Jumatatu, 8 Juni 2020

MAHAKAMA ZA MWANZO GEITA ZASIKILIZA MASHAURI NDANI YA MIEZI MINNE


Na Magreth Kinabo na Innocent  Kansha -  Bukombe

Mahakama za Mwanzo katika Mkoa wa Geita zimejipanga kumaliza mashauri ndani ya kipindi cha miezi minne, licha ya utaratibu uliopangwa na Mahakama ya Tanzania wa kumaliza mashauri hayo ndani ya miezi sita. 

Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Mhe.  Ainawe Moshi amesema  kwamba  Mahakama  hizo zimejipangia utaratibu huo  ili kuwawezesha wananchi   kupata fursa ya kutosha ya kuendelea  kushiriki  katika shughuli za  kiuchumi na kijamii.

‘‘Napenda kuwaambia wananchi   na wadau wetu kuwa  Mahakama  ya Tanzania imeboresha miundombinu, hivyo sisi tumejipanga kumaliza mashauri kwa wakati tofauti na zamani  ambapo watu  walikuwa wanafahamu shauri linaweza kukaa  miaka miwili hadi saba mahakamani. Hivi sasa Mahakama inaenda na wakati, hakuna shauri la Mahakama ya Wilaya linalokaa zaidi ya miezi 12, pia kwa Mahakama za Mwanzo tumejipanga kumaliza shauri ndani ya miezi minne,’’ alisema Mhe. Moshi.

Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania, Hakimu Moshi aliwataka wananchi  wasiogope kufikisha mashauri yao mahakamani, bali wafike kwenye eneo hilo na watapata haki zao kwa wakati na bila upendeleo.


Kwa upande wake Afisa Tawala  wa Mahakama ya Wilaya, Bukombe, Bw.Sauwael  Urio alisema  kutokana na maboresho yaliyofanyika hivi sasa wanatoa nakala za hukumu ndani ya siku 21. Hali hiyo imetokana kuwepo kwa mazingira wezeshi ya vitendea kazi na watumishi wa kutosha.

Alisema Mahakama ya wilaya ya Bukombe hupokea wastani wa  mashauri 600 kwa mwaka na kuhudumia takribani  wananchi 200,000  wanaotoka kwenye wilaya hiyo na Wilaya ya Mbogwe. 

 Aliongeza kuwa kutokana na maboresho yaliyofanywa na Mahakama ya Tanzania, uwajibikaji na hamasa ya utendaji kazi  imeongezeka kwa kuwa  hakuna tatizo la upungufu wa watumishi, nafasi ya kufanya kazi  pamoja na vitendea kazi.

Naye Hakimu Mkuu Mfawidhi wa Mahakama ya Mwanzo Ushirombo, Mhe.  Damas  Gakwaya alisema  wanafanikiwa kusikiliza mashauri ngazi za Mahakama hiyo kwa kipindi cha miezi miezi minne kwa  sababu  wanayapokea mashauri tayari yakiwa na ushahidi uliokamilika. Alisema pia wao hutumia utaratibu  wa kuwa karibu na wananchi ili kuwasaidia kuwapa elimu juu ya masuala mbalimbali ya kisheria. Mahakama  hiyo hupokea wastani wa mashauri 800 kwa mwaka. 
    
Kwa upande wake Mtendaji wa Kata ya  Igulwa,  eneo  ilipo Mahakama ya Wilaya ya Bukombe ameishukuru Serikali kwa kuwapatia jengo kubwa na la kisasa la Mahakama ikiwemo Mahakama ya Mwanzo ya Ushirombo, ambapo  kwa sasa kila mtumishi ana chumba chake cha kufanyia kazi hali inayosababisha mashauri kumaliza saa 4.00 asubuhi  na wananchi wanapata muda kuendelea  na shughuli nyingine za uzalishaji.

Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe lilizinduliwa rasmi na Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma Desemba 19 mwaka jana.

Mahakama ya Tanzania kupitia Mpango Mkakati wake wa Miaka Mitano (2015/16 hadi 2019/20), inasisitiza utoaji haki kwa wote na kwa wakati ambapo imejiwekea muda wa kumalizika kwa shauri mahakamani. Katika Mahakama za Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama za wilaya  shauri linatakiwa kumalizika ndani ya miezi 12, Mahakama Kuu ndani ya miaka 2 na Mahakama za Mwanzo ni miezi sita.

 Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Wilaya ya Bukombe, Mhe.  Ainawe Moshi , akizungumzia  maboresho ya Mahakama hiyo.
Jengo la Mahakama ya Wilaya ya Bukombe.





  
  

Hakuna maoni:

Chapisha Maoni