Jumatano, 11 Machi 2020

TANZIA


Mahakama ya Tanzania inasikitika kutangaza kifo cha mtumishi wake, Mhe. Charles Herman Shoo (pichani) aliyekuwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo Ilemela-Mwanza.

Kwa mujibu wa taarifa iliyotolewa na Mtendaji, Mahakama Kuu-Kanda ya Mwanza, Bw. Sumera Manoti anasema kuwa, m arehemu Shoo amefariki dunia baada ya kupata ajali ya gari usiku wa kuamkia Machi 10, 2020 eneo la Nganza Nyegezi mkoani Mwanza.

Mwili wa marehemu unatarajiwa kuagwa Machi 11, 2020 saa 08:00 mchana katika Hospitali ya Bugando na saa 10:00 jioni safari ya kuelekea Machame-Kilimanjaro kwa mazishi yanayotarajiwa kufanyika Machi 12, 2020 itaanza. 

Marehemu Shoo alizaliwa Oktoba 22, 1979 Wilayani Arumeru mkoa wa Arusha alipata elimu ya msingi katika Shule ya Msingi ya Mkuu iliyoko Rombo mkoani Kilimanjaro.

Marehemu alipata elimu ya Sekondari katika Shule ya Sekondari ya Mkuu (kidato cha I-IV) mwaka 1995-1998, Shule ya Sekondari Karatu (Kidato cha V-VI) 1999-2001.

Baada ya kuhitimu elimu ya Sekondari, marehemu alijiunga na masomo ya Chuo kwa ngazi ya Stashahada ya Sheria katika Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto kuanzia mwaka 2007 hadi 2009. Shahada ya kwanza ya Sheria kutoka Chuo cha Mtakatifu Augustino-Mwanza 2012-2016 na baadae alijiunga na kufuzu masomo ya uanasheria kwa vitendo kutoka Shule ya Sheria Tanzania (Law School of Tanzania) mwaka 2018.

Kwa mujibu wa Bw. Manoti anasema kuwa mpaka mauti yanamkuta, marehemu alikuwa ni Mwanafunzi wa Chuo Kikuu cha Mt. Augustino Mwanza kwa ngazi ya Shahada ya Uzamili ya Sheria (LLM).

Marehemu Shoo aliajiriwa na Mahakama ya Tanzania mnamo Juni 21, 2010 akiwa Hakimu wa Mahakama ya Mwanzo. Enzi za uhai wake marehemu alifanya kazi katika vituo mbalimbali ikiwemo Mahakama ya Mwanzo Kondoa Dodoma mwaka 2010-2011, Mahakama ya Mwanzo Igarukilo-Magu Mwanza (sasa Busega Simiyu) mwaka 2011-2012 na Mahakama ya Mwanzo Ilemela-Mwanza mwaka 2012 mpaka umauti ulipomkuta Machi 09, 2020.

Marehemu ameacha mke mmoja.

Mahakama ya Tanzania imepata pengo kubwa kwa kuondokewa na mtumishi huyo hodari na mchapa kazi.

MWENYEZI MUNGU AILAZE ROHO YA MAREHEMU MAHALI PEMA PEPONI, AMINA

Maoni 3 :