juni, 2020 na kukamilisha uchambuzi wa maamuzi ya Juzuu ya mwaka huu mwishoni mwa mwaka huu. 

Akizungumza katika  kikao cha Bodi hiyo, kilichofanyika  katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sheria kwa Vitendo jijini Dar es Salaam, Mwenyekiti wa Bodi, Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jacobs Mwambegele alisema lengo ni kuhakikisha  hadi kufikia mwaka 2021 Mahakama inaweza kutoa Majuzuu kwa awamu mbili au nne ndani ya mwaka mmoja wa fedha.   

“Bodi imekutana ikiwa tayari imeshaandaa
maamuzi kwa ajili ya taarifa za majuzuu ya Sheria ya Mwaka 2007 hadi Mwaka 2017 na katika kikao hicho kuweza kukamilisha maamuzi kwa ajili ya Juzuu la Taarifa za  Sheria la Mwaka 2018.  Majuzuu yote ya Taarifa za Sheria ambayo maamuzi yake tayari yameshachambuliwa yatakamilika baada ya uongozi wa Mahakama ya Tanzania kukamilisha taratibu za kupata mzabuni wa kufanya kazi hiyo,” alisema Mhe. Mwambegele.

Bodi hiyo ya Majuzuu ya Sheria imemaliza kikao chake  cha siku mbili (2) Machi 11 mwaka huu cha kuchambua maamuzi ya Mahakama Kuu kwa upande wa Zanzibar  na Mahakama ya Rufani Tanzania na hivyo kukamilisha kuandaa  Juzuu la Taarifa za Sheria la mwaka 2018.

Bodi hiyo ina jumla ya Wajumbe 12, ambao ni Majaji kutoka Mahakama ya Rufani, Majaji wa Mahakama Kuu Tanzania  Bara na Zanzibar, Wawakilishi wa Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na upande wa Ofisi ya Mkurugenzi wa Mashtaka wa pande zote mbili, Katibu pamoja na Mratibu wa Bodi hiyo
 


Baadhi ya wajumbe Bodi ya Udhamini wa Taarifa ya Majuzuu ya Sheria      wakiendelea  na kikao katika ukumbi wa mikutano wa Shule ya Sheria kwa Vitendo, iliyopo Barabara ya Sam Nujoma, jijini Dar es Salaam.
 Wajumbe Bodi ya Udhamini wa Taarifa ya Majuzuu ya Sheria wakiwa  katika picha   ya pamoja. Waliokaa  katikati ni Mwenyekiti wa Bodi ya Udhamini  ya Taarifa ya Majuzuu ya Sheria ambaye pia ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Jaji Jacobs Mwambegele.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni