Na Lydia Churi- Dodoma
Jaji
Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis Juma amezitaka taasisi zote za utoaji
haki nchini kushirikiana katika mapambano dhidi ya vitendo vya rushwa ili zifanikiwe.
Akifungua
Kongamano la Wadau la kujadili mapambano dhidi ya rushwa katika mfumo wa utoaji
haki jijini Dodoma, Jaji Mkuu wa Tanzania amesema Kongamano hilo ni kielelezo tosha
cha ushirikiano wa taasisi za utoaji haki nchini katika vita dhidi ya rushwa.
Kwa mujibu wa Jaji Mkuu,
umuhimu wa kushirikiana katika vita dhidi ya rushwa ulitambuliwa mwaka 2003
wakati Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa lilipotunga Mkataba wa Kimataifa Dhidi ya
Rushwa (The United Nations Convention Against Corruption) ambao ulianza kufanya
kazi tarehe 14 Disemba mwaka 2005.
“Mkataba
huu uligusia ukweli kuwa Mhimili wa Mahakama hautafanikiwa katika vita dhidi ya
Rushwa endapo utasimamia vita hivyo peke yake bila kushirikiana na wadau na
taasisi nyingine”, alisema Jaji Mkuu.
Kuhusu
mapambano dhidi ya rushwa ndani ya Mahakama, Jaji Mkuu alisema mbinu nyingi
zimetumika ili kuibua na kupima mitizamo na hisia waliyonayo wananchi juu ya
vitendo vya rushwa. Baadhi ya mbinu hizo ni kuwekwa kwa mabango yanayopinga
rushwa katika Mahakama zote nchini, kujitathmini kupitia utafiti uliofanywa na taasisi
isiyo ya Kiserikali ya REPOA mwaka 2015 na 2019.
Akifafanua
kuhusu utafiti uliofanyika, Prof. Juma alisema ulijikita kwenye maeneo ya uridhishwaji
na huduma za Mahakama, upatikanaji wa taarifa muhimu za mashauri na huduma
zinazotolewa na Mahakama ya Tanzania.
Alisema
taasisi za utoaji haki hazina budi kuwasikiliza wananchi na kutoa nafasi ili
wananchi wazikosoe. “Tusiwazuie wananchi kulalamika kwa kuwa malalamiko yao
yanaweza kutufumbua macho kuhusu tatizo la rushwa lililojificha ndani ya
taasisi zetu”, alisisitiza Jaji Mkuu.
Kuhusu
maboresho, yanayofanywa na taasisi yoyote iliyo katika mfumo wa utoaji haki
Tanzania Jaji Mkuu alisema hayatokuwa na maana iwapo suala la rushwa katika
vyombo hivyo litafumbiwa macho na pale ambapo wananchi wanaofika mahakamani
kupata huduma hawatasikilizwa.
Awali
akitoa neno la utangulizi, Jaji Kiongozi wa Mahakama Kuu ya Tanzania Mhe. Dkt.
Eliezer Feleshi alisema jitihada
za Mahakama za kuandaa mijadala ya aina hii kwa kushirikiana na Chuo cha
Uongozi wa Mahakama Lushoto (IJA) pamoja na wadau wengine ni kielelezo dhahiri
cha dhamira ya dhati ya Mhimili huo katika kuhakikisha kuwa mapambano dhidi ya rushwa
yanakuwa endelevu na yanaleta matunda chanya.
Jaji Kiongozi alisema
rushwa haiathiri Mahakama peke yake bali mfumo mzima wa utoaji haki ndiyo
sababu Kongamano hilo limewashirikisha wadau wote wa utoaji haki ili kuweza
kujadili kwa mapana kwa vile malalamiko ya rushwa kutoka kwa wananchi
yanaelekezwa kwa wadau mbalimbali wa utoaji haki nchini.
Kongamano la wadau kujadili mapambano dhidi ya Rushwa katika Mfumo wa Utoaji haki limewakutanisha wadau wa utoaji haki jijini Dodoma kwa lengo la kujadili changamoto zilizopo, lakini pia mikakati iliyopo ya kukabiliana na rushwa nchini. Baadhi ya taasisi zilizoshiriki ni pamoja na Takukuru, BSAAT, Ofisi ya Mpelelezi wa Makosa ya Jinai (DCI), TLS, Wizara ya Mambo ya Ndani ya Nchi, Magereza, na Polisi.
Wadau wa Utoaji haki nchini wakiwa kwenye Kongamano la kujadili mapambano dhidi ya Rushwa lililofanyika jijini Dodoma. Pichani ni Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine.
Jaji Mkuu wa Tanzania Mhe. Prof. Ibrahim Hamis
Juma akifungua Kongamano la Wadau wa utoaji haki nchini kujadili mapambano dhidi ya Rushwa lililofanyika jijini Dodoma.
Wadau wa Utoaji haki nchini wakiwa kwenye Kongamano la kujadili mapambano dhidi ya Rushwa lililofanyika jijini Dodoma. Pichani ni Waheshimiwa Majaji Wafawidhi wa Mahakama Kuu ya Tanzania na Majaji wengine, Watendaji na Naibu Wasajili wa Mahakama.
Mtendaji Mkuu wa Mahakama ya Tanzania Bw. Mathias Kabunduguru (Katikati) na Msajili Mkuu Mhe. Wilbert Chuma (kushoto) wakiwa kwenye Kongamano la kujadili mapambano dhidi ya Rushwa lililofanyika jijini Dodoma.
Wadau wa Utoaji haki nchini wakiwa kwenye Kongamano la kujadili mapambano dhidi ya Rushwa lililofanyika jijini Dodoma.
Hakuna maoni:
Chapisha Maoni