Siku ya wanawake
Duniani huadhimishwa Machi 8 kila mwaka nchini Tanzania na kwingineko
ulimwenguni. Mwaka huu, Chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) kimeanza
maadhimisho hayo kwa kutoa elimu ya sheria kwa kuwalenga watoto wote ili wawe
na ufahamu na masuala yanayohusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia kwa
kuzitembelea shule kumi za msingi zilizoko jijini Dar es salaam.
Kwa mujibu wa Mwenyekiti
wa chama hicho ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De
Mello, wameanza
na shule kumi lakini mpango ni kuzifikia shule nyingi zaidi na elimu hiyo
itakuwa ikitolewa wakati wa sherehe na maadhimisho mbalimbali iliwemo siku ya
Mtoto wa Afrika.
Machi
6, 2020 wanachama wa TAWJA walitoa elimu katika shule kumi zilizopo kwenye wilaya
za Ilala, Kinondoni, Temeke, Ubungo pamoja na Kigamboni. Yafuatayo yalijiri
kwenye maeneo hayo.
Na Lydia Churi-ILALA
Mwenyekiti wa
chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake Tanzania (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa
Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine
De Mello amewataka wanawake wenye watoto kuchukua nafasi zao katika malezi ya
watoto wao ili kuwaepusha na vitendo vya ukatili wa kijinsia wanavyowezesha
kufanyiwa.
Akizungumza
na watoto wa shule za Msingi za Ilala Boma na Mkoani zilizopo wilayani Ilala
jijini Dar es salaam, Jaji De Mello alisema licha ya wanawake kuwa na majukumu
mengi bado wanatakiwa kufahamu ni changamoto gani watoto wao wanapitia tangu
wanapotoka asubuhi kwenda shule mpaka jioni wanaporudi.
Amewataka
wanawake kuwa makini na watu wanaowazunguka watoto majumbani wakiwemo ndugu
wanaoishi majumbani kwani tathmini ya matukio ya unyanyasaji wa kijinsia
inaonesha kuwa watoto wengi hufanyiwa vitendo hivyo na ndugu waliopo majumbani.
Vitendo hivyo ni pamoja na ubakaji, ulawiti kupigwa na kunyanyaswa.
Jaji
De Mello pia aliambatana na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Rehema Mgonya
na Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmilla Sarwatt ambao pia
walizungumza na watoto wa shule hizo na kuwataka kuwa makini na kufahamu sheria
inayowalinda watoto (Sheria ya Mtoto) na pia kufahamu haki za msingi za watoto
zikiwemo haki ya kuishi na kupata elimu.
Zaidi
ya wanafunzi 1300 wa shule za Msingi za Ilala Boma na Mkoani walipatiwa elimu
ya masuala ya unyanyasaji wa kijinsia.
Wanafunzi wa shule za msingi za Ilala Boma na Mkoani jijini Dar es salaam wakifurahia jambo wakati wa mazungumzo yao na wanachama wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) Kuhusu ukatili na unyanyasaji wa kijinsia dhidi ya Watoto.
Mwenyekiti wa chama cha Majaji na Mahakimu Wanawake (TAWJA) ambaye pia ni Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Joaquine De Mello akitoa elimu kwa watoto.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Rehema Mgonya akitoa elimu kwa
watoto.
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Sharmilla Sarwatt akitoa elimu kwa
watoto.
Na Magreth Kinabo-KINONDONI
Jaji Mfawidhi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi, Mhe. Sophia Wambura amewataka wazazi na walezi
waliowatelekeza watoto wao kuwajibika kuwatunza ili watoto hao waweze kupata
haki zao za msingi ikiwemo elimu, malazi na chakula.
Akizungumza
baada kutoa elimu kwa wanafunzi 667 wa shule za msingi za Kinondoni na Msisiri,
Jaji Wambura pia aliwataka wazazi na walezi kuhakikisha watoto hao wanapata pia elimu
ya kidini kwa lengo la kuwajenga kimaadili.
Naye Mwalimu wa
Shule ya Msingi Kinondoni, Joyce Julias alizitaja baadhi ya changamoto zinazowakabili
watoto watoto wa wilaya hiyo kuwa ni pamoja na wazazi kutowajibika kimalezi, kuvunjika kwa
ndoa hali inayosababisha asilimia kubwa kulelewa na bibi zao au mzazi
mmoja na kuwepo kwa mazingira hatarishi na umasikini.
Mwalimu huyo pia
aliwataka wazazi na wazee wa kimila kuacha kuwafanyia tohara watoto wa kike kwa
kuwa kitendo hicho ni ukatili wa kijinsia.
Majaji na
Mahakimu wanawake ambao ni wanachama wa chama cha Majaji na Mahakimu wanawake
(TAWJA) walitoa elimu kwa wananfunzi kuhusu masuala ya kijinsia. Majaji hao ni
kutoka Mahakama ya Rufani, ambao ni Mhe. Winfrida Korosso na Mhe. Barke Sehel,
pamoja na Majaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania ambao ni Mhe. Sophia Wambura, ambaye pia ni Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi na
Mhe. Dkt. Modesta Opiyo. Wengine ni baadhi ya Mahakimu wa Mahakama ya Hakimu
Mkazi Kinondoni na Mahakama ya Wilaya ya Kinondoni.
Jaji wa Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Winfrida Korosso akitoa elimu hiyo kwa wanafunzi wa darasa la saba na sita wa Shule ya Msingi Kinondoni na Msisiri zilizoko Wilaya ya Kinondoni Jijini Dar es Salaam.
Jaji wa Mfawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Kazi Mhe. Sophia Wambura( wa pili kulia ) akiwa katika picha ya pamoja na wajumbe waliokuwa wakitoa elimu. Kulia waliokaa ni Jaji wa Mahakama ya Rufani Mhe. Barke Sehel na mwenzake (wa pili kushoto )Mhe. Winfrida Korosso.
Na Innocent Kansha-TEMEKE
Hakimu
Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya wilaya ya Temeke Mhe. Mariam Mchomba amewataka
watoto kutambua njia sahihi za kutoa taarifa dhidi ya vitendo vya kikatili wanapofanyiwa.
Akitoa
Elimu juu ya vitendo vya kikatili dhidi ya watoto katika Shule za Msingi za Umoja
na Migurani Wilayani Temeke mkoani Dar es salaam, Hakimu huyo amezitaja baadhi
ya sehemu watoto wanazopaswa kutoa taarifa endapo watafanyiwa vitendo hivyo
kuwa ni kwa watoto wenzao, kwa marafiki, walezi, waalimu, makanisani,
misikitini na mjumbe aliye karibu na mahali mtoto aliyefanyiwa ukatili
anapoishi.
Mhe.
Mchomba alisema ukatili dhidi ya mtoto ni hatari katika jamii endapo tabia kama
hizi hazitakemewa kwa nguvu zote na kila mlezi, mzazi, jamii na serikali kwa
ujumla kwa kuwa vitachangia kwa kiasi kikubwa kuporomoka kwa maadili ya kizazi
kijacho.
Naye,
mtoa mada mwingine Hakimu Mkazi wa Mahakama ya Mwanzo Mwambao Bagamoyo Mhe.
Mwanakombo Twalib aliwakumbusha watoto kutojiunga na kushiriki katika makundi
mabaya ya kuvuta bangi, kunywa pombe na madawa ya kulevya, na vitendo vya
ulawiti kwani havikubaliki katika jamii.
Kwa
upande wake, Mwalimu Mkuu wa Shule ya Msingi Umoja Salim Matibwa alitoa
ufafanuzi juu ya aina ya kamati zilizoundwa shuleni za kupambana na ukatili
dhidi ya Mtoto kuwa ni Kamati za Nidhamu, Wazazi, Watoto Tuseme, Kamati ya
Ushauri nasaha hasa kwa wale watoto wenye matatizo ya malezi.
Mahakimu
hao pia walitoa mada zilizowaelimisha watoto juu ya mambo mengine ikiwa ni
pamoja na ukeketaji, mimba za utotoni, ajira na kazi nzito kwa mtoto, na vipigo
vinavyopita kiasi kwa wazazi na walezi.
Kwa
mujibu wa kifungu cha 4(1) cha Sheria ya Mtoto ya Mwaka 2009 Mtoto ni mtu yeyote
aliye chini ya umri wa miaka 18. Sheria hii ya mtoto inakataza ubaguzi wa aina
yeyote dhidi ya watoto.
Na Tawani Salum-KIGAMBONI
Mkurugenzi
wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya
amewataka watoto kutonyamaza wanapofanyiwa vitendo vya kikatili na badala yake
watoe taarifa ili vitendo hivyo vikomeshwe.
Akizungumza
kwa niaba ya wanachama wa TAWJA waliokuwa wakitoa elimu kwa watoto wa shule za
msingi za Vijibweni na Darajani zilizopo wilayani Kigamboni jijini Dar es
salaam, Mhe.Nkya alisema endapo mtoto atanyanyaswa kijinsia anapaswa kutoa
taarifa haraka iwezekanavyo.
Alifafanua
kuwa shauri la aina hiyo linapofikishwa mahakamani, katika usikilizwaji wake,
mtoto hataonyeshwa kwa watu ili kumlinda na pia hata hukumu ya shauri hilo haitatolewa jina la
mtoto husika. Aliwasisitiza watoto kutokaa kimya wanapofanyiwa ukatili kwani
wakikaa kimya watu waofanya vitendo hivyo wataendela kufanya kwa kujua hakuna
adhabu yoyote watakayopewa.
Aidha
Mhe. Nkya pia aliwaelimisha watoto juu ya haki zao pamoja na wajibu wao kwa
wazazi wao, aliwataka watoto wasikubali kuolewa chini ya umri wa miaka 18 hiyo
ni haki yao kimsingi kwani wanatakiwa kusoma kwa bidii.
Naye
Hakimu wa Mahakama ya Jiji Mhe. Hanifa Mwingira aliwataka watoto kutokubali
kunyanyaswa kijinsia kwa kigezo cha kutoka katika familia maskini.
Aliwaeleza
watoto hao kutomwamini mtu yeyote na endapo wataona dalili za mtu kutaka
kuwanyanyasa kijinsia wakimbie huku wakipiga kelele. Aliwataka kutokubali
kuitwa majina kama mume, mke, baby na mengineyo na namna nyingine ya kujikinga
ni kutopita vichochoni na kujiepusha na walevi.
Kwa
upande wake, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Butamo Phillip amefurahishwa
na elimu iliyotolewa na Chama cha Wanawake Cha Majaji na Mahakimu Tanzania
katika shule za Msingi za Vijibweni na kusema elimu hiyo imesaidia kuwapa ufahamu wanafunzi ni jinsi gani ya kukabiliana na unyanyasaji
wa jinsia na nini wakifanye mara ikitokea wamefanyiwa unyanyasaji huo.
Wanachama wa TAWJA waliotoa elimu ni Jaji Mhe. Butamo Phillip, Jaji wa Mahakama Kuu Mhe. Masabo, Mhe. Eva Nkya. Wengine ni Mahakimu Mhe.Hanifa Mwingira, Mhe.Agness Mchome, Mhe. Lusajo Mtuwa na baadhi ya Maafisa wa ustawi wa Jamii katika Manispaa ya Kigamboni.
Mkurugenzi wa Menejimenti ya Usimamizi wa Mashauri wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Eva Nkya akiwa na wanafunzi wa shule za msingi za Vijibweni na Darajani mara baada ya kutoa elimu.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Butamo Phillip akifurahia jambo wakati wanachama wa TAWJA walipotoa elimu kwa watoto wa shule za Msingi za Vijibweni na Darajani ziliopo kwenye wilaya ya Kigamboni.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni