Alhamisi, 11 Juni 2020

MASHAURI YA JINAI 554 YAMALIZIKA MKOANI GEITA


Innocent Kansha na Magreth  Kinabo-Mahakama, GEITA

Imeelezwa kuwa Mkoa wa Geita una idadi kubwa ya mashauri ya jinai  yanayofunguliwa katika Mahakama ya Hakimu Mkazi pamoja na Mahakama ya Wilaya ya  Geita kutokana na kuwepo kwa shughuli mbalimbali za kiuchumi kwenye eneo hilo.
  
Akizungumza na Maafisa Habari wa Mahakama ya Tanzania, leo Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama  ya Hakimu Mkazi Geita, Mhe. Obadiah Bwegoge, amesema mashauri ya jinai ndio yanayofunguliwa kwa wingi katika Mahakama hizo, ukilinganisha na mashauri ya madai.

‘‘Kuongezeka kwa makosa ya jinai kunatokana na kuwepo kwa shughuli za uchimbaji, usafirishaji na uuzaji wa madini ya dhahabu bila ya kuwa na leseni. Makosa mengine ni uvamiaji wa Hifadhi ya Taifa ya Rubondo iliyopo Wilaya ya Chato Mkoani Geita, kukutwa na nyara za Serikali pamoja na makosa ya wizi na unyang’anyi,’’ alisema Bwegoge.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa na Mhe. Bwegoge, katika kipindi cha mwaka 2019 jumla ya mashauri ya jinai na madai  yaliyofunguliwa kwenye Mahakama ya Hakimu  Mkazi  Geita na  Mahakama ya Wilaya ya Geita ni 704 ambapo, kati ya hayo mashauri ya jinai yalikuwa ni 321, na madai yalikuwa ni 132. 

Alisema kati ya mashauri yote 680 yaliyosikilizwa na kumalizika, mashauri ya jinai yalikuwa ni 554 huku mashauri ya madai yalikuwa ni 126. Aidha katika kipindi cha Januari hadi Juni 9, mwaka huu, mashauri ya jinai yaliyofunguliwa  kwenye Mahakama hizo yalikuwa ni 321 na madai 48.

Alifafanua kuwa Maboresho ya miundombinu ya Mahakama na mabadiliko ya sheria, inayoruhusu makubaliano ya kukiri kosa na kulipa faini ndiyo yamewezesha mashauri mengi ya jinai kumalizika kwa muda mfupi na kuwezesha haki  kupatikana kwa wakati,

‘‘Tumejikita kusikiliza mashauri haya kwa muda mfupi ili kutoathiri shughuli za uzalishaji na uwekezaji kupitia sheria hii, ambapo wahusika wakikiri makosa yao na kupata adhabu ya kulipa faini, alisisitiza.

Mahakama imekuwa ikisisitiza umuhimu wa mashauri kumalizika kwa wakati ili kutoa fursa kwa wananchi kushiriki kikamilifu katika shughuli za uchumi ambapo Kaulimbiu ya Maadhimisho ya  Wiki na Siku ya Sheria nchini mwaka huu  ni “Uwekezaji na Biashara: Wajibu wa Mahakama na Wadau kuweka Mazingira wezeshi ya Uwekezaji.’’

Akizungumzia maudhui hayo wakati wa kilele cha Wiki na siku ya Sheria nchini, Jaji Mkuu wa Tanzania, Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma alisema kuwa yanaweka wazi kwamba, sheria, utawala wa sheria, na mfumo wa utoaji haki kwa wakati ni nyenzo muhimu katika kufanikisha na kurahisisha biashara, uwekezaji, ukuaji wa uchumi na ustawi wa wananchi.

Hakimu Mkazi Mfawidhi  wa Mahakama  ya Hakimu Mkazi Geita, Mhe. Obadiah Bwegoge, akizungumzia uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama  katika Mahakama ya Hakimu  Mkazi Geita na Mahakama ya Wilaya ya  Geita, iliyorahisisha utoaji haki kwa wakati kama yalivyo maono ya Mahakama ya Tanzania.

 Kaimu Katibu Tawala wa Mkoa wa Geita, Bw. Herman Matemu akizungumzia uboreshaji wa miundombinu ya Mahakama ya Tanzania, Ofisini kwake Mjini Geita.

Mtumishi wa Mahakama ya Hakimu Mkazi Geita Bw. Sosteness Kiboga akimpa huduma mteja aliyefika Mahakamani hapo.

Picha ya Jengo la zamani lililokuwa likitumiwa na Mahakama ya Hakimu Mkazi, pamoja na Mahakama ya Wilaya ya Geita.

 Jengo la kisasa la Mahakama  ya Hakimu Mkazi Geita na Mahakama ya Wilaya ya Geita.






Hakuna maoni:

Chapisha Maoni