Na
Lydia Churi-Mahakama
Mahakama
ya Tanzania imeanza ujenzi wa majengo sita ya vituo Jumuishi vya utoaji haki katika
mikoa mitano nchini ikiwa ni hatua ya Mhimili huo ya kusogeza huduma karibu
zaidi na wananchi.
Mkuu
wa Kitengo cha Kusimamia Maboresho ya Mahakama (JDU) Mhe. Zahra Maruma amesema
majengo hayo yameanza kujengwa kuanzia mwezi Januari mwaka huu na yanatarajiwa
kukamilika katika kipindi cha miezi 10.
Alisema
majengo hayo yatakuwa na sakafu nne yaani gorofa 3 na yatajumuisha ngazi zote
za Mahakama kuanzia Mahakama Kuu mpaka Mahakama ya Mwanzo pamoja na ofisi za baadhi
ya wadau wa Mahakama wakiwemo Polisi, Ustawi wa Jamii, Mawakili na Waendesha
Mashitaka.
Kwa
mujibu wa Mkuu wa Kitengo cha Kusimamia Maboresho ya Mahakama, majengo hayo
yameanza kujengwa katika miji ya Arusha, Mwanza, Dodoma, Morogoro na Dar es Salaam
katika wilaya za Kinondoni pamoja na Temeke.
Kusudi
la kuweka ngazi zote za Mahakama ndani ya jengo moja pamoja na ofisi za wadau
ni kurahisisha na kuongeza ufanisi wa utoaji wa huduma za utoaji haki pamoja na kumpunguzia mwananchi gharama za kufuatilia huduma hizo katika ofisi
tofauti ambapo humlazimu mwananchi kutumia rasilimali fedha na rasilimali muda
katika kufuatilia huduma hizo.
Upatikanaji wa huduma shirikishi katika
majengo haya utampatia mwananchi fursa ya kutumia muda mchache wa kupata huduma
na kumuongezea muda wa kujishughulisha katika shughuli za uzalishaji na kijamii
badala ya kutumia muda huo kuzunguka katika ofisi tofauti kupata huduma za
haki.
Majengo
haya yanajengwa na
Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na Benki ya Dunia kupitia mradi wa
Maboresho ya Huduma za utoaji haki wa kipindi cha miaka mitano (Citizen -
Centric Judicial Modernisation of Justice Service Delivery).
Lengo la
Mahakama ya Tanzania ni kuhakikisha kunakuwepo na Mahakama Kuu katika kila
mkoa, Mahakama za Hakimu Mkazi katika kila Mkoa, Mahakama za Wilaya kwenye kila
Wilaya na Mahakama za Mwanzo kwenye kila Tarafa kulingana na upatikanaji wa
rasilimali fedha.
Mahakama
ya Tanzania imeanza ujenzi wa majengo sita ya vituo Jumuishi vya utoaji haki katika
mikoa mitano nchini ili kusogeza huduma karibu zaidi na wananchi. Pichani ni
jengo lililoanza kujengwa katika wilaya ya Kinondoni jijini Dar es salaam.
Ujenzi wa jengo la kituo Jumuishi cha utoaji haki lililoanza kujengwa jijini Mwanza.
Ujenzi wa jengo la kituo Jumuishi cha utoaji haki unavyoendelea jijini Arusha
Ujenzi wa jengo la kituo Jumuishi cha utoaji haki unavyoendelea mkoani Morogoro
Ujenzi wa jengo la kituo Jumuishi cha utoaji haki unavyoendelea jijini Dodoma.
Ujenzi wa jengo la kituo Jumuishi cha utoaji haki lililoanza kujengwa jijini Dar es salaam katika wilaya ya Temeke.
Kazi nzuri sana. Hongera sana Mahakama ya Tanzania kwa maboresho.
JibuFuta