Rais
wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Mhe. Dkt. John Pombe Magufuli ametuma salaam
za rambirambi kwa Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Kufuatia
kifo cha Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani aliyefariki dunia
leo katika hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam.
Jaji
Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani amefariki dunia leo saa 2:05 asubuhi katika
Hospitali ya Agha Khan jijini Dar es salaam baada ya kuugua kwa muda mrefu
maradhi ya cancer na mwishoni kupata Mshtuko wa Moyo (Heart Attack).
Rais
Magufuli amempigia simu Jaji Mkuu wa Tanzania na kumpa pole baada ya kupata
taarifa ya kifo cha Jaji Mkuu huyo Mstaafu.
“Nimepokea
kwa masikitiko makubwa taarifa za kifo cha Jaji Mkuu Mstafu Augustino Ramadhani,
napenda kutoa pole kwako, familia ya marehemu, waheshimiwa Majaji wote pamoja
na watumishi wa Mahakama ya Tanzania”, alisema Rais Magufuli.
Marehemu
Jaji Ramadhani alianza kuugua mwaka 2011 na kugundulika kuwa na ugonjwa wa Cancer
ambapo alitibiwa katika hospitali mbalimbali nje na ndani ya nchi. Hospitali
alizotibiwa ni pamoja na hospitali za Apollo na Bangalow nchini India, Afrika
ya Kusini, Nairobi Agha Khan na Dar es salaam Agha Khan.
Marehemu
Jaji Augustino Ramadhani alizaliwa tarehe 28/12/1945. Alisoma elimu ya Msingi kati
ya mwaka 1952 na 1959 wilayani Mpwapwa mkoani Dodoma. Mwaka 1960-1965 alisoma
kidato cha kwanza mpaka cha sita katika shule ya wavulana ya Tabora (Tabora Boys).
Alijiunga na masomo ya Chuo kikuu mwaka 1966 ambapo alisomea fani ya Sheria na
kumaliza mwaka 1970.
Marehemu
Jaji Ramadhani alijiunga na Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) tarehe 26/3/1970
na kulitumikia jeshi hilo mpaka Januari 1978 alipoazimwa na Serikali ya
Mapinduzi ya Zanzibar kuwa Naibu Mwanasheria Mkuu. Wakati wa vita vya Kagera
alirejea Jeshini na kwenda vitani mpaka Desemba 1979 aliporejea.
Tarehe
8/1/1980, Marehemu Jaji Augustiono Ramadhani aliapishwa kuwa Jaji Mkuu wa
Zanzibar wadhifa alioushikilia mpaka mwaka 1989 alipoteuliwa na Rais wa awamu
ya Pili Mhe. Ali Hassan Mwinyi kuwa 28/6/1989 kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani.
Aidha akiwa na wadhifa huo aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Taifa ya
Uchaguzi (NEC).
Akiwa
Mahakamani, aliendelea kupanda vyeo vya kijeshi mpaka kufikia kuwa Brigedia
Generali mwaka 1995. Mwaka 1997
alistaafu kwa hiari Jeshi.
Mwaka
2007, Rais wa awamu ya nne Mhe. Jakaya Kikwete alimteua Jaji Ramadhani kuwa
Jaji Mkuu wa Tanzania ambapo alidumu kwenye cheo hicho mpaka tarehe 27/12/2010 alipostaafu kwa mujibu wa Sheria.
Miongoni
mwa nyadhifa nyingine alizowahi kushika ni pamoja na kuwa Jaji wa Mahakama ya
Afrika ya Haki za Binadamu, wadhifa alioushika kwa kipindi cha miaka miwili
kuanzia mwaka 2014 hadi mwaka 2016.
Marehemu
Jaji Ramadhani pia aliwahi kuwa Makamu Mwenyekiti wa Tume ya Mabadiliko ya
Katiba iliyoundwa na Rais wa Awamu ya nne Mhe. Dkt. Jakaya Mrisho Kikwete Julai
4, 2012.
Mipango
ya mazishi itajulikana baadaye.
BWANA ALITOA NA BWANA AMETWAA, JINA BWANA
LIHIMIDIWE.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni