Na Lydia
Churi- Mahakama
Mwili wa aliyekuwa Jaji
Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani umezikwa leo katika makaburi
ya familia yaliyopo Kimara King’ong’o baada ya ibada ya kumuaga iliyofanyika
katika kanisa la Anglikana la Mt. Albano jijini Dar es salaam.
Ibada hiyo iliyoongozwa
na Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es salaam Mhashamu Jackson Sosthenes ilihudhuriwa na Waziri wa Mambo ya Nje
na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi pamoja na Viongozi
mbalimbali kutoka Taasisi za Serikali, Mahakama na Taasisi za Kidini.
Akimuelezea Marehemu Jaji
Augustino Ramadhani, Prof. Kabudi alisema alikuwa ni aliyefanya mageuzi makubwa
na maendeleo ya Zanzibar. “huwezi kuzungumzia mageuzi na maendeleo ya Zanzibar bila
ya kumtaja Jaji Ramadhani”, Tanzania imepoteza mtu muhimu, hodari, muadilifu na
mchapakazi”,alisema.
Aidha, mwili wa Jaji Mkuu
Mstaafu huyo ulizikwa kwa heshima zote za kijeshi kwa kupigiwa mizinga 21 kama
ishara ya kutoa heshima za mwisho kwa Brigedia wao taratibu za kijeshi.
Wakati huo huo Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ) limemuelezea Brigedia Generali Augustino Ramadhani
kuwa ni mtu makini, muadilifu na mchapakazi na kuwa jeshi hilo limempoteza mshauri
na mwalimu wa masuala ya kijeshi.
Akitoa salaam za jeshi
hilo kwa niaba ya Mkuu wa Majeshi, Generali Venance Mabeyo, Meja Generali
Shariff Othman alisema Mkuu wa Majeshi amepokea taarifa za msiba huo kwa masikitiko
makubwa na kwa niaba ya jeshi hilo anatoa pole kwa familia kutokana na
kumpoteza mpendwa wao.
Naye mtoto wa marehemu
Bw. Francis Ramadhani aliishukuru Serikali, Mahakama ya Tanzania, Jeshi la
Wananchi wa Tanzania (JWTZ), Waumini wa kanisa la Anglikana pamoja na wananchi
wote kwa ujumla kwa kuonyesha mshakamano mkubwa katika msiba wa baba yao.
Jaji Ramadhani alifariki
dunia Aprili 28, mwaka huu saa 1:00 asubuhi katika Hospitali ya Agha Khan
jijini Dar es salaam, baada ya kuugua kwa muda mrefu maradhi ya saratani na mwishoni kupata Mshtuko wa Moyo (Heart
Attack).
Marehemu Jaji Ramadhani
alianza kuugua mwaka 2010 na kugundulika kuwa na ugonjwa wa saratani ambapo
alitibiwa katika hospitali mbalimbali nje na ndani ya nchi. Hospitali alizotibiwa
ni pamoja na hospitali za Apollo na Bangalore nchini India, Afrika ya Kusini,
Nairobi Agha Khan na Dar es salaam Agha Khan.
Jeneza lenye Mwili wa aliyekuwa Jaji
Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani likiingizwa kaburini wakati wa Mazishi yaliyofanyika kwenye Makaburi ya Familia Kimara King'ong'o jijini Dar es salaam leo.
Askofu wa Kanisa la Anglikana Dayosisi ya Dar es salaam, Jackson Sosthenes akiongoza Ibada ya Mazishi.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma (wa kwanza kushoto) akifuatiwa na Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt. Eliezer Feleshi wakiwa kwenye Mazishi ya marehemu Jaji Mkuu Mstaafu wa Tanzania Mhe. Augustino Ramadhani.
Ibada ya Mazishi ikiendelea katika Kanisa la Anglikana la Mt. Albano jijini Dar es salaam .
Waziri wa Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Afrika Mashariki Mhe. Prof. Palamagamba Kabudi (wa kwanza kulia) akiwa kwenye Ibada ya Mazishi katika Kanisa la Anglikana la Mt. Albano jijini Dar es salaam .
Waheshimiwa Majaji wa Mahakama ya Rufani waliohudhuria Ibada ya Mazishi katika Kanisa la Anglikana la Mt. Albano jijini Dar es salaam .
Mke wa Marehemu Lt. Col. Mstaafu Saada Mbarouk Ramadhani pamoja na watoto wake wakiweka mchanga kwenye kaburi la Mpendwa wao wakati wa mazishi yaliyofanyika kwenye Makaburi ya Familia Kimara King'ong'o jijini Dar es salaam leo.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akiweka mchanga kwenye kaburi la Jaji Augustino Ramadhani wakati wa mazishi yaliyofanyika kwenye Makaburi ya Familia Kimara King'ong'o jijini Dar es salaam leo.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru akiweka Shada la maua kwenye kaburi la Jaji Augustino Ramadhani baada ya mazishi.
Wanajeshi wa Jeshi la Wananchi wa Tanzania (JWTZ) wakitoa heshima zao kwa mujibu wa taratibu za kijeshi baada ya mazishi. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni