Na
Mary Gwera, Mahakama
Jumla ya Washiriki 22
kutoka mikoa mbalimbali nchini wanashiriki katika Mafunzo ya kusajiliwa kama
Madalali wa Mahakama na Wasambaza nyaraka za Mahakama ya Tanzania yanayotolewa
na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA).
Akizungumza mapema Machi 09, 2020 wakati
akifungua rasmi mafunzo hayo yanayofanyika katika Shule ya Sheria jijini Dar es
Salaam, Mkuu wa Chuo cha ‘IJA’, Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo alisema kuwa mafunzo
haya ambayo ni ya awamu ya tano (5) kufanyika yamelenga kuwajengea uwezo
washiriki wa namna ya kufanya kazi ya udalali na usambazaji wa nyaraka za
mbalimbali za Mahakama.
“Mnamo mwaka 2017
kanuni mpya za kusimamia Kada ya Madalali na Wasambaza nyaraka za Mahakama
zilitungwa na kupitishwa na Mhe. Jaji Mkuu, miongoni mwa masuala yaliyopitishwa
ni pamoja na kutenganisha kada hizi mbili ili kuleta ufanisi zaidi,” alieleza
Mhe. Jaji Kihwelo.
Mkuu huo wa Chuo
aliongeza kuwa lengo jingine la mafunzo hayo ni kuwawezesha washiriki hao
kufanya mtihani ambao utawawezesha kupata cheti cha umahiri endapo watafaulu
mtihani akisisitiza kuwa hii ni moja ya takwa la kanuni kwa washiriki hao
kukubaliwa kufanya kazi hiyo.
Kwa mujibu wa Jaji Dkt.
Kihwelo alisema kuwa tofauti na awali, kwa sasa yeyote anayetaka kufanya kazi
hizi ni lazima awe na elimu ya angalau kidato
cha nne (4) na kuhudhuria Mafunzo yanayotolewa na Chuo hicho ili kupata hati ya
umahiri ‘certificate of competence.’
Mafunzo hayo ya siku 14 yamehudhuriwa na washiriki kutoka
mikoa mbalimbali kama Mwanza, Bukoba, Geita, Arusha, Ruvuma, Shinyanga na Dar
es Salaam na wanatarajia kupatiwa mada kadhaa na Naibu Wasajili na Mahakimu
wenye uzoefu Mahakamani.
Katika Mpango Mkakati
wa miaka mitano (5) wa Mahakama wa 2016/2017-2020/2021, miongoni mwa maeneo
yaliyopewa kipaumbele ni pamoja na kuboresha shughuli za utoaji haki ili
kujenga taswira chanya kwa jamii.
Katika kutekeleza azma
nzima ya uboreshaji wa huduma ya utoaji haki nchini, kada ya Madalali wa
Mahakama na Wasambaza nyaraka za Mahakama ilizingatiwa kwa kuwa ni mojawapo ya
makundi muhimu yanayotekeleza amri mbalimbali za Mahakama.
Pichani ni Washiriki wa Mafunzo ya kusajiliwa kama
Madalali wa Mahakama na Wasambaza nyaraka za Mahakama wakifuatilia mada inayotolewa na Mwezeshaji kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto.
Mkuu wa Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA), Mhe. Jaji Dkt. Paul Kihwelo (katikati) akiwa katika picha ya pamoja na baadhi ya washiriki wa Mafunzo hayo, kulia ni Mhe. Victoria Nongwa kutoka Kurugenzi ya Usimamizi wa Mashauri-Mahakama ya Tanzania na kushoto ni Bi. Hamisa kutoka Chuo cha Uongozi wa Mahakama.
(Picha na Innocent Kansha, Mahakama)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni