Na Magreth Kinabo- Mahakama
Mahakama ya Tanzania imesikiliza jumla ya mashauri 1,519 kupitia Mahakama
Mtandao (Video Conferencing) kati ya Machi 23 hadi Aprili 21mwaka huu ikiwa ni
utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania alilolitoa Machi 23 mwaka huu.
Akizungumza na Waandishi wa habari Machi 23, 2020 jijini Mwanza, Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma aliitaka Mahakama kuongeza kasi ya matumizi ya Teknolojia
ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ikiwa ni hatua ya kupambana na ugonjwa wa COVID 19
unaosababishwa na virusi vya Corona.
Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano wa Mahakama ya Tanzania (TEHAMA), Bw. Machumu Essaba
amesema Mashauri hayo yamesikilizwa katika Mahakama za Hakimu Mkazi za Kisutu na Kinondoni pamoja na Mahakama za wilaya za Ilala, Temeke na Kigamboni jijini Dar es Salaam.
Akitaja idadi ya mashauri yaliyosikilizwa na Mahakama hizo, Bw. Essaba
alisema Mahakama ya Hakimu Mkazi Kisutu ilisikiliza na mashauri 424 na Mahakama
ya Hakimu Mkazi Kinondoni ilisikiliza
mashauri 324. Aidha, Mahakama za wilaya za Ilala, Temeke na Kigamboni
zilisikiliza mashauri kama ifuatavyo;
Ilala mashauri 465, Temeke 230. Mashauri hayo yalisikilizwa kutoka magereza ya
Keko na Segerea.
Katika hatua nyingine, Essaba
alisema Mahakama imeanza kutumia
teknolojia maalumu inayomuwezesha Jaji kusikiliza kesi akiwa ofisini bila ya kufika katika chumba cha Mahakama ya
wazi au cha chenye vifaa vya Mahakama Mtandao ‘Video Conference’.
Alisema teknolojia hiyo imeanza kutumiwa na Mahakama ya Tanzania ikiwa ni njia mojawapo ya kuepuka kuenea kwa maambukizi ya Virusi vya
Corona.
‘‘Teknolojia hii inamwezesha Jaji
kusikiliza kesi akiwa ofisini huku
mhusika wa kesi akiwa katika chumba maalumu.
‘‘Utaratibu huu hauruhusu watu wengine kuwa katika vyumba hivyo, isipokuwa
wahusika wa kesi, ambao ni Jaji na mleta maombi,’’alisema Essaba. Aliongeza kuwa teknolojia hiyo inamuwezesha Jaji kutumia kompyuta mpakato.
Mahakama imeanza kutumia teknolojia hiyo Aprili 21, mwaka huu katika
Mahakama ya Rufani Tanzania, ambapo Jaji wa Mahakama hiyo, Mhe. Dkt. Gerald
Ndika alisikiliza kesi, akiwa ofisini kwake jijini Dar es salaam huku mleta
maombi akiwa Mahakama Kuu Kanda Mwanza. Hivyo teknolojia hiyo itakuwa inaendelea
kutumiwa na Mahakama.
Uongozi wa Mahakama katika kuunga
mkono juhudi za Serikali kukabiliana na
virusi vya Corona tayari imekabidhi
vifaa vya TEHAMA kwa Maafisa
TEHAMA wa kanda 16 za Mahakama Kuu
Aprili 21, mwaka huu ili kuziwezesha Mahakama nyingine kuanza
kusikiliza kesi kwa njia ya
Mahakama Mtandao.
Jaji wa
Mahakama ya Rufani Tanzania, Mhe. Dkt. Gerald Ndika akiendesha shauri kwa kutumia teknolojia maalumu bila ya kufika chumba cha mahakama ya wazi au Mahakama Mtanado Video Conference'.
|
Vifaa vya TEHAMA vikipakiwa kwenye gari kwa ajili ya kusambazwa katika kanda mbalimbali za Mahakama .
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni