Jumanne, 10 Machi 2020

MAHAKAMA YA TANZANIA YAPIGA HATUA UWIANO WA KIJINSIA



Na Innocent Kansha - Mahakama

Mahakama ya Tanzania imepiga hatua kubwa katika uwiano wa kijinsia  wa nafasi za kazi kwenye kada mbalimbali za Utumishi wa Umma.

Mgeni rasmi kwenye hafla ya Siku ya Wanawake Duniani ya Chama cha Majaji na Mahakimu wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi, amezitaja  baadhi ya kada ambazo zina asilimia 100  ya idadi ya wanawake kuwa ni Mwanasheria wa Mahakama ya Tanzania anayeshughulikia migogoro ya kisheria inayotokea mahakamani kwa kushirikiana na Mwanasheria Mkuu wa Serikali.
Jaji Kiongozi aliitaja kada ya Maafisa Utumishi ambayo  ina idadi kubwa ya  wanawake ikilinganishwa na ile ya wanaume. Mahakama ya Tanzania ina jumla ya Maafisa Utumishi wanawake 66 na wanaume 44, sawa na asilimia 58 kati yao.

Aidha, alieleza kuwa kwa upande wa Mahakimu katika Mahakama za Mikoa na za  Wilaya mlinganyo wao upo sawa ambapo wanawake ni 467 na wanaume ni 467 pia. Katika Mahakama za Mwanzo nchini Mahakimu wanawake ni 147 na wanaume ni 203, Maafisa Ugavi wanawake ni 17 na wanaume ni 14 sawa na asilimia 55, kwa Upande wa Maafisa Habari Wanawake ni watatu na wanaume wawili sawa na asilimia 60.

Dkt. Feleshi aliwasisitiza Majaji wanawake kutumia muda wao kuendelea kuwafunza watumishi wengine wa jinsia ya kike na kuwaongoza  kwa misingi ya utendaji kazi kwa uaminifu, uadilifu, bidii ya kujituma na maarifa.

Aliwataka Majaji na Wasajili wanawake watumie kauli mbiu yake katika kutimiza majukumu yao  inayosema “Jaji ni Kiongozi na anao wajibu wa kusimamia utekelezaji wa Mpango Mkakati wa Mahakama ya Tanzania wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/20 na Utawala, kueni na upendo miongoni mwenu, majungu na fitina mahala pa kazi havina nafasi,’’ alisisitiza.

Aliongeza kuwa siku zote duniani mwanamke akifaulu mahali pa kazi panakuwa na ustawi wa hali ya juu, hivyo wakubali kusahihishwa pale inapooneka mambo hayaendi sawa ili kuondoa tofauti zao.

Naye Mwenyekiti wa TAWJA ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Joaquine De Mello aliwaasa wanawake hao  kutokubali kutumika wala kujihusisha na  vitendo vya rushwa ya ngono mahala pa kazi kwani vinadhalilisha jinsia ya kike na kuondoa utu wa mwanamke katika eneo hilo.
Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Kuu ya  Tanzania,  Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi (aliyesimama) akisisitiza jambo wakati wa hafla ya maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika Mahakama Kuu Jijini Dar es salaam (kulia kwake )ni Jaji wa Mahakama Kuu  ya Tanzania, Mhe. Joaquine De Mello ambaye pia ni Mwenyekiti wa (TAWJA) na (kushoto )ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Rehema Kerefu.



 Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe Joaquine De Mello ambaye pia ni Mwenyekiti wa Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) akitoa mada  wakati wa hafla ya kusherekea Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika Ukumbi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Jijini Dar bes salaam.




 Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakimsikiliza mgeni rasmi Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe.Dkt. Eliezer Feleshi (ambaye hayupo pichani).
                               

Baadhi ya Watumishi ya Mahakama Kuu  ya Tanzania Masijala Kuu ya Tanzania wakiwa ukumbini wakimsikiliza Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania ( ambaye hayupo pichani) wakati wa hafla ya sherehe ya kuadhimisha Siku ya Wanawake Duniani iliyofanyika mahakamani hapo  Jijini Dar es salaam wakiongozwa na Naibu Msajili Mwandamizi wa Mahakama Kuu  ya Tanzania Mhe. Messeka Chaba (wa pili Kushoto).

Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Kuu ya  Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi akiwa (katikati) akiwa  kwenye picha ya pamoja  na  baadhi ya  Majaji wa Mahakama Kuu  ya Tanzania Masijala Kuu ya Tanzania na Naibu Wasajili ambao ni wajumbe wa Chama TAWJA, (kulia) ni Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Joaquine De Mello, ambaye Mwenyekiti wa TAWJA na (kushoto) ni Jaji wa Mahakama ya Rufani ya Tanzania Mhe. Rehema Kerefu na wa kwanza kulia waliosimama ni Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharimillah Sarwatt.
 


 Baadhi ya Watumishi wa Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa kwenye hafla ya Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) wakimsikiliza mgeni rasmi Jaji Kiongozi wa Mahakama ya Tanzania Mhe.Dkt. Eliezer Feleshi (ambaye hayupo pichani).

(Picha na Innocent Kansha- Mahakama)

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni