Ijumaa, 8 Mei 2020

MAJAJI 125 WAJADILI UZOEFU WA UTOAJI HAKI KWA MTANDAO

Na Magreth Kinabo-Mahakama

Majaji 125 kutoka katika mabara manne duniani wamefanya mkutano kwa njia ya mtandao kujadili jinsi ya kuendelea na shughuli za utoaji haki kwa kutumia Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuepuka kuenea kwa maambukizi ya virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa homa ya mapafu (COVID 19).

Mkutano huo uliandaliwa na Shirika la Miliki Bunifu Duniani (WIPO) ambalo liko  chini ya Umoja wa Mataifa (UN), uliofanyika Makao Makuu ya shirika hilo Geneva, kwa njia ya mtandao hivi karibuni. Lengo la mkutano huo wa siku moja lilikuwa ni kubadilishana uzoefu jinsi gani Mahakama zinaweza kuendelea na huduma za utoaji haki katika kipindi cha janga la Corona.

Akizungumza kuhusu mkutano huo, Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe. Stephen Magoiga alisema mkutano huo ulishirikisha Majaji kutoka Bara la Afrika, Ulaya, Marekani na Asia. Katika mkutano huo, Tanzania iliwakilishwa na yeye pamoja na Mwakilishi wa WIPO kutoka Mahakama ya Tanzania, ambaye ni Hakimu Mkazi na Msaidizi wa Msajili Mkuu, Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri.

Jaji Magoiga alifafanua kwamba miongoni mwa waliyopendekeza katika mkutano huo, ni Majaji kuwezeshwe kuwa  na huduma ya mtandao (internet) nyumbani  na sio ofisini tu ili waweze kuendelea na huduma ya utoaji haki hususan kipindi cha ugonjwa wa homa ya mapafu, ikiwemo kuenda sambamba na mabadiliko ya teknolojia.

 “Suala la mabadiliko ya TEHAMA) ni muhimu ili tuendane na   mabadiliko ya teknolojia. Hivyo Majaji wasiwe na huduma ya mtandao maofisini tu bali hata kwenye nyumba zao ili waweze kuendelea na huduma za utoaji haki hasa katika kipindi hiki cha janga la Corona hata wakiwa nyumbani kwa kuwa wakati mwingine hawawezi kumaliza kazi ofisini, pia itawawezesha kufanya tafiti mbalimbali,” alisema Jaji Magoiga. 

Jaji Magoiga  alisema  kupitia mkutano huo, wamejifunza kuwa Majaji wa Uingereza  mazingira yao yanawaruhusu kufanya kazi hata  wakiwa nyumbani kwa mujibu wa Jaji wa  Mahakama Kuu ya Uingereza, Mhe. Collins Birss.

Aliongeza kwamba matumizi ya TEHAMA pia yanasaidia kulinda usalama wa watumishi katika kipindi hicho na kutoa huduma kwa gharama nafuu.

Kwa upande wake Mhe. Ngitiri alisema  katika mkutano huo, wamejifunza kwamba huduma za utoaji haki zinaweza kuendelea kutolewa  kwa njia ya  mawasiliano ya simu kwa nchi ambazo zimewekewa zuio la kutotoka nje ikiwa ni hatua za kukabiliana na virusi vya Corona, kupitia  Jaji wa   Mahakama ya Rufani ya Marekani, Mhe. Cathleen O’ Malley.

Aidha Ngitiri alitoa uzoefu wa Mahakama ya Tanzania katika kipindi hiki, akisema imechukua hatua stahiki, shughuli za Mahakama zinaendelea kufuatia agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma kusisitiza   matumizi ya TEHAMA kwenye suala la ufunguaji mashauri kwa njia ya kielektroniki na Mahakama Mtandao ‘Video Conference’ itumike kusikiliza.

Katika mkutano huo walijadili matumizi ya kamera mahakamani kuwa yanaweza kufanyika kwa kurekebisha  baadhi ya kanuni.

WIPO ilifanya mkutano wa siku 7 hapa nchini Tanzania mwaka jana katika Hoteli ya Hyatt Regency jijini Dar es Salaam ulioshirikisha washiriki 35 kutoka nchi za Sweden, Switzerland, Nepal, Cambodia, Rwanda, Uganda, Mozambique, Zambia, Malawi, Burtan, Ethiopia n.k.

Aidha Mahakama ya Tanzania kwa kushirikiana na WIPO kwa mara ya kwanza iliwapatia Mafunzo ya Haki Miliki jumla ya Mahakimu 30 yaliyolenga kuwawezesha kuandika hukumu bora zaidi kwa mashauri yanayohusiana na haki miliki.
Jaji wa Mahakama Kuu ya Tanzania Divisheni ya Biashara, Mhe. Stephen Magoiga akizungumzia mkutano huo uliofanyika kwa njia ya mtandao.
Mwakilishi wa WIPO kutoka Mahakama ya Tanzania, ambaye ni Hakimu Mkazi na Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri akihudhuria mkutano huo kwa njia ya mtandao.
Baadhi ya Majaji wakiwa katika mafunzo ya WIPO yaliyofanyika Geneva mwaka jana. Kulia ni  Mwakilishi wa WIPO kutoka Mahakama ya Tanzania, Hakimu Mkazi ambaye pia ni Katibu wa Msajili Mkuu wa Mahakama ya Tanzania, Mhe. Upendo Ngitiri (Picha kutoka Maktaba).

                                






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni