Jumamosi, 13 Juni 2020

HUKUMU 12 ZA UHUJUMU UCHUMI ZATOLEWA SIMIYU KIPINDI CHA MWAKA HUU


Na Innocent kansha na Magreth Kinabo – Mahakama,Simiyu

Jumla ya mashauri 28 ya uhujumu uchumi yamefunguliwa na hukumu 12 zimeshatolewa kutokana na  makosa ya aina hiyo katika Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu pamoja  na Mahakama ya Wilaya ya Bariadi.

Akifafanua chanzo cha makosa hayo kwa Maafisa Habari wa Mahakama  ya Tanzania, ofisini kwake katika  mahojiano maalum, Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu Mhe. Venance  Mlingi alisema yanatokana na wananchi kuingia kwenye Hifadhi za Taifa za  Wanyama  Pori ya  Serengeti na  Pori la akiba la Maswa.

“Mashauri mengine tunayoyapokea ni ya dawa za kulevya ikiwemo, bangi na mirungi pamoja na mashauri ya talaka na mirathi, lakini mashauri tunayoyapokea kwa wingi zaidi ni ya kuingia hifadhini na kukutwa na nyara za Serikali na silaha kama vile, visu, panga na rungu ,’’ alisema Mlingi.

Takwimu  zilizotolewa na  Hakimu  huyo zinaonyesha kuwa Desemba  mwaka 2019, Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Bariadi zilibakiwa na mashauri ya uhujumu uchumu 125 na yalibaki kwa sababu mbalimbali ikiwemo kutokamilika kwa upelelezi na mengine kukosa kibali cha kuyasikiliza kutoka kwa Mkurugenzi wa Mashtaka Nchini (DPP).

Mlingi alifafanua  kwamba   kuanzia Januari mwaka 2020  hadi Juni Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya Wilaya Bariadi zilifanikiwa kusajili mashauri ya uhujumu uchumi yapatayo 28 na kumaliza mashauri 51,na kubakiwa  na mashauri yapatayo 102.

Aliongeza kuwa  kutoka na mashauri ya uhujumu uchumi Mahakama ya Hakimu Mkazi na Mahakama ya  Wilaya ya Bariadi zilifanikiwa  kutoa  hukumu 12 za  vifungo jela kwa watuhumiwa  waliothibitika kutenda makosa hayo visivyopungua  kuanzia miaka 20 hadi 30 jela.

Mlingi  alizungumzia pia hali ya usikilizaji wa mashauri kwa upande wa Mahakama za Mwanzo katika Mkoa wa Simiyu ambapo alisema wamefanikiwa kumaliza mashauri yote ndani ya miezi sita ikiwa ni utekelezaji wa maelekezo ya viongozi wa Mahakama kwa asilimia 100,  licha ya  kujiwekea malengo ya kumaliza mashauri yote ndani ya miezi mitatu kwa kila Hakimu.

Aliongeza kwamba  katika Mahakama hiyo, wanatoa elimu kuhusu masuala ya kisheria yanayohusu mirathi, ndoa na migogoro ya ardhi kwa wananchi ili kuwapa uelewa zaidi wa masuala hayo.

‘‘Ninaomba wananchi wafike  katika Mahakama hii, ili kuweza kapata elimu ya masuala mbalimbali ya kisheria, hili ni jengo lao kwa ajili ya kupata elimu pia, alisisitiza Mhe. Mlingi".

Alisema katika kipindi cha mwaka mmoja, Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu mashauri husajili wastani wa mashauri 120 na Mahakama ya Wilaya ya Bariadi ni m ashauri 660.

Kwa upande  wake  Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa wa Simiyu, Bw. Leonard Maufi alisema uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama umesaidia kwa kiasi kikubwa kupunguza gharama kubwa za ulipaji wa pango kwani ikumbukwe kuwa awali Mahakama ya Mkoa wa Simiyu ilikuwa inatumia jengo la mtu binafsi kuendeshea shughuli zake za utoaji haki.

Alisema kuwepo kwa jengo hilo kutaondoa gharama ya ulipaji kodi katika jengo walilokuwa wamekodi. Aliongeza kuwa kiasi cha shilingi milioni 3 zilizokuwa zikitumika kulipa kodi kila mwezi  sasa fedha  hizo zinaelekezwa kwenye matumizi mengine ya shughuli za Mahakama.

“Kutokana  na maboresho haya, hivi sasa ari  ya watumishi ya utendaji kazi  ipo juu sana na ufanisi wa kazi umeongezeka kwa kiwango kikubwa na kila mtumishi anafanya kazi kwa nafasi, na vitendea kazi vipo vya kutosha,’’, alisema.

Maufi alisema hali hiyo imeongeza ubora  wa utoaji huduma kwa wadau wa Mahakama,  utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za mahakama umeboreka.

Hata hivyo, baadhi ya wateja waliofika mahakamani hapo walisema wameridhika na huduma zinazotolewa na kuishukuru Serikali kwa kujenga jengo hilo.


Hakimu Hakimu Mkazi Mfawidhi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu Mhe. Venance  Mlingi, akizungumzia kuhusu usikilizaji wa mashauri baada ya uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama.

Mtendaji wa Mahakama ya Mkoa wa Simiyu, Bw. Leonard Maufi akielezea jinsi  uboreshaji wa miundombinu ulivyosaidia kuongeza ari utendaji kazi katika huduma za utoaji haki kwenye Mahakama hiyo.

Msaidizi wa Kumbukumbu Mwandamizi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu, Bw. William Mbeke akizungumza kuhusu utunzaji wa nyaraka na kumbukumbu za Mahakama katika Mahakama hiyo.
Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Mahakama ya Wilaya ya Bariadi.

Jengo la Mahakama ya Hakimu Mkazi Simiyu na Mahakama ya Wilaya ya Bariadi.


Sehemu ya kupumzika wananchi  wanaofika mahakamani kupata huduma.





Hakuna maoni:

Chapisha Maoni