Na
Magreth Kinabo- Mahakama
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amewataka Mahakimu kuwa na utayari wa kuanza kusikiliza mashauri
yanayohusu ardhi ili kutatua changamoto na malalamiko yaliyojitokeza kwenye
eneo hilo kupitia Mabaraza ya Ardhi hali iliyosababisha suala hilo kwenda Serikalini.
Akizungumza leo mara
baada ya kumuapisha Hakimu Mkazi, Mhe.
Olivia Towilo ofisini kwake, iliyopo Mahakama ya Rufani Tanzania, Jijini Dar es
Salaam. Jaji Mkuu alisema Mahakama imekuwa ikifanya vizuri ndio maana Serikali
imeona ikabidhi jukumu hilo katika mhimili huo.
“Kuanzia mwaka wa fedha
ujao yaani 2020/2021 Mahakama itaanza kusikiliza mashauri ya ardhi, Hivyo
tumeongezewa mzigo Mahakimu watapewa mashauri. eneo hili lina mashauri mengi,
changamoto na malalamiko.
“Mimi naona Mahakimu
ninyi muwe mstari wa mbele kuhakikisha kwamba changamoto na malalamiko
yaliyojitokeza kupitia Mabaraza ya Ardhi hali iliyosababisha suala hili kwenda
Serikalini yanatatuliwa,’’ alisema Jaji Mkuu.
Jaji Mkuu aliongeza
kwamba anatarajia Mahakama itafanya kazi hiyo kwa ubora na kutenda hakin na
kutoa kwa wakati, kutatua migogoro, ikiwemo kutorudia makosa yaliyojitokeza
hapo awali.
Aidha Prof. Juma aliwataka
mahakimu hao, kuwa mstari wa mbele wa utoaji wa haki kwa kuwa hivi sasa kutokana na janga la
ugonjwa wa homa ya mapafu (COVID 19) unaosababishwa na virusi vya Corona
utendaji kazi wa Mahakama umebadilika kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA).
“Mahakimu sasa wako
mstari wa mbele katika mapambano hayo
wanapofanya kazi ya hutoaji haki, hivyo
wanachangamoto ya kuangalia afya zao na
watu wanaofika mahakamani ili kuepusha kuenea kwa virusi vya Corona,’’
alisisitiza huku akisema kazi ya uhakimu ni muhimu kwa kuwa asilimia 80 ya
mashauri yote yanayosajiliwa na yanasikilizwa katika Mahakama za Mahakimu.
Pia alifafanua kuwa unapozungumzia
haki kwa mwananchi wa kawaida anatambua kuwa ni Hakimu,ambapo aliwataka
Mahakimu hao kutoa haki kulingana na
viapo vyao.
Aliongeza kuwa Mahakimu
wanapaswa kujutumia elimu waliyonayo kujiendeleza kutafuta taarifa mbalimbali
bila hata ya kupata cheti kwani katika karne ya 21 ya ushindani na TEHAMA,
hivyo wanatakiwa kuwa weledi katika suala hilo, uandishi na lugha ili hukumu
zao ziwe zinasomeka na kueleweka.
Hakimu huyo
aliyeapishwa ametokea katika Mahakama ya Mwanzo Arusha Mjini (Maromboso).
( Picha na Magreth
Kinabo- Mahakama)
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akimuapisha Hakimu Mkazi, Mhe. Olivia Towilo leo
ofisini kwake, iliyopo Mahakama ya Rufani Tanzania, Jijini Dar es Salaam.
|
Jaji Mkuu wa Tanzania,
Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma akizungumza mara baada ya kumuapisha Hakimu
Mkazi, Mhe. Olivia Towilo leo ofisini kwake, iliyopo Mahakama ya Rufani
Tanzania, Jijini Dar es Salaam.
Msajili Mkuu wa
Mahakama ya Tanzania, Mhe. Wilbert Chuma (wa kwanza kulia) akizungumza jambo
kabla ya uapisho huo.
|
Hakimu huyo akitia saini kiapo chake. |
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni