Na Innocent Kansha – Mahakama
Aliyekuwa Jaji
Mkuu Mstaafu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, marehemu Augustino Stephen
Lawrence Ramadhani, ameagwa leo Mei, Mosi, mwaka huu katika ukumbi wa Karimjee uliopo
Jiji Dar es salaam.
Akitoa salamu za rambirambi kwa
familia ya marehemu na Watanzania wote kwa ujumla Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe,
Prof, Ibrahim Hamis Juma kwa niaba ya Mahakama ya Tanzania alisema anapenda
kutoa shukrani tele kwa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. John
Pombe Joseph Magufuli kwa salamu zake za rambi rambi alizotoa mara baada ya
kujulishwa kifo cha Jaji Mstaafu Ramadhani.
“Namshukuru sana Mhe. Rais kwa
ukaribu aliouonyesha kwa marehemu, tokea wakati alipokuwa akimtembelea alipolazwa
Hospitali ya Aga Khan na kumjulia hali. Mahakama ya Tanzania haitasahau msaada
wako wa
hali na mali”, alieleza Jaji
Mkuu.
Mhe. Prof. Juma alimuelezea marehemu
kama mtumishi mahiri, muadilifu,
mwadilifu aliyetakiwa na kila Taasisi ndani
na nje ya nchi wasifu wa marehemu Jaji Ramadhani unaonyesha uwezo wake mkubwa
na umahiri katika sehemu zote alizopitia, Mtumishi wa Umma wa aina hii
hugombewa na taasisi mbali mbali.
“Ni Majaji wachache wanajaaliwa
kupata nafasi ya kutoa huduma za utoaji haki katika Mahakama zilizo juu katika
kilele kwa kipindi kirefu cha miaka 21. Hivyo basi, jambo lolote alilokuwa
akilisema au kuliandikia, lilikuwa limebeba uzoefu wa miaka mingi ya utumishi,
bali uliobereshwa kwa uzoefu wa sehemu mbali mbali alizofanya kazi.
“Jaji Ramadhani alianzisha na
alishiriki kikamilifu katika maboresho ya Mahakama ya Tanzania yanayoendelea
hivi leo ameshiriki katika mageuzi mengi na maboresho ya sekta ya Sheria.
Alishiriki katika hatua za mwanzo wakati Rasimu ya Sheria ya Uendeshaji wa Mahakama
(Judiciary Administration Act, 2011) ilipokuwa ikitayarishwa kabla ya
kuwasilishwa Bungeni, mosi ikiwa ni kutenganisha shughuli za kimahakama na
kiutawala”, alifafanua Prof. Juma.
Alitetea sana matumizi ya
Teknologia ya Habari na Mawasiliano(TEHAMA) wakati Majaji na Mahakimu walikuwa
bado wana sita kutumia teknologia hiyo, dhamira yake na nia kwamba Mahakama ya
Tanzania iingie katika matumizi ya TEHAMA kuboresha shughuli zake za kila siku
za utoaji haki nchini.
Alifafanua kuwa katika kipindi
hiki cha ugonjwa wa COVID 19 inatulazimu kusikiliza mashauri mahakamani kwa kutumia
teknologia hiyo.
Hivyo alipenda kutumia hukumu zake kama njia ya
kuelimisha, kufafanua na kupendekeza Maboresho, pia alishiriki katika kuamua mashauri mengi ambayo yalisheheni elimu,
tafsiri na hata mapendekezo ya mabadiliko ya sheria, siku zote aliwahimiza
Mawakili wa Serikali na wananchi kwa ujumla wawe na kawaida ya kusoma hukumu
mbali mbali zinazotolewa Mahakamani.
Marehemu Ramadhani alifariki
dunia mnamo April 28, 2020 saa moja asubuhi katika Hospitali ya Aga Khan
kutokana na maradhi yaliyomsumbua kwa muda mrefu.
Katibu Mkuu Kiongozi,
Mhe. Balozi John Kijazi akitoa heshima za mwisho kwa mwili wa marehemu.
|
(Picha na Magreth
Kinabo- Mahakama.)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni