Na Magreth Kinabo –Mahakama
Mahakama ya Tanzania imefanikiwa
kuendesha mashauri 4,711 kwa njia ya Mahakama Mtandao maarufu kama ‘Video
Conference’ ikiwa ni hatua mojawapo za
kujikinga na maambukizi ya Virusi vya Corona vinavyosababisha ugonjwa wa COVID
19 katika kipindi cha miezi miwili.
Mashauri hayo yamesikilizwa kwa njia hiyo, kufuatia
utekelezaji wa agizo la Jaji Mkuu wa Tanzania, Prof. Ibrahim Hamis Juma alilolitoa Machi 23, mwaka huu la kutumia
Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) ili kuwaepusha Watumishi wa
Mahakama, Magereza, wafungwa na mahabusu na wateja wengine wa Mahakama dhidi ya
maambukizo hayo, wakati shughuli za utoaji haki zikiendelea kufanyika.
Agizo hilo lilitolewa na Prof. Juma kupitia mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Jijini Mwanza, la kuongeza matumizi ya TEHAMA kwenye kipindi hichi ambacho Tanzania na dunia kwa ujumla kukumbwa na janga la ugonjwa huo.
Agizo hilo lilitolewa na Prof. Juma kupitia mkutano wake na waandishi wa habari uliofanyika Jijini Mwanza, la kuongeza matumizi ya TEHAMA kwenye kipindi hichi ambacho Tanzania na dunia kwa ujumla kukumbwa na janga la ugonjwa huo.
Akizungumzia kuhusu usikilizaji wa
mashauri kwa kutumia teknolojia hiyo, Mkurugenzi Msaidizi wa Teknolojia ya
Habari na Mawasiliano (TEHAMA), Bw. Machumu Essaba alisema imelipunguzia pia Jeshi
la Magereza gharama za usafiri wa kila
siku za kuwaleta wafungwa au mahabusu mahakamani na msongamano.
‘‘Njia hii imetumika katika kipindi
cha ugonjwa huu, kuanzia Machi 23, mwaka huu hadi Mei 26, mwaka huu, ambapo Mahakama ya
Rufani Tanzania, imesikiliza mashauri 48 kupitia vikao vitano, kati ya hivyo
vitatu vilifanyika katika Jiji la Dar es Salaam, vilivyohusisha mashauri 30 na
kimoja Tabora kilichohusisha mashauri tisa na kingine Iringa kilichokuwa na
mashauri tisa,’’ alisema Essaba.
Alisema kuwa Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya Dar es Salaam imesikiliza mashauri
3,188 kati ya hayo, mashauri 804 ymesikilizwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi
Kisutu, Mahakama za Wilaya, Kinondoni 714, Ilala 992, Temeke 523, na Kigamboni 155.
Mahakama Kuu ya Tanzania Kanda ya
Mbeya, Mahakama ya Mkoa na Wilaya mashauri yaliyosikilizwa kwa teknolojia hiyo ni
367, kanda zingine ni Tanga 310, Musoma 158, Tabora 130,
Dodoma 78, Mtwara 66, Moshi 46, Arusha 41, Kigoma, 37, Sumbawanga 23, Iringa 15, Songea 14, Shinyanga 12, Mwanza 28
na Bukoba 5.
Essaba alifafanua kwamba Mahakama Kuu Divisheni za
Biashara imesikiliza mashauri 55 na Kazi mashauri 90, ambazo zilitumia vifaa
vilivyopo kwenye maeneo yao.
Aidha aliongeza kwamba zaidi mashauri 300 yamesikilizwa na Mahakama
Kuu ya Tanzania Kanda ya Mwanza kwa kutumia simu ya mezani ‘Teleconference’ kwa
sababu kuna tatizo la ukosefu wa huduma ya
mtandao ‘internet’ kwenye ofisi za Mwanasheria wa Serikali, hali inayosababisha kutumia njia
hiyo.
Uongozi wa Mahakama katika kuunga mkono juhudi za Serikali za kukabiliana na Virusi vya Corona ulikabidhi vifaa vya TEHAMA kwa Maafisa TEHAMA wa kanda 16 za Mahakama Kuu yaTanzania Aprili 16 mwaka huu ili kuziwezesha Mahakama nyingine kusikiliza mashauri kwa teknolojia hiyo,
Awali teknolijia hiyo ilikuwa
inatumika katika vituo sita, ambavyo ni mfumo huo, umefungwa ambavyo ni Mahakama Kuu ya Tanzania katika Kanda za Dar
es salaam, Mbeya, na Bukoba pamoja na Kituo cha Habari Mafunzo cha Kisutu, Gereza la
Keko na Chuo cha Uongozi wa Mahakama (IJA), Lushoto.
Moja ya Shauri likiendeshwa kwa njia ya Mahakama Mtandao.
(Picha na Maktaba ya Mahakama ya Tanzania)
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni