Na
Lydia Churi -Mahakama
Mwili wa aliyekuwa Jaji
Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani umeagwa rasmi leo katika
viwanja vya Karimjee huku akielezewa kuwa alikuwa ni Kiongozi mahiri na muadilifu
aliyeitumikia Mahakama ya Rufani kwa zaidi ya miaka 21.
Jaji Mkuu wa Tanzania
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amesema Marehemu Jaji Ramadhani ameacha hazina
kubwa ya maarifa, uzoefu na maono ambayo ni jukumu la watanzania kukusanya,
kuelewa na kujifunza.
Alisema Jaji Ramadhani
alidumu katika Mahakama ya Rufani kwa takriban miaka 21, kuanzia alipoteuliwa
na Mhe. Rais Ali Hassan Mwinyi mwaka 1989 kuwa Jaji wa Mahakama ya Rufani, hadi
tarehe 27 Disemba 2010, alipostaafu akiwa Jaji Mkuu.
“Miaka hiyo 21 ilikuwa ni
miaka ya kutoa maamuzi ya mwisho ya kimahakama yenye nguvu kubwa ya kisheria.
Kupitia maamuzi hayo, sauti yake ya kimaamuzi itaendelea kutuongoza kwa muda
mrefu”, alisema Jaji Mkuu.
Prof. Juma alisema kuwa
ni Majaji wachache wanajaaliwa kupata nafasi ya kutoa huduma za utoaji haki
katika Mahakama zilizo juu kwa kipindi kirefu, hivyo kutokana na uzoefu wake, jambo
lolote alilokuwa akilisema au kuliandikia, lilikuwa limebeba uzoefu na
kuboreshwa hasa kwa kuwa alifanya kazi sehemu mbali mbali.
Akimuelezea marehemu Jaji
Ramadhani, Jaji Mkuu alisema alikuwa ni mtu aliyependa
maboresho ya Mahakama na Sekta ya Sheria kwa kushiriki katika mageuzi mbalimbali
ikiwa ni pamoja na kushiriki katika hatua za mwanzo wakati Rasimu ya Sheria ya
Uendeshaji wa Mahakama (Judiciary Administration Act, 2011) ilipokuwa
ikitayarishwa kabla ya kuwasilishwa Bungeni.
Alisema marehemu Jaji
Ramadhani alipenda kutumia hukumu zake kama njia ya kuelimisha, kufafanua na
kupendekeza maboresho. Aliongeza kuwa katika miaka yake ya utumishi mahakamani alishiriki
katika kuamua mashauri mengi ambayo yalisheheni elimu, tafsiri na hata
mapendekezo ya mabadiliko ya sheria huku akiwahimiza Mawakili wa Serikali, na
wananchi kwa ujumla kuwa na utamaduni wa kusoma hukumu mbali mbali zinazotolewa
Mahakama.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
Mahakama itafanya kumbukumbu rasmi ya kumuaga Marehemu Jaji Ramadhani Kitaaluma
Mwenyezi Mungu atakapojaalia janga la COVID 19 kuisha.
Akitoa shukrani kwa Serikali,
Jaji Mkuu amemshukuru Mhe. Rais John Pombe Magufuli kwa ukaribu aliouonyesha
kwa Marehemu, tangu alipokuwa akimtembelea alipolazwa Hospitali ya Aga Khan kumjulia
hali. Jaji Mkuu pia amemshukuru Waziri Mkuu Mhe. Kassim Majaliwa Majaliwa, kwa
kufanikisha shughuli ya leo kupitia Kamati ya Kitaifa ya Mazishi ya Viongozi wa
Kitaifa ambayo yeye ni Mwenyekiti kwa mujibu wa Sheria inayoratibu Mazishi ya
Viongozi wa Kitaifa ya 2006.
Aidha amesema amepokea salaam
za pole kwa Mahakama ya Tanzania na kwa familia kutoka kwa Majaji wakuu wa Uganda,
Kenya, Rwanda, Gambia pamoja na Rais wa Mahakama ya Afrika Mashariki Prof.
Emmanuel Ugisherabuka. Wote wakielezea namna walivyomfahamu na kumheshimu Jaji
Mkuu Mstaafu Augustino Ramadhani.
Viongozi mbalimbali wa
Kitaifa walishiriki kuaga mwili wa marehemu Jaji Ramadhani wakiwemo Marais
Wastaafu wa Tanzania Mhe. Benjamin William Mkapa na Jakaya Mrisho Kikwete. Viongozi
wengine ni Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Dkt. Hussein Mwinyi aliyewakilisha
Serikali, Katibu Mkuu Kiongozi Mhe. John Kijazi, Majaji,
Makatibu Wakuu, Mabalozi, wabunge na Viongozi wa Dini.
Baba Askofu wa Kanisa
la Anglikana, Jackson Sosthness akitoa sala.
|
Sheikh Alhad Mussa Salum, ambaye ni mwakilishi wa
Muufti akiomba dua.
|
Baadhi ya Majaji wa
Mahakama ya Rufani Tanzania na Mahakama Kuu ya Tanzania wakiwa katika Mazishi
hayo.
|
Baadhi ya viongozi wa
Vyombo vya Ulinzi na Usalama na Wadini wakiwa katika Mazishi hayo.
Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu Tatu, Mhe. Benjamin Mkapa akitoa heshima za mwisho kwa mwili
wa marehemu.
|
Mke wa Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu Tatu, Mama Anna Mkapa akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa
marehemu.
|
Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu Nne, Mhe. Jakaya Kikwete akitoa heshima za mwili wa marehemu.
|
Rais Mstaafu wa
Serikali ya Awamu Nne, Mhe. Jakaya Kikwete na mkewe Mama Salma Kikwete wakitoa
pole kwa familia ya marehemu.
|
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania, Mhe. Barnabas Samatta
akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu.
|
Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania,
Mhe. Mohamed Chande Othman akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu.
|
Rais wa Mahakama ya
Afrika, Mhe. Sylvain Ore akimzungumzia marehemu.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni