Na Magreth Kinabo
Msajili wa Mahakama Kuu ya Tanzania, Mhe. Sharmillah
Sarwatt amewataka wadau mbalimbali wanaohusika na mashauri na haki za watoto
kushirikiana ili kutatua changamoto zilizopo katika mahabusu na baadhi ya Magereza kwa lengo la hakikisha mtoto
anapewa haki kwa wakati na kwenye mazingira bora, ikiwemo kulindwa.
Mhe. Sarwatt amezungumza hayo leo wakati akifungua kikao kazi cha
wadau wa Mahakama kilichofanyika baada ya ukaguzi wa mahabusu za watoto na baadhi ya
magereza uliofanyika kati ya Machi 16 na 25, mwaka huu.
Alisema moja ya jukumu la Mahakama Kuu Masjala Kuu
ni kukagua Mahakama zote za chini, magereza na mahabusu za watoto nchini ili
kuboresha huduma za Mahakama kwa kuhakikisha haki inapatikana kwa wote na kwa
wakati.
Msajili huyo alisema kila mdau ana wajibu wa
kuhakikisha anafanikisha upatikanaji wa haki ya mtoto kwa wakati, ikiwemo kutafuta suluhisho la
changamoto zilizojitokeza katika ukaguzi huo kwa haraka.
“Miongoni
mwa changamoto iliyojitokeza katika ukaguzi huu ni pamoja na baadhi ya watoto kukutwa kwenye gereza la watu wazima kwa sababu ya kushindwa kutathimini umri wao
wakati wa kuandaa hati zao za mashtaka na hivyo kusomeka ni watu wazima. Katika
suala hili ni jukumu la kila mdau kuweza kuangalia jinsi ya kulitatua,” alisema
Mhe. Sarwatt.
Kwa upande wake, Naibu Msajili wa Mahakama wa Kuu ya Tanzania
Dawati la Watoto, Mhe. Nyigulila Mwaseba alizitaja changamoto nyingine zilizotokana na ukaguzi huo, kuwa ni watoto
waliokinzana na sheria kupigwa wakati wa
kukamatwa hali inayowasababishia baadhi yao kupata ulemavu wa kudumu hasa
katika mkoa wa Dare es Salaam,
kutokuwepo kwa mahabusu za watoto hali inayosababisha watoto kuchanganywa
na watu wazima katika magereza.
Changamoto nyingine ni Maafisa Ustawi wa Jamii kutohusishwa katika
hatua za ukamataji wa watoto ili haki zao za msingi zifuatwe, baadhi ya majengo
ya mahabusu ni chakavu na yana maeneo finyu hivyo kuwanyima watoto uhuru na
nafasi ya kujifunza kwa vitendo,ikiwemo kuwabadilisha tabia, upungufu wa
Maafisa Ustawi wa Jamii, kutokuwepo kwa fungu la kuwahudumia watoto waliokinzana na sheria magerezani( watoto waliopo gerezani baada ya mama zao kutuhumiwa kwa kosa la jinai au kufungwa) na kutokuwepo kwa usafiri katika mahabusu za watoto
na kusababisha kutofikishwa mahakamani kwa wakati.
Akichangia hoja kuhusu kuwepo kwa bajeti au fungu la
kuwahudumia watoto wanaoishi magerezani na mama zao(waliopo gerezani baada ya
mamazao kutuhumiwa na kosa la jinai au kufungwa na kuwarekebisha watoto
waliokinzana na sheria, ikiwemo kuwepo kwa mazingira wezeshi ya kusomea. Mrakibu
Mwandamizi wa Jeshi la Magereza, Amina Kavirondo alisema kuna haja ya kupaza sauti ili taasisi zinazohusika zitenge bajeti kwa ajili hiyo.
Wadau hao, pia walipendekeza kuwepo kwa mikakati ya
kuanzisha mahabusu za watoto waliokinzana na sheria.
Ukaguzi huo ulifanyika baada ya Jaji Kiongozi kuteua
timu ya watu sita, ambayo ilifanya kazi hiyo kwenye mahabusu nne za watoto.zilizopo
mikoa ya Dar es Salaam, Tanga, Moshi, Arusha na Mbeya, Shule ya Maadilisho
iliyopo Irambo – Mbeya na baadhi ya magereza ambayo ni gereza la Maweni,
Karanga, Ruanda, Kisongo, Chumbageni.Jumla vituo 13 na watoto 131 walihusika katika
ukaguzi huo.
Mrakibu Mwandamizi wa
Magereza, Amina Kavirondo akichangia jambo kwenye kikao hicho.
|
Baadhi ya wadau hao
wakiwa katika kikao hicho.
|
Wakili wa Serikali
Mwandamizi kutoka Ofisi ya Taifa ya Mashtaka Dodoma, Beatrice Mpembo akifafanua
jambo.
|
Mrakibu Msaidizi wa
Magereza Justine Kipeta akichangia jambo wakati wa kikao hicho.
|
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni