Na Emmanuel Oguda –Mahakama Kuu, Shinyanga
Mahakama Kuu ya
Tanzania Kanda ya Shinyanga, leo tarehe 15/5/2020 imetoa maamuzi madogo ya
maombi ya dhamana ya Mbunge wa Kishapu Mhe. Seleman Masoud Seleman,
maarufu kwa jina la Nchambi na Mkewe Aisha Soud. Maombi hayo yalisikilizwa na kusomwa maamuzi yake
kwa njia ya Mahakama Mtandao (video conference).
Maamuzi hayo yamesomwa
kwa njia hiyo na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe.
Cyprian Mkeha ambaye ametoa dhamana kwa waombaji hao kwa masharti matatu, yakiwa ni kusaini hati
ya dhamana ya shilingi milioni 50 kwa kila mtuhumiwa na kuwa na mdhamini mmoja
atayekusaini dhamana ya milioni 10 kwa kila mmoja. Sharti la tatu ni wote
wawili kukabidhi polisi hati zao za kusafiria na kutoruhusiwa kusafiri nje ya
nchi.
Masharti hayo ya
dhamana yatathibitishwa na Mahakama ya Wilaya Shinyanga mbele ya Hakimu aliyewasomea
mashitaka. Hata hivyo Mbunge huyo alirudi gerezani na taratibu za dhamana zitaendelea.
Maombi haya ya dhamana
yalifunguliwa mahakamani hapo baada ya Mahakama ya Wilaya Shinyanga ambako
washitakiwa walisomewa mashitaka hapo awali yanayowakabili kuamua kuwa haina
mamlaka kisheria ya kuwapa dhamana watuhumiwa wanaotuhumiwa kwa makosa ya
uhujumu uchumi ambayo thamani yake haikutajwa kwenye hati ya mashitaka.
Mbunge huyo na Mkewe
walishitakiwa katika Mahakama ya Wilaya Shinyanga mnamo Mei 8, mwaka huu wakikabiliwa na mashitaka 12
ya Uhujumu Uchumi, ikiwemo kumiliki silaha za moto kinyume na sheria za nchi.
Mahakama Kuu Shinyanga
ilisikiliza shauri hilo kwa njia hiyo kufuatia uzinduzi wa mfumo wa kidijitali
wa kusikiliza mashauri bila wahusika kufika mahakamani moja kwa moja. Uzinduzi huo uliofanyika Mei 13, mwaka huu katika ukumbi wa Mahakama Kuu
Shinyanga.
Aidha katika uzinduzi huo, usikilizwaji
wa mashauri mengine mawili ulifanyika kwa njia ya hiyo, ambayo yalihusu
maombi namba 34/2019 la mfungwa Juma
Masunga dhidi ya Jamhuri kuomba kuongezewa muda wa kukata rufaa na shauri
la rufaa namba 9/2020 la mfungwa Kulwa
Ndaki dhidi ya Jamhuri yaliyosikilizwa na Jaji Mfawidhi wa Mahakama
hiyo, Mhe. Gerson Mdemu.
Wafungwa hao, walifuatilia usikilizwaji wa
mashauri hayo kwa njia ya hiyo wakiwa
gereza la Mhumbu Wilaya ya Shinyanga, huku Waendesha Mashitaka wa Serikali
Pamoja na Mawakili wa kujitegemea wakiwa katika ukumbi wa mahakama na Majaji wakiwa kwenye chemba zao.
Wakati huo huo, Festor Sanga, anaripoti kuwa Kaimu Jaji
Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe.
Athumani Kirati amewataka
waandishi wa habari kusaidia kuuhabarisha Umma juu ya Usikilzaji wa
Mashauri kwa njia ya Video Conference na Usajili wa Mashauri kwa njia ya
mtandao (Electronic filling) ili kuweza kuondokana na msongomano usiokuwa wa
lazima katika kipindi hiki changamoto ya ugonjwa huo.
‘‘Tumewezeshwa vifaa
ambavyo vimefungwa katika Gereza la Bangwe na Mahakama Kuu vinavyowezesha
usikilizaji wa mashauri kwa njia ya Video’’ alisema Jaji Kirati.
Kwa upande wake Naibu
Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Arnold Kirekiano alieleza kwamba
tangu kuanza kwa mfumo huo Mahakama Kuu Kigoma, Mahakama ya Hakimu Mkazi na
Mahakama za Wilaya Kibondo na Kigoma wameanza kutumia mfumo huo. Hivyo kwa wiki
hii mashauri mawili yalisikilizwa Mahakama Kuu ambapo mawakili walikuwa Dar es
salaam, Kigoma na Tabora.
Hatua hiyo imekuja
wakati Mahakama ya Tanzania ikiendelea kuimarisha matumizi ya mifumo ya kisasa
ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA), katika kusikiliza na usimamizi
wa mashauri. Mfumo huu Pamoja na faida nyinginezo unasaidia kupunguza msongamano
wa watu wanaofika kupata huduma mahakamani katika kipindi hiki cha
kukabiliana na kuenea kwa virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa
wa homa kali ya mapafu (COVID – 19).
Jaji Mfawidhi wa Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Shinyanga, Mhe. Gerson Mdemu akizindua usikilizaji wa
mashauri kwa njia ya mtandao Mei 13, mwaka huu.
Baadhi ya waandishi wa habari wakipata maelezo kutoka kwa Kaimu Jaji Mfawidhi wa Mahakama Kuu Kanda ya Kigoma Mhe. Jaji Athumani Kirati.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni