“Mahakama imekuwa
ikitumia Tehama katika kurahisisha shughuli zake za utoaji haki nchini licha ya
kuwepo kwa ugonjwa wa Corona na baadhi ya mifumo iliyokuwa ikitumika ni pamoja
na mfumo wa kusajili na kuratibu mashauri
pamoja na mfumo wa kusikiliza mashauri
kwa njia ya mkutano mtandao (Video Conferencing),” alisema Jaji Mkuu.
Alisema matumizi ya
Tehama ndani ya Mahakama yanatokana na Mpango wa miaka mitano wa maboresho ya
huduma za Mahakama ambapo maboresho hayo sasa yatatusaidia katika kukabiliana
na kupambana na ugonjwa huu ambao umesambaa kwenye nchi nyingi duniani ikiwemo
Tanzania.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
kupitia mifumo ya Tehama iliyopo Mahakamani, wananchi na wadaawa wa mashauri
huweza kupata huduma za kimahakama bila ya kuwalazimu kufika mahakamani hivyo
kutoa fursa kwao ya kutumia muda huo kufanya shughuli za nyingine za uzalishaji
na za kijamii.
Alisema ili kutekeleza azma
yake ya kutumia Tehama, Mahakama imeweka mitambo ya kisasa ya Tehama kwenye
Mahakama Kuu Masjala Kuu jijini Dar es salaam, Mahakama kuu za Mbeya na Bukoba,
kwenye Kituo cha Mafunzo Kisutu, Chuo cha Uongozi wa Mahakama Lushoto pamoja na
kwenye magereza ya Keko na Segerea.
“Hatua ya Mahakama iliyofikiwa
katika matumizi ya Tehama itakuwa ni njia mojawapo itakayosaidia kukabiliana na
maambaukizi ya virusi vya COVID 19 kwa kuwa itaondoa mikusanyiko kwenye maeneo
ya Mahakama na wananchi kuendelea kupata huduma hizo kwa njia ya mtandao”.
Kwa sasa, mashauri yote ya
jinai jijini Dar es salaam yanayoahirishwa kutokana na sababu mbalimbali,
watuhumiwa waliopo katika magereza ya Keko na Segerea hawatalazimika kufikishwa
mahakamani, badala yake mashauri hayo yataahirishwa kwa njia ya Mahakama
mtandao ili kuepuka msongamano na mkusanyiko wa kuwaleta Mahabusu mahakamani.
Ili kupanua huduma ya
Mahakama mtandao kwenye kanda nyingine za Mahakama Kuu ya Tanzania, vifaa vya kuwezesha
huduma hiyo vitafungwa pia katika magereza yaliyopo kwenye maeneo hayo ili
huduma hiyo pia ianze kutolewa. Juhudi za kuweka vifaa hivyo kwenye kanda
nyingine zinaendelea na tunarajia baada ya muda mfupi huduma itatolewa kwenye
maeneo hayo. Kanda zenye huduma hiyo ni Mbeya na Bukoba.
Akifafanua kuhusu kanuni za
kufungua mashauri kwa njia ya mtandao, Jaji Mkuu alisema zilianza kufanya kazi April,
2018 na kuongeza kuwa kanuni hizi ni muhimu katika kufungua mashauri kwa njia
ya mtandao hivyo zitasambazwa ili kuwasaidia wananchi na wadau kufungua
mashauri bila ya kufika mahakamani.
Alitoa wito kwa wananchi
kufungua mashauri kwa njia hii ili kupunguza mikusanyiko isiyokuwa na lazima
hasa katika kipindi hiki cha maambukizi ya virusi vya Corona.
Alisema Mahakama
inawashauri wananchi, Mawakili wa Serikali na Mawakili wa kujitegemea kutoa
ushirikiano hasa upande wa mashauri ya madai kutumia njia hii ya kusajili online.
Tunatarajia hivi karibuni, hata mashauri ya jinai yatasajiliwa kupitia mitandao
itakayotayarishwa kwa ajili hiyo. Njia hii itawaondolea wananchi usumbufu wa
kusafiri kufika mahakamani na kutumia muda huo kwa shughuli za uzalishaji na
kijamii.
Aidha, Jaji Mkuu amewashauri
Viongozi wote wa Mahakama katika ngazi zote kutumia wakati huu kuonyesha uongozi wao kwa
kuwasaidia watanzania kuendelea kupata huduma za utoaji haki katika dunia
ambayo inapata msukosuko mkubwa wa ugonjwa wa Corona.
Hivi sasa Mahakama ina
mifumo mbalimbali kama Mfumo wa kusajili
na kuratibu mashauri, mfumo wa kusimamia mawakili, mfumo wa kuhifadhi maamuzi
ya Mahakama ya Rufani na Mahakama Kuu, mfumo wa video conferencing na mfumo wa
utambuzi wa majengo ya Mahakama.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni