Na Magreth Kinabo- Mahakama
Jaji Kiongozi
wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi amewakumbusha wapelelezi
na waendesha mashtaka kuhakikisha kesi za jinai zinakamilishwa upelelezi wake
kabla ya kufunguliwa mahakamani.
Aidha Jaji
Kiongozi ameziagiza Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za Wilaya
kuhakikisha kwamba kesi zinazofunguliwa zinazingatia matakwa
ya Tangazo la Serikali Na. 296 la mwaka 2012 linalotoa
mwongozo wa kesi nyingi isipokuwa zile zinazohusisha makosa makubwa
kufunguliwa baada ya kukamilishwa kwa upelelezi ili kuepusha kuongeza
mlundikano usio wa lazima magerezani.
Akizungumza na
waandishi wa habari leo kwenye Kituo cha Habari na Mafunzo cha Mahakama ya Tanzania (JMC), Dkt. Feleshi amesema kuwa kesi zote za Mahakama
za Mwanzo zifunguliwe baada ya mlalamikaji kuwa ameshandaa mashahidi wake na
Mahakama kujiridhisha mshtakiwa yupo na apewe fursa ya kuita wadhamini.
Alisema kwamba
Mahakama imechukua hatua hiyo ili kuepuka msongamano wa mahabusu na wafungwa
mahakamani, ikiwa ni jitihada ya hatua ya kuweza kukabiliana na
maambukizi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID 19 vilivyosambaa nchi nyingi duniani.
Dkt. Feleshi
alisema kutokana na matumizi ya Tehama, hivi sasa watuhumiwa waliopo katika magereza
ya Keko na Segerea hawatalazimika kufikishwa mahakamani.
‘‘Mahakama
itaongeza matumizi ya Mahakama inayotembea (Mobile Court) kwa kadri mahitaji
yanapotokea, pia inaendelea kujipanga zaidi juu ya hatua zingine za uwezeshaji wa
usikilizaji wa mashauri na upatikanaji wa huduma nyingine za kimahakama,’’
alisema Jaji Kiongozi.
Alifafanua kuwa
Mahakama itahakikisha mashauri yanasajiliwa kwa njia ya kielektroniki yanahudumiwa
mara tu yapofika kwenye mfumo na taarifa zimrudie mteja ndani ya muda mfupi. Aliongeza kuwa Mahakama kupitia Kurugenzi yake ya Usimamizi wa
Mashauri na Teknolojia ya Habari na Mawasiliano
(TEHAMA) inaandaa
timu ya itakayotoa msaada na ushauri wa kiufundi kwa saa 24.
‘Mahakama
itaendelea na mfululizo wa programu ya elimu ya namna ya kusajili mashauri,
kupata taarifa pamoja na kutoa msaada wa usajili wa mashauri kwa njia ya
kielektroniki kwa kuanza na Mahakama zenye mashauri mengi, ambazo zinaweza
kusababisha mkusanyiko wa watu wengi,’’ alisisitiza.
Alisema chini
ya usimamizi wa waheshimiwa Majaji Wafawidhi
Mahakama kwa kufuata sheria na miongozo iliyopo, zitakuwa zikitoa
ratiba za usikilizaji wa mashauri hayo kwa muda maalumu. Hivyo wadaawa
wanashauriwa kuwa makini na kuzingatia muda wanaopangiwa kufika mahakamani na
kuhakikisha namba zao za mawasiliano ziko kwenye fomu ya kufungulia kesi au
hati za kesi.
Kwa upande wake
Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Dar es Salaam, Mhe. Lameck Mlacha
aliwataka wadaawa na mashahidi kutoa ushirikiano na kuhakikisha wananawa mikono
wanapofika kwenye maeneo ya mahakamani.
Aliongeza
kwamba idadi ya watu wanaofika mahakamani ili kumwona Hakimu inapaswa kupungua na
kubaki wadaawa na mawakili tu.
Akizungumzia
mashauri, Jaji Mfawidhi huyo alisema Mahakama za Wilaya za Kinondoni na
Ilala nazo zitawekewa mfumo wa TEHAMA ili ziweze kuendesha mashauri
kwa mtandao.
Alitoa wito kwa
watumishi wa Mahakama, waadawa pamoja na wananchi kushirikiana kwa pamoja
katika kuwezesha matumizi ya TEHAMA ili kuendeleza mapambano ya kujikinga na
ugonjwa huo na haki kupatikana kwa wakati.
Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi akizungumza na Waandishi wa Habari kuhusu Hatua zinazochukuliwa na Mahakama ya Tanzania katika kuunga mkonojuhudi za Serikali katika kukabiliana na ugonjwa unaosababishwa na virusi vya Corona.
Baadhi ya Viongozi wa Mahakama ya Tanzania walioambatana na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu
ya Tanzania, Mhe.
Dkt. Eliezer Feleshi alipokuwa akizungumza na Waandishi wa Habari leo jijini Dar es salaam. Katikati ni Mkurugenzi wa TEHAMA wa Mahakama ya Tanzania Bw. Kalege Enock.
Jaji Mfawidi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es salaam Mhe. Lameck Mlacha akizungumza kwenye Mkutano huo. Kulia ni Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi. |
Waandishi wa habari kutoka vyombo mbalimbali vya habari nchini wakimsikiliza Jaji Kiongozi (hayupo pichani).
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni