Jumanne, 12 Mei 2020

MAHAKAMA KUU SONGEA YAANZA KUSIKILIZA MASHAURI KWA MTANDAO


Na Brian Haule –Mahakama Kuu Songea



Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea imeanza kusikiliza mashauri na kutoa hukumu kwa Mahakama Mtandao yaani ‘Video Conference’.

Mahakama hiyo imeanza kusikiliza mashauri kwa njia hiyo, baada ya jitihada za Mahakama ya Tanzania kununua vifaa maalumu vya  kuendesha mahakama kwa mtandao  kwa ajili ya mahakama mbalimbali nchini, ikiwa ni  hatua  za kuepuka kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha  ugonjwa wa  (COVID 19) sambamba na mabadiliko ya teknolojia. 

Mahakama  hiyo imeanza kusikiliza shauri la jinai namba 4 la mwaka 2020  kwa njia hiyo  Mei 11, mwaka huu lililoendeshwa na Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea, Mhe.Isaya Arufani, linalohusu Jamhuri ambayo iliwakilishwa na Wakili wa Serikali Amina Mawoko dhidi ya  mshtakiwa Bakari Omari, ambaye aliwakilishwa na Wakili   wa utetezi Makame Sengo.

Katika shauri hilo kwa mara ya kwanza Mahakama hiyo imelisikiliza bila    ya          mshtakiwa kwenda Mahakama Kuu Kanda ya Songea kwa kuwa   mshtakiwa alikuwa katika Gereza la Wilaya ya Songea. Shauri hilo lilisikilizwa huku Jaji, Mawakili na wasaidizi wa kumbukumbu wakiwa katika ukumbi wa Mahakama hiyo.

Wakili wa Mawoko alidai kuwa mshtakiwa huyo alitenda kosa la mauaji ya ndugu yake Omari Mohamedi Omari katika Kijiji cha Mbise Wilaya ya Tunduru mkoani Ruvuma Aprili 20, mwaka 2019, ambapo alimfuata ndugu yake (marehemu) nyumbani kwake na kumkuta anaongea na simu akamuuliza, kwa nini  amewatukana watoto zake, lakini  marehemu  alikataa kuwa hakuwatukana. Ndipo mshtakiwa  alikasirika  na kuanza kumshambulia kwa ubapa wa upanga.

Baada ya kumaliza kumshambulia baadaye watoto wawili wa mshtakiwa walirudi nyumbani kwa marehemu na kuanza kumpiga tena marehemu kwa sababu alipigana na baba yao.

Mahakama hiyo ilimtia hatiani mshtakiwa huyo baada ya kukiri kosa lake. Hivyo iliamuru afungwe kifungo cha nje kwa muda wa mwaka mmoja na kutotakiwa kufanya kosa lolote katika kipindi hicho. Watoto wa mshtakiwa huyo bado wanatafutwa. 

Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Songea ikiendesha shauri kwa njia ya mtandao.







Hakuna maoni:

Chapisha Maoni