Ijumaa, 6 Machi 2020

WATUMISHI MAHAKAMA YA KAZI WATOA MSAADA KWA YATIMA


Na Mary Gwera, Mahakama

Watumishi wa Mahakama Kuu, Divisheni ya Kazi wakiongozwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama hiyo, Mhe. Sophia Wambura wamefanya tendo la huruma kwa kutoa msaada wa vitu mbalimbali katika Kituo cha Watoto Yatima cha Al Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo jijini Dar es Salaam.

Akizungumza wakati wa kukabidhi msaada kwa Katibu wa Kituo hicho mapema Machi 06, 2020, Mtendaji wa Mahakama hiyo, Bi. Hellen Mkumbwa alisema wamefanya hivyo ikiwa ni sehemu ya Maadhimisho ya Siku ya Wanawake Duniani ambayo kilele chake ni Machi 08, mwaka huu.

“Leo, sisi Watumishi wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi tumeona ni vyema kujumuika na watoto hawa, lengo likiwa ni kufurahi pamoja nao kwa kidogo tulichochangishana,” alisema Bi. Mkumbwa.

Miongoni mwa vitu walivyopatiwa watoto hao ni pamoja na mchele kilo 132, maharage, unga, mafuta ya kupikia, maharage, nyama, sukari, chumvi, maziwa, majani ya chai, maji ya kunywa, sabuni na kadhalika.

Kwa upande wake, Katibu wa Kituo hicho, Bw. Hamad Kondo aliwashukuru Watumishi hao kwa kutambua uhitaji wa watoto wa Kituo hicho na kuomba makundi mengine kutosita kujitokeza kusaidia watoto hao.

Aidha; Katibu huyo alitaja baadhi ya mahitaji mengine wanayohitaji ni pamoja na vyakula, madawa, luku, mavazi pamoja na vifaa vya shule.

Kwa mujibu wa Bw. Kondo, Kituo hicho kilichoanzishwa mwaka 2004 na kina jumla ya watoto yatima 42, huku watoto wa kiume wakiwa 26 na wa kike 16 na kuongeza kuwa zaidi ya watoto 10 wanasoma katika shule mbalimbali jijini Dar es Salaam.
 Watumishi wa Mahakama ya Kazi wakitoa msaada kwa watoto yatima wa Kituo cha Al-Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo jijini Dar es Salaam.
 Sehemu ya Watoto wanaolelewa katika Kituo cha Al Madina kilichopo Tandale kwa Tumbo jijini Dar es Salaam wakifurahia baadhi ya vitu walivyopatiwa na Watumishi wa Mahakama ya Kazi.
 Watumishi wa Mahakama ya Kazi wakiwa katika picha ya pamoja na watoto mara baada ya kutoa msaada.
Jaji Mfawidhi, Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Mhe. Sophia Wambura akifurahia jambo na watoto wa kituo hicho, katika tukio hilo Watumishi wa Mahakama ya Kazi walipata fursa ya kula keki ya Maadhimisho ya Siku Wanawake Duniani ambayo kilele chake ni Machi 08, 2020.
Jaji wa Mahakama Kuu Divisheni ya Kazi, Mhe. Zainabu Muruke akikabidhi msaada kwa Mama mlezi wa Kituo hicho, Bi. Kuluthumu.

Mtendaji wa Mahakama Kuu-Divisheni ya Kazi, Bi. Hellen Mkubwa akikabidhi msaada kwa Mama mlezi wa Kituo hicho, Bi. Kuluthum.

(Picha na Mary Gwera, Mahakama)








Hakuna maoni:

Chapisha Maoni