Na Magreth Kinabo na Innocent Kansha- Mahakama
Watumishi wa Mahakama ya Tanzania na Mawakili wamehimizwa kuwa mstari wa
mbele katika matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kupunguza
msongamano wa watu mahakamani, kuepuka maambukizi ya virusi vya Corona na
kuokoa gharama za utoaji haki.
Akizungumza leo ofisini kwake, Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania,
Mhe.Wilbert Chuma alisema matumizi ya
TEHAMA kwa watumishi na Mawakili yawe ni
sehemu ya utendaji kazi wao wa kila siku ili kuendesha mashauri pasipokuwa na
ulazima wa wananchi kufika mahakamani na hivyo kupunguza msongamano usio wa
lazima.
‘‘Mashauri yote ya madai yanayohusisha
mawakili yafunguliwe kwa njia ya mtandao na si vinginevyo,’’ alisema Msajili
Mkuu.
Kanuni za ufunguaji wa mashauri kwa njia ya mtandao (Electronic Filling Rules,
2018 GN 148/2018) iliyotolewa na Jaji Mkuu na kuanza kutumika Aprili 13, mwaka
2018 inasisitiza mashauri kufunguliwa kwa njia ya mtandao.
Alisema hivi sasa kuna Mawakili 1,732 waliojisajili katika mfumo wa kufungua
mashauri kwa njia ya mtandao, lakini wanaoutumia ni 1,250. Hivyo alitoa wito
kwa Mawakili hao, wakiwa kama Maofisa wa Mahakama kuona umuhimu wa kutumia
mfumo huo hasa katika kipindi hiki cha kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona.
Kuhusu masuala ya utoaji wa elimu ya matumizi ya njia hiyo, Msajili Mkuu alisema Maafisa TEHAMA wa Mahakama kwa
kushirikiana na Maafisa wengine wa Mahakama wanapaswa kutoa elimu kwa wananchi
wa kawaida juu ya mfumo huo.
Mhe. Chuma alisema viongozi wa kila
ngazi ya Mahakama kuanzia Mahakama ya Rufani hadi Mahakama ya Wilaya wanapaswa kuhakikisha kuna
kioski au sehemu maalumu yenye vifaa
vyote muhimu kwa ajili ya kusajili mashauri kimtandao ili kuwasaidia wananchi wasioweza
kumudu kutumia huduma hiyo hususani wale wasio na uwakilishi.
Aliongeza kuwa Maafisa TEHAMA wahakikishe kwamba wanatoa msaada
unaohitajika wakati wote katika maeneo hayo ili kufanikisha zoezi hilo, ikiwa
ni pamoja na kuwapa haki wale wote wanaopaswa kupewa kwa mujibu wa
taratibu.
‘‘Ni jukumu la kila Mtendaji wa Mahakama katika eneo lake kuhakikisha
mahitaji muhimu yanapatikana ili kufanikisha zoezi hili, ’’alisisitiza.
Msajili Mkuu huyo aliwataka
watendaji kushirikiana na maafisa TEHAMA katika maeneo yao kuhakikisha Majaji
na Mahakimu wote wanatengenezewa sahihi za kielektroniki ndani ya siku 21
kupitia maagizo aliyoyatoa Aprili 14,
mwaka huu.
Mhe. Chuma aliwataka viongozi wa Mahakama
kudhibiti idadi ya waandishi wa habari wanaoingia maeneo ya Mahakama na
kutoruhusu midahalo au mahojiano yoyote ya waandishi wa habari maeneo ya
viwanja vya Mahakama kuanzia sasa ili kupunguza msongamano.
Kwa upande wa uendeshaji mashauri kwa njia ya Mahakama Mtandao (Video
Conference), alisema tayari taratibu za manunuzi zimeshafanyika ili kuwezesha upatikanaji
wa vifaa hivyo kwa Mahakama ambazo hazina. Alisema televisheni za ukutani 13 zitapelekwa katika
magereza mbalimbali na saba (7) zitapelekwa kwenye vituo vya Mahakama Kuu. Aidha kompyuta
mpakato 24 na scanner zitakazogawiwa kwenye maeneo hayo.
Machi 23, mwaka huu, Jaji Mkuu wa Tanzania, katika taarifa yake aliyoitoa kwa
Umma kupitia mkutano wake na waandishi wa uliofanyika Jijini Mwanza, aliwataka viongozi wote wa Mahakama katika ngazi zote kuonyesha uongozi kwa
kuwasaidia Watanzania ili waendelee kupata huduma za utoaji haki kipindi ambacho dunia inapata msukosuko mkubwa wa ugonjwa wa COVID 19 unaosababishwa virusi vya Corona.
Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Mhe. Wilbert Chuma akizungumzia umuhimu wa matumizi ya mfumo wa kusajili mashauri kwa njia mtandao.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni